Haki za binadamu kwa mujibu wa Qur'an

"Na kwa (ajili ya kuleta) haki (ulimwenguni ndio) tumeteremsha, na kwa haki imeteremka. Na hatukukuleta ila uwe mtoaji wa khabari njema na muonyaji"
Q 17:105

Kwa muda wa karne zisizopungua tano kabla ya kuzaliwa Yesu (a.s), Wanafalsafa wa kale walilumbana kuhusu maana ya Haki. Historia inabainisha kuwa wanafalsafa hao walielewa wajibu wa Haki kwa kila mwanaadamu, lakini nini maana ya haki, ipi na kwa msingi upi iwe Haki, likabaki kuwa suala la mjadala na ukinzani baina yao kwa karne hizo.

Kwa mfano:
Aristotle anasema '...hatuwezi kuifasiri haki kwa kuwa hakuna haki duniani.

Socrates
huko nyuma alisema '...ni haki kwetu kuzitii sheria tulizojiwekea.
Plato
nae ana yake aliyosema kuhusu haki na sheria.

Katika Uislamu Haki ni muungano wa, au mfumo wa sheria na maadili unaolenga kuiweka jamii katika murua ili kupatikane amani, furaha na mahusiano mema katika maisha ya waanadamu. Sheria hapa inajaribu kuoanisha maslahi ya mtu binafsi na yale ya jamii aishiyo.

Kwa hakika Haki ndicho kiungo kinachoweza kuiunganisha jamii na kuiweka katika hali ya udugu, ambapo kila mwanajamii anakuwa mlinzi wa wengine na huwajibika kikamilifu katika ustawi wa jamii hiyo. Kwa ufupi Haki katika Uislamu inafasiriwa kama ni utaratibu wa kukiweka kitu mahali au katika njia ya sawa na kutimiza majukumu binafsi na ya kijamii pasipo chuki wala upendeleo huku yakizingatiwa maelekezo ya M'Mungu Muumba (s.w).

Mwanaadamu yoyote, akiwa wa nchi moja au wa nchi nyingine, akiwa mkazi wa kijijini au wa mjini, akiwa mfalme au raia, akiwa Muumini au kafiri, kwa vyovyote vile atakavyokuwa, maadamu yeye ni mwanaadamu anastahiki kupata Haki za kimsingi ambazo ni wajibu kwa kila Muislamu kuzitambua na kuzisimamisha. Haki zenyewe za Kimsingi zinazohusu wanaadamu wote ni hizi zifuatazo:-
  • Haki za Kuishi (maisha)
  • Haki ya Usalama wa maisha
  • Haki ya kupata mahitaji ya lazima ya maisha.
  • Haki ya Uhuru (Kila mtu kuwa huru)
  • Haki ya kulinda maadili.
  • Haki ya Uadilifu katika hukumu.
  • Haki ya Usawa.
Kila mwanaadamu awe muumini au kafiri anastahiki kupata haki hizi za msingi kwa sababu ndizo zinazofanya kuwezekana kwa maisha ya mwanaadamu hapa ulimwenguni kwa mujibu wa umbile lake:

Na aliposema Ibrahimu:
"Ee Mola wangu! Ufanye mji huu uwe wa salama uwape na wakazi wake matunda(mahitaji ya lazima); wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho."(Mwenyezi Mungu) akasema: Na mwenye kukufuru(pia) nitamstarehesha...
Q 2:126

Na imefardhishwa (lazima) kwa waumini kuendesha harakati za kijamii mbali ya kuhakikisha mwanaadamu anatawaliwa kwa sheria ya Muumba bali pia inapotokezea watu kudhulumiwa haki hizi kwa hila au mbinu yoyote ile iwe ya kisiasa, kijeshi au kifalme. Ibada zote za kiroho zinalenga kwenye kupigania na kusimamia haki hizo. Swala au ibada yoyote ya kiroho ifwanyayo na muislamu haina maana yoyote iwapo jamii aishiyo dhulma na ukandamizaji vimeshitadi na hana jitihada yoyote anayoichukuwa kusimamisha haki za kimsingi. Watu wanapouwawa bila ya haki au wanapokufa kwa njaa, kukosa matibabu mazuri kwa magonjwa mbalimbali na mazingira machafu na vilevile wanapokoseshwa uhuru, wanapodhulumiwa haki zao katika mahakama, kubaguliwa na kunyanyaswa, dhima(lawama) ya hayo yote inarejea kwa waumini. Hebu tuziangalie kwa ufupi ufupi haki hizo:

Haki ya Kuishi (Maisha).
Kila mtu pasina ubaguzi wa aina yoyote ana haki ya kuishi na kulindwa maisha yake. Kumuua mtu yeyote awaye ni kosa la jinai na muuaji ni lazima ahukumiwe. Makemeo ya Qur'an kuhusu kosa hili yanadhihirisha kwa uwazi ubaya wa kumuua mtu yoyote pasi na haki:

Kwa sababu ya hayo tukawaandikia wana wa Israil ya kwamba atakayemuua mtu bila ya yeye kuua mtu, au bila ya kufanya fisadi katika nchi; basi ni kama amewaua watu wote...
Q 5:32

"... Wala msimuue mtu ambaye Mwenyezi Mungu ameharamisha (kuuawa) ila ikiwa (imetokea) haki (ya kuuawa)..."
6:151

Hukumu ya muuaji aliyekusudia ni kuuawa kama inavyobainishwa katika Qur'an:

Wala msiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameiharamisha kuuawa isipokuwa kwa haki (Akahukumu hakimu wa Kiislamu kuwa mtu amestahiki kuuawa na akatoa amri ya kuuawa), nani mwenye kuuawa kwa kudhulumiwa, basi tumempa nguvu mrithi wake (juu ya muuaji huyo, akitaka ataomba kwa hakimu kuwa amuue au akitaka amtoze fidia au akitaka (amsamehe).
Q 17:33

Haki ya Usalama wa Maisha.
Kila mtu anayo haki ya kuokolewa au kupata ulinzi utakaomuweka katika hali ya usalama bila ya ubaguzi wa aina yoyote. Tunafahamishwa katika Qur'an kuwa:

"... Na mwenye kumwacha mtu hai (kumsaidia kuishi) ni kama amewaacha hai watu wote..."
5:32

Kila mtu awe mgeni au raia ana haki ya kupata mahitajio muhimu ya maisha yatakayomuwezesha kuishi, na kila mtu anayo haki ya kupata hifadhi itakayomuhakikishia kuishi kwa usalama. Ni katika makosa makubwa mtu kunyimwa haki ya usalama kwa sababu ya kabila, ukoo, rangi, taifa au dini. Ukandamizaji wa sura yoyote ile ni dhambi ambayo katika historia ya mwanaadamu imekuwa sababu mojawapo ya kutumwa mitume:

"Tunakusomea habari za Musa na Firauni kwa (njia ya ) haki kwa ajili ya watu wanaoamini."
Tunakusomea khabari za Musa na Firauni kwa Haki kwa ajili ya watu wanao amini. Hakika Firauni alitakabari katika nchi, na akawagawa wananchi makundi mbali mbali. Akalidhoofisha taifa moja miongoni mwao, akiwachinja watoto wao wanaume na akiwaacha watoto wao wanawake. Hakika yeye alikuwa katika mafisadi. Na tukataka kuwafadhili walio dhoofishwa katika nchi hiyo na kuwafanya wawe waongozi na kuwafanya ni warithi. Na kuwapa nguvu katika nchi, na kutokana na wao kuwaonyesha kina Firauni na Hamana na majeshi yao mambo yale waliyo kuwa wakiyaogopa.
Q 28:3-6

Haki ya kupata mahitaji ya lazima ya maisha

Kila mtu ana haki ya kupata mahitaji ya lazima kama vile chakula, malazi, mavazi, matibabu, elimu, nakadhalika, bila ubaguzi wowote ule uwe wa rangi, dini, kabila, au utaifa. Ni wajibu wa serikali kuhahakisha kila mwanajamii anapata mahitaji haya ya lazima, isipotekeleza wajibu huo ni halali kuondolewa madarakani kwa njia yoyote ile. Kibinafsi wale wasio na uwezo wa kujikimu mahitaji hayo ni jukumu la wenye uwezo kuwasaidia:

"Na ambao katika mali zao iko sehemu maalumu. Kwa ajili ya aombaye na anayejizuilia kuomba (japo mahitaji)."
Q 70:24-25

Qur'an inatuamrisha kwamba, kama mtu anao uwezo na mtu mwingine akamuomba msaada au hata kama hajamuomba lakini anajua kuwa anahitaji msaada ni wajibu wake kumsaidia. Mwenyezi Mungu (s.w.) amepitisha riziki ya mja wake huyo kupitia kwa mwenye uwezo.

Haki ya Uhuru

Ili kuhakikisha kuwa kila mtu anakuwa huru na hawi mtumwa wa mwingine kimabavu au kifikra, Uislamu umeliweka suala la mamlaka au utukufu kwa Mwenyezi Mungu (s.w.). Uislamu umeharamisha kitendo cha kumfanya mtu huru kuwa mtumwa au kumuuza kwenye masoko ya watumwa. Kuhusu habari hii Mtume Muhammad (s.a.w.) anatuambia kama yafuatavyo:

"Kuna watu wa aina tatu ambao Mimi mwenyewe nitasimama kuwashitaki katika Siku ya Hukumu (Siku ya Hesabu), miongoni mwa hao ni yule anayemfanya mtu huru kuwa mtumwa na kumuuza..." (Bukhari).

Maneno haya ya Mtume (s.a.w.) yanawahusu wanaadamu wote bila ya kujali utaifa wao, rangi zao, dini zao na kadhalika. Hata hivyo kumekuwa na propaganda kuwa Uislamu ndio ulioeneza utumwa na nchi za Magharibi ndizo zilizokuja kukomesha utumwa. Pamoja na madai kwamba ni nchi za Magharibi zilizokuja kukomesha utumwa baada ya nusu ya karne ya 19 lakini watu hao hao kabla ya wakati huo ndio walioivamia Afrika na kuwateka Waafrika waliokuwa huru, wakawafunga na kuwasafirisha kwenye makoloni yao kama vile Amerika, Australia na New Zealand. Waafrika hawa waliotekwa na kufanywa watumwa walifanyiwa vitendo vya ukatili mno; kuliko wanyama.

Haki ya Kulinda maadili.

Ili kuhakikisha kuwa jamii inaishi katika mwenendo mwema na kuondokana na mifarakano, imesisitizwa kuwa anapata hifadhi ya kutoguswa na mwanamume yoyote awaye nje ya utaratibu wa ndoa, kitendo cha zinaa au kishawishi chochote cha zinaa kimekatazwa katika Uislamu bila ya kujali kuwa kimefanywa na Muislamu au na asiye Muislamu, kimefanywa na raia au mgeni. Makemo ya Qur'an juu ya kitendo hiki ni haya yafuatayo:

Wala msikaribie zinaa. Hakika hiyo ni uchafu na ni njia mbaya kabisa.
Q 17:32

Uzinifu katika Uislamu ni kosa la jinai na mzinifu yeyote anastahiki adhabu kali ya kupigwa viboko mia moja. (Qur'an, 24:2) au kupondwa mawe mpaka kufa bila ya ubaguzi wa aina yote (Kwa ambaye alishawahi kuoa).

Haki ya Uadilifu katika Hukumu

Ili kusimamisha uadilifu, kila mtu bila ya kujali dini yake, rangi yake, taifa lake, uraia wake (n.k.), anastahiki kuhukumiwa kwa uadilifu. Uadilifu katika kutoa hukumu( (Right to Justice) unasisitizwa mno katika Uislamu kama tunavyojifunza katika Qur'an:

Enyi mlioamini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu, mtowapo ushahidi kwa ajili ya Allah, ijapo kuwa ni juu ya nafsi zenu, au wazazi wawili na jamaa zenu. Akiwa tajiri au masikini Allah Anawastahikia zaidi. Basi msifuate matamanio, mkaacha kufanya uadilifu. Na mkiupotoa au mkajitenga nao basi Allah Anajua vyema mnayo yatenda”
Q 4:135

Enyi mlioamini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Allah mkitoa ushahidi kwa haki. Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchamngu. Na mcheni Allah. Hakika Allah Anazo khabari za mnayoyatenda.
Q 5: 8).

“Enyi watu! Kwa hakika Tumekuumbeni (nyote) kwa (yule) mwanamume (mmoja; Adam) na mwanamke (mmoja; Hawwa). Na Tumekufanyeni mataifa na makabila (mbali mbali) ili mjuane (tu basi; siyo mkejeliane). Hakika ahishimiwaye sana miongoni mwenu mbele ya Allah ni yule amchaye Allah zaidi katika nyinyi. Kwa yakini Allah ni Mjuzi, Mwenye habari (za mambo yote)”
Q 49: 13).

“Hakika Allah Anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe. Na mnapo hukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Hakika haya anayo kuwaidhini Allah ni mazuri sana. Hakika Allah ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kuona”
Q 4: 58).

“Hao ni wasikilizaji kwa ajili ya kusema uwongo, na ni walaji mno vya haramu! Basi wakikujia, wahukumu baina yao au jipuuze nao. Na ukijipuuza nao, basi wao hawatakudhuru kitu. Na ukiwahukumu, basi hukumu baina yao kwa uadilifu. Hakika Allah Anawapenda waadilifu”
Q 5: 42)

0 comments/Maoni: