Kisa Cha Bi Diams, Mwimbaji wa Ufaransa


Hiki ni kisa cha mwimbaji wa Ufaransa Bibi Diams na baada ya kusilimu alijiita Sakina na vipi amesilimu. Bibi huyu alikuwa anapenda sana kuwa pamoja na waalgeria na waafrika au kwa maana sahihi alikuwa akipenda kufuatana na wananchi wa kiislamum wa Algeria na waafrica. Alikuwa akiwaona wakiswali,  mpaka naye akajifunza kuswali na kusoma surat Al-fatiha na sura ya ikhlaasw. Si hivyo tu bali aliwaona wakitamka shahada, lakini kwa masikitiko anasema hakuna mtu ambaye aliniambia nisema hapana Mola apaswae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyeezi Mungu. Akimaanisha atamke shahada (Asilimu).

Siku moja akapata maradhi ya nafsi, alikuwa akihisi dhiki katika nafsi yake, bila kujuwa sababu gani, akaenda hospitali daktari akampa dawa, lakini maradhi yake yalizidi. Akaamuwa kuacha kutumia dawa hizo. Kisha miongoni mwa marafiki zake wa Algeria alimpa kitabu cha Qur'an kilicho tafsiriwa kwa lugha ya kifaransa kama zawadi, na hakumwambia kama hiki ni kitabu gani (yaani hakumwambia kama hii ni Qur'an tukufu). Isipokuwa alimwambia soma kitabu hiki utapona maradhi yako.

Bibi Sakina alichukuwa kile kitabu, akaenda katika kisiwa cha Morris katika Ufaransa na kukaa huko siku kumi katika hoteli akisoma kitabu hicho (Qur'an iliyo tafsiriwa kwa lugha ya kifaransa).

Baada ya kukisoma akasema haiwezekani aliye andika kitabu hiki au aliye kitunga ni mtu wa kawaida ni mtu Mtukufu. Akasema Kisha nikaanza kusoma kuhusu asili, na kuanza kutafakari kuhusu jua, mwezi, ardhi,  nyota na mvua. kikaniathiri sana. Nikawa nina jiuliza je maneno haya yaliyo andikwa ni maneno ya Mtume Swala Lwahu alayhi wasalam (na yeye alimjuwa Mtume Swala Lwahu Alayhi Wasalam kutokana na kufuatana na marafiki wa kiislamu watokao Afrika). Nikawa ninainuka usiku na kuomba ewe Mola wangu nijaalie nimuamini aliye andika kitabu hiki. Nilisoma kurasa 200 za Qur'an zilizo tafsiriwa kwa lugha ya kifaransa.

Nikaona hakuna kosa hata moja katika maneno haya. Nikajisemea haiwezekani kitabu hiki kikawa ni cha binaadamu, inawezekana aliye kiandika ni Mtume (Swala lwahu Alayhi Wasalam),  nikaanza kumpenda. Nikakuta kitabu hiki kinawataja manabii Sulaymaan na Issa ( Alayhimu Salaam).

Pia nikashangazwa kuona kwamba Waislamu wanamuamini Nabii Isa (Alayhi Salaam). Kila nilivyo soma nilizidi kupendezewa nacho, nikakisoma chote kwa uchache muda wa siku kumi. Nikasema haiwezekani haya yakawa maneno ya binaadamu, inaweza kuwa ni maneno ya Mwenyeezi Mungu, lakini Sikuweza kumwambia mtu maneno haya,  nikaanza kuhisi kwamba Mwenyeezi Mungu Mtukufu anazungumza nami, nikaanza kumuamini Mwenyeezi Mungu. Na kuhisi kwamba kuna makosa nimefanya katika maisha yangu. Nikaamuwa kuyamaliza yote haya na kuwa Muislamu wa asili. Kisha akasema nilipo soma nililia sana kwani ukweli uko. Na nilipo soma surati  Al-Mulk  nilipo fika katika kauli ya Mwenyeezi Mungu yenye maana ya kwamba:
 Aliye umba mbingu saba kwa matabaka. Huoni tafauti yoyote katika uumbaji wa Mwingi wa Rehema. Hebu rudisha nadhari! Unaona kosa lolote?
Surat Al-Mulk [67]: 3

Nikazichukulia aya hizi nikaanza kuangalia mbinguni, kweli hukuti kasoro, nikashangazwa sana. Kisha nikasoma katika sura hiyohiyo ayah yenya maana ya kwamba:
Tena rudisha nadhari mara mbili, nadhari yako itakurejea mwenyewe hali ya kuwa imehizika nayo imechoka.
Surat Al-Mulk [67]: 4

Nikayarudisha macho yangu kama alivyo amrisha Mwenyeezi Mungu kisha nikaendelea kuisoma sura hiyo na hapo nikagunduwa ukweli. Na hapo nikatangaza Uislamu wangu, kisha nikaenda kwa wazazi wangu na kumwaambia mama yangu kuwa mimi nimesilimu. Mama yangu hakupinga uamuzi wangu kwani mimi nilikuwa mgonjwa na Mwenyeezi Mungu ameniponyesha. Baada ya hapo nikavaa hijabu ya kawaida, na koti pana na suruali pana ili nisigundulike kama nimesilimu.

Kisha nikaondoka kwa muda wa miezi minane hakuna aliye juwa niko wapi. Nikawa ninaenda msikitini na nikavaa hijabu ya kisawa, lakini nikapigwa picha na mimi nikiwa nina enda msikitini na huku nimevaa hijabu. Kwani wengi walikuwa hawajuwi kama mimi nimesilimu. lakini baada ya kupigwa picha hiyo nikagundulika kama nimesilimu. Kukawa kuna maandiko katika magazeti kwamba wakristo waingia katika Uislamu (Wasilimu).

Baada ya hapo nikarudi kuimba, kwani nilikuwa sijui kama kuimba ni haramu. Lakini kabla ya kusilimu nilipo kuwa nikifanya sherehe nilikuwa daima nawaona wasichana saba mbele ya jukwaa, lakini baada ya kusilimu siku niliyo panda juu ya jukwaa kuimba sikuwaona wasichana wale. Kisha nikaangalia upande mwingine nikaona wasichana watatu wamevaa hijabu ambao ni miongoni mwa wasichana wale saba. Nilipo maliza kuimba wakaja na kuniambia kwamba sisi hatuwezi kuja kusikiliza nyimbo zako, kwasababu nyimbo ni haramu katika Uislamu. Na kwamba wao wamesilimu na wasichana wale wenzao wengine pia wamesilimu.

Akasema nikarudia kuisoma tena Qur'an ili nihakikishe kama kweli nyimbo ni haramu au laa, nikakuta aya katika surati Luqmaan yenye maana ya kwamba:

Na miongoni mwa watu wapo wanao nunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipo kujua, na wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha
Surat Luqman [31]: 6

Hapo nikagunduwa kwamba nyimbo ni haramu nikatubu kwa Mwenyeezi Mungu na kuacha kuimba. Kwani kabla ya hapo nilikuwa sijui kwamba nyimbo ni haramu. Nikalazimishwa kulipa fidia ya kuacha kuimba nikakubali nikawalipa.

Baada ya hapo Bibi Sakina akaelezea kuhusu hisia zake kwa kusema: Nilipo kuwa mwimbaji watu walikuwa wakinipa zawadi lakini baada ya kusilimu hawakunipa tena. Lakini Mwenyeezi Mungu amenitajirisha kuliko kwa walivyo kuwa wakinipa. Kwani watu wanataka nivuwe hijabu yangu kwani nimeleta picha mbaya kwa kila mkristo. Kwani sisi katika nchi yetu hii ya Ufaransa hawataki tuwe Waislamu na waumini wa kweli tufuatao sheria za dini ya kiislamu, bali wanataka kuwa Uislamu uwe ni kama maneno au kwa maana sahihi tuwe Waislamu jina. Na Mwenyeezi Mungu Mtukufu anasema kwa maana ya kwamba:

Mayahudi hawawi radhi nawe, wala Wakristo, mpaka ufuate mila yao. Sema: Hakika uwongofu wa Mwenyezi Mungu ndio uwongofu. Na kama ukifuata matamanio yao baada ya ujuzi ulio kwisha kujia, hutapata mlinzi wala msaidizi kwa Mwenyezi Mungu
surat Al-Baqara [2]: 120

Akaendelea kusema katika nchi za Magharibi kila kilicho haramishwa na Mwenyeezi Mungu kiko kama zina, uasherati, riba,  ulevi nk. Na kwa mtu ambaye hanywi pombe si mtu wa kawaida. Yaani hakuendelea. Na ndoa haitiliwi umuhimu,  na mtu anaye amuwa kufunga ndoa kesha kuwa mzee.

Baada ya hapo Sakina aliolewa na mwanamume wa kiislamu kutoka Morocco, akaenda Makkah Mukarramah kuchukuwa umra. Alipo fika katika maeneo matakatifu alikutana na baadhi ya waandishi wa habari ambao walimuuliza kuhusu ndoto zake ? Alisema nina tamani kuhamia Makkah na Madinah kwani ni sehemu bora kuliko zote ulimwenguni.

Alipo ulizwa kuhusu Mwenyeezi Mungu Mtukufu alisema. Mwenyeezi Mungu ndiye aliye niumba, na ndiye atakaye nifisha,  na ndiye aliye niongoza. Kabla ya kusilimu kwangu sikuhisi nilikuwa nina upendo, baada ya kusilimu kwangu nimekuwa nina penzi kubwa nalo ni kumpenda Mwenyeezi Mungu Mtukufu.

Mwisho akasema nina tamani Mwenyeezi Mungu anighufirie dhambi zangu, zilizo tangulia na zijazo na kunipa ithibati katika dini ya kiislamu. na kutuomba sote tumuombee Mwenyeezi Mungu ampe ithibati katika Uislamu.

Kisa hiki cha Diams au sakina na jinsi alivyo silimu. Na inapasa kutowa takbira kwa kusilimu kwake na tujiulize ni wangapi ambao bado hawajasilimu? Na wangapi ambao wanahitaji kutoka kwetu maneno mazuri na vitendo vizuri ili waongoke na kusilimu? Je tumeipa nini dini yetu? Je tumefanya jambo gani ili kuineza dini yetu? Je tume jitolea roho zetu na miili yetu kuinusuru dini yetu? Ninaapa ndugu zangu katika imaani Mwenyeezi Mungu ametupa neema kubwa, na kutufungulia Nyanja nyingi za kuhudumia dini hii. Na miongoni mwa hizo ni kutumia mtandao wa internet kama njia ya kutowa daawa, si hivyo tu hata kwa njia za simu ya mkononi (sms) badala ya kutuma message za kawaida tufanye ziwe njia ya daawa.

Na jambo la kushangaza kwa Bibi huyu huvaa jilbaab anapo toka. Si kama wasichana wengi wa sasa ambao hupenda kuvaa abaya zenye mapambo au za kubana na kufuata mitindo mipya ya abaya inayo toka kila siku. Mko wapi enyi wasichana wa kiislamu. Mna mfuata shetani ambaye anataka kukuwekeni mbali na Mwenyeezi Mungu.

Ikiwa Sakina alikuwa ni mkristo na mwimbaji mashuhuri, ameacha yote hayo baada ya kusilimu. Vipi wewe usema kwamba siwezi kuishi bila ya nyimbo?! Wala bila ya umaarufu?

Unajuwa kwanini Sakina hakusema yote hayo? Kwa sababu yeye ameonja utamu wa imani na utamu wa kuwa karibu ya Mwenyeezi Mungu na utiifu.

0 comments/Maoni: