Uislam


Nini maana ya Uislamu, maana ya Neno Allah, asili ya Mwanaadamu; uhusiano kati ya mja na Muumba wake na nafasi ya Mwanaadamu hapa Ulimwenguni.

Uislamu  
Kumekuwa na maeleweko potofu juu ya maana ya Uislamu, hivyo ni vema kusahihisha hapa. Kiistilahi, neno Islam halinasibiani na mahali mahususi, kabila au Taifa fulani. Kwa hakika ni makosa na kejeli kuuita Uislamu kuwa ni dini ya Muhammadiya (Mohamedanism) kama inavyoeleweka Amerika ya Kaskazini yote na Ulaya. Makosa hayo yanatokana ukweli kwamba kiini cha mafundisho ya Uislamu hakitokani na mtu kama ilivyo kwa itikadi ya umaksi unaotokana na mwasisi wake Karl Marx au itikadi nyingine mfano wa hiyo. 
Mtume Muhammad (s.a.w.) haabudiwi na Waislamu na pia yeye binafsi si mwanzilishi wa Uislamu wala si mtunzi wa kitabu kitakatifu, Qur’an.

Neno Islam linatokana na kiini (SLM) au Salam, ambayo maana yake ni amani au kujisalimisha. Kwa hiyo kimaana, neno Uislamu (Islam) ni kule kupatikana amani ya ndani na nje kunakotokana na kujisalimisha kwa Muumba (s.w.). Kwa maana nyingine Uislamu ni kufuata mwenendo mwema unaozingatia maelekezo ya Muumba.

Nini kujisalimisha? Ni kuwa hadhiri (mtambuzi), mtiifu na mnyenyekevu kikamilifu katika kufuata maamrisho ya Allah, kukiri utukufu wake na pia kufuata njia yake.

Kwa maana hiyo, Waislamu huitakidi kuwa Uislamu ndio ujumbe uliofundishwa na Mitume wote katika historia ya Mwanaadamu.

Uislamu si itikadi iliyozushwa na Muhammad mnamo karne ya saba miladia. Bali kuja kwa Muhammad ni ukamilisho wa ujumbe wa Allah kwa wanaadamu wote.

Lazima ifahamike hapa kwamba kutokufahamika ukweli huu juu ya Uislamu ndio sababu kuu inayohatarisha uwezekano wa majadiliano baina ya Waislamu na wasio Waislamu. Wasio Waislamu, na hapa wanamaanishwa Wakristo, kwa upande wao wanautazama Uislamu kama ni itikadi mpya iliyozushwa na Muhammad.

Allah, na imani ya Uungu 
Nini maana ya Neno Allah?
Neno Allah halimaanishi Mungu wa jamii, kundi, kabila, Waarabu au Mungu wa Waislamu. Hatuna rejea nyingine inayoweza kutupa maana halisi ya neno Allah zaidi ya Qur’an ambayo ilishushwa (Revelation) kwa Kiarabu, lugha ambayo ndiyo kiini cha neno hilo.

Katika Lugha ya Kiarabu neno Allah maana yake ni Mungu mmoja, wa kweli, na wa Walimwengu wote. Kwa mfano iwapo tutamfikiria Allah ni tofauti na Mungu Mwenyezi basi pia tutapaswa kukubali kuwa Wafaransa Wakristo wanaabudu Mungu mwingine minghairi ya God kwa G kubwa, kwa sababu wao humwita Dieu katika lugha yao.

Kwa hiyo kuielewa maana halisi ya Neno Allah hatuna budi kuangalia baadhi ya sifa zake. Qur’an imetaja majina matukufu ya Allah, ambayo pia ni sifa zake. Hapa tutarejea sifa chache miongoni mwa hizo. 
Baadhi ya sifa za Allah zinatilia mkazo uwezo usiomithilishwa alionao Allah. Qur’an inatufahamisha kwamba Allah yuko juu ya ufahamu wetu wenye ukomo. 
"Hakuna chochote mfano wake; naye ni mwenye kusikia, mwenye kuona (42:11). 
Macho hayamfikii (kumwona), hali yeye anayafikia macho. Naye ni mwenye kujua yaliyofichikana na yaliyodhahiri.
Q 6:103

Kwa hiyo Muislamu hamuelewi Allah kwa taswira fulani mahususi iwe ya mtu, kitu, kiumbe au chochote kile. Kwa lugha nyepesi Allah amekienea kila kitu hata kile kisichoweza kuonwa na jicho la mwanaadamu, anakijua kila kitu hata vile visivyoweza kudirikiwa na milango yetu ya fahamu. Kuhusu sifa hii ya Allah, Qur’an inatufahamisha: 
Je! Huoni kwamba Allah Amteremsha maji kutoka mawinguni, na ardhi inakuwa chanikiwiti? Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kujua yaliyofichikana na mwenye kujua yaliyodhahiri.
Q22:63

Zipo sifa kadhaa zinazokazia utukufu wa Allah, kwamba yeye ni mjuzi wa kila kitu, kwamba ni wa milele na kwamba ndiye mwenye kudura, muadilifu na mtawala wa kila kitu. Pamoja na mkazo huu juu ya sifa za Allah, hata hivyo hiyo haina maana kwamba kwa Muislamu Allah ni wazo tu la kifalsafa, tafsiri au Mungu aliyembali kabisa na waja wake. Sambamba na kukazia utukufu wa Allah Qur’an vile vile inaeleza katika aya ya kwanza kabisa: 
Kwa jina la Allah Mwingi wa Rehma Mwenye Kurehemu.
Q1:1

Kwa hiyo kwa Muislamu, Mungu mmoja haina maana ya umoja katika Uungu. Fikra ya Umoja katika Uungu haikubaliki katika Uislamu kwa sababu imebeba dhana ya nafsi tofauti katika umoja huo (kama Baba, Mwana na Roho Mtakatifu).Uislamu unasisitiza Tawhiid au umoja na upweke wa Allah na unaipinga fikra ya umoja katika Uungu au nafsi tatu tofauti zinazoshirikiana katika Uungu.

Kinyume na upweke wa Allah, ni shirki, yaani kumpa washirika Allah (s.w.) ambako ni pamoja na kuwaitakidi Waungu wengi au wawili. Shirki vile vile inajumuisha fikra kwamba Mwenyezi Mungu yumo ndani ya kila kitu.

Aina zote za falsafa za Mungu anayewakilishwa kiumbile, zinapigwa vita na dhana ya Mungu mpweke katika Uislamu. Utii wa kibubusa kwa madikteta, wafalme au matashi binafsi ni sehemu ya kumjaalia Allah wenza hivyo ni shirki.

Kwa Muislamu, umoja wa Mungu (Tawhiid) haumaanishi kufuata kiupofu. 
Utakasifu, utukuzo na mkazo juu ya fikra ya Mungu mmoja umepindukia maoni, mtazamo au imani, ni jambo lililozama katika kina kirefu chenye athari kubwa katika maisha ya kila siku. 
Mtazamo huu juu ya Allah ni muhimu sana ufahamike na wasio Waislamu kabla ya kujiingiza katika majadiliano ya aina yoyote ile.

Mwanaadamu 
Nani Mwanaadamu? Nani wewe na nani mimi? Kwa nini tupo hapa katika ardhi. Haya ni maswali muhimu sana, hasa baada ya kutoa maelezo juu ya Allah. Kumzungumzia Mwanaadamu kwa kumuhusisha na Allah (s.w.) ni eneo jingine linalohitaji kufahamika vyema ili kuifanya midahalo kati ya Waislamu na wasio Waislamu, hasa Wakristo, iwe yenye maana.

Qur’an inatufahamisha kwamba sisi Wanaadamu tumeumbwa kwa vitu vitatu. Kwanza, tumetokana na udongo ambao unawakilisha umbile la mwili. Pili, tumetunukiwa akili na kipawa cha kufikiri (Intellect) ambacho hakina budi kutumiwa na Mwanaadamu.

Akili inaweza kuwa si toshelevu lakini vile vile si kikwazo cha imani. Na tatu, tumepuliziwa roho inayotokana na Allah: 
Ambaye ametengeneza umbo la kitu, na akaanzisha umbo la mwanaadamu kwa udongo.
Q32:7

Katika aya nyingine Allah analiweka wazi zaidi hili kwa kutufahamisha:- 
"Na (kumbuka) Mola wako alipowaambia Malaika, "Hakika Mimi nitamuumba mtu kwa udongo mkavu unaotoa sauti, wenye kutokana na matope meusi yaliyovunda." 
"Basi nitakapomkamilisha na kumpulizia roho inayotokana na Mimi, basi mumwangukie kwa kumtii.
Q15:28-29

Kwa hiyo, Muislamu hayaoni maisha ya Mwanaadamu hapa ardhini kama ni adhabu iliyotokana na wazazi wetu wawili Adamu na Hawa kula tunda la mti uliokatazwa. Bali tukio hilo kihistoria linaitakidiwa kuwa ni fundisho kwa Adamu na Hawa kabla ya kuletwa hapa duniani. Hili ni eneo jengine lenye ukinzani. 
Qur’an inafundisha kwamba hata kabla kumuumba mtu wa kwanza, Allah (s.w.) alikusudia kuanzisha maisha na ustaarabu wa kiumbe huyu hapa ardhini. 
"(Wakumbushe watu khabari hii) wakati Mola wako alipowaambia Malaika: "Mimi nitaleta khalifa katika ardhi.".
Q2:30

Hii ina maana kwamba Muislamu haikubali dhana ya dhambi ya asili iliyorithiwa kutoka kwa wazazi wao kwa kuasi amri ya Mwenyezi Mungu ya kutokula tunda la mti uliokatazwa.

Allah amemuumba mtu ili aje kuwa Khalifa; mdhamini au mwakilishi wa Allah katika ardhi. Dhamana aliyobeba Mwanaadamu na jukumu lake kwa kujumla kwa Muumba (Allah) ni kumuabudu.

Ibada kwa Muislamu haikomei katika kutekeleza kaida fulani fulani (rituals). Ibada katika Uislamu ina tafsiri pana; ni kuiendea shughuli yoyote yenye manufaa kwa mtu binafsi au jamii kwa ujumla kwa mujibu wa maelekezo ya Allah (s.w.).

Kwa maana hii, Muislamu anaitazama ardhi, mazingira na rasilimali zake kama ni neema kutoka kwa Allah kwa Mwanaadamu ambayo anapaswa kuitumia ili kufikia utimilifu wa amana (lengo) atakayowajibika kwayo mbele ya Muumba. Hii ndiyo sababu kubwa Qur’an kusisitiza kusoma, kama inavyojitokeza katika Wahyi wa kwanza:

"Soma kwa jina la Mola wako Aliyeumba. Soma na Mola wako ni karimu sana. Ambaye amemfundisha (Binaadamu) kwa wasitu wa kalamu. Amemfundisha Mwanaadamu mambo aliyokuwa hayajui".
Q96:1-5

Hivyo, kwa kuwa Waislamu huko nyuma walikuwa na yakini juu ya imani yao, na juu ya maamrisho ya Qur’an kuhusu kusoma, walianzisha na kusimamia ustaarabu na taaluma za sayansi zilizopea. Walirithishana na kuziboresha hazina hizo ambazo baadaye zikaja kuwa cheche za mwamko wa Ulaya. Tungependa kusisitiza hapa kwamba iwapo Waislamu wa zama hizi watakuwa wakweli katika imani yao, historia ile itajirudia.

Wale wote woga hawako tayari kulipokea dai hili na kwa hiyo wanaogopa mdahalo na hilo linathibitisha utukufu wa Uislamu. Bila shaka ndilo umbile aliloumbiwa kwalo Mwanaadamu:

"Basi uelekeze uso wako katika dini iliyo sawa sawa - ndilo umbile Mwenyezi Mungu alilowambia watu. Hakuna mabadiliko katika maumbile ya viumbe vya Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo dini iliyo ya khaki lakini watu wengi hawajui.
Q30:30