NADHARIA YA EVOLUSHENI (EVOLUTION THEORY)

Kabla sijaingia katika mada hii, kwanza kabisa hatuna budi kuelewa kitu kimoja. Nacho ni elimu ya Sayansi (science). Baada ya hapo ndipo tutakuja kuangalia Nadharia ya Evolusheni (Evolution theory). Nadharia ambayo ni maarufu sana mashuleni na kwenye asasi za elimu.Sayansi maana yake ni Elimu au ujuzi unaotokana na maarifa ya uchunguzi unao randana na majaribio na vipimo mbalimbali vya kinadharia na vitendo. Kwa maana hiyo basi elimu hii ni muhimu sana kwa maisha ya binadamu tangu enzi za mwanzo kabisa za kuwepo kwake mwanadamu. Kwa maana hiyo kwa ufupi tunaweza kusema kuwa Elimu ya Sayansi ni ujuzi na maarifa ya kukabiliana na mazingira ya dunia yetu hii. Kutokana na hayo basi ndio maana kukajitokeza wanasayansi mbalimbali wenye ujuzi wa kinadharia na vitendo. Miongoni mwao ni Bwana huyu mwenye uraia wa kiingereza ajulikanaye kwa jina la Charles Robert Darwin.

Kutokana na historia ya kimagharibi kutofautiana na imani za kidini, na maendeleo ya elimu mbali mbali za Sayansi, wanasayansi wengi ambao wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kutafiti vitu mbalimbali katika elimu, wakajikuta wanatengwa na makasisi na watawa wa kidini hususani dini ya kikristo. Kwa kuelezwa kuwa wanakwenda nje ya imani ya kidini na wanakufuru Mungu. Kwa hali hiyo wakajikuta wanasayansi wengi wakiteswa ama kutengwa au wakiuwawa kwa sababu ya tafiti zao. Na hali hiyo ikapelekea wanasayansi wengi wa kimagharibi kuwa na upeo mdogo sana au kutokuelewa kabisa elimu ya kumjua Muumba wao. Na hii si kwa matakwa yao bali ni kutokana na kutengwa na kanisa. Kutokana na kutengwa huko, wanasayansi wengi wakawa si wenye kujihusisha na wala hawakuihusisha elimu yao wala uvumbuzi wao na suala la kuwepo kwa Mwenyezi Mungu. Na ndio maana Ugiriki ya kale (Ancient Greece), iliyokuwa na wanasayansi mbalimbali na kwa bahati mbaya ilikuwa na miungu wengi wa kuabudiwa, na hii ikapelekea wavumbuzi wengi kuwa wapagani, kwani wengi wa wanasayansi hao hawakujua ni Mungu gani hasa wa kuabudiwa. Na huku ndipo kulikoanzishwa elimu hii ya nadharia ya evolusheni. Elimu hii ilipokelewa na wanasayansi mbalimbali, mmoja wao ambaye ni maarufu sana ni huyu tuliyemtaja hapo juu Bwana Charles Robert Darwin. Lakini mwanzilishi haswa wa farsafa hii ni mwanabailojia wa kifaransa ajulikanae kwa jina la Jean Baptiste Lamarck. Mwanabaiolojia huyu katika moja ya kazi zake, aliwahi kueleza kuwa Twiga anatokana na mnyama ajulikanaye kwa jina la Paa au Palahala. Paa huyu kutokana na tamaa zake za kutaka kula majani machanga yatokanayo na miti iliyo mirefu, akajikuta ni mwenye kujitahidi kurefusha shingo yake ili kufikia majani yaliyo nchani, jitihada zake hizo zikapelekea kizazi chake kidogo kidogo wakawa ni wenye kuwa na shingo ndefu. Na hii ni baada ya miaka mingi sana kupita. (French biologist in his Zoological Philosophy 1809). Mtetezi mwingine aliyefuatisha mawazo yake ni huyu Charles Robert Darwin. Na ndiye aliye iendeleza elimu hii ya evolusheni, mpaka kufikia hapa ilipo. Na imempatia umaarufu sana katika elimu za kimaumbile. Mwingereza huyu ambaye alitumia miaka takribani mitano, akikusanya masalia (Fossils) ya wanyama wa baharini na nchi kavu, na kuyafanyia utafiti mnamo miaka ya 1859. Akaandika kitabu kiitwacho Chimbuko la Viumbe. (The Origin of Species). Nadharia hii imekuwa maarufu sana na kupigiwa debe na wanasayansi mbalimbali, pamoja na wanasiasa wakishirikiana na vyombo vya habari vya kimagharibi na kufundishwa mashuleni. Katika kitabu chake hiki, mwananadharia huyu ameelezea chimbuko la viumbe mbalimbali akiwemo mwanadamu. Mwanadamu ambaye kwa mujibu wa utafiti wake, amemgawanya sehemu takribani nne na amepitia vipindi mbali mbali vya kimaendeleo mf: zama za mawe, zama za shaba zama za chuma(The Stone Age, Bronze Age and Iron Age). Na pia mwanadamu anatokana na Nasaba zipatazo nne nazo ni:

**Australopithecus Robustus (Zinjathropus), aina ya Manyani. Halafu akabadilika kuwa Homohabilis na baadaye kuwa Homoerectus na Mwisho kabisa ni huyu binadamu wa sasa ambaye anaitwa Homosapien. Na kabla ya kuwa Zinjathropus. Binadamu alitokea baharini kwa bahati nasibu. Alianzia na kiumbe mmoja dhaifu sana, aliyekuwa na chembe hai moja. Ambaye alipitia mabadiliko mengi na kwa miaka mingi sana. Kutoka kuwa kiumbe mwenye chembe hai mmoja na kuwa aina ya jamii ya Pweza na kubadilika kuwa jamii ya Chura na kisha kuwa jamii ya Mjusi na kuwa jamii ya Manyani kabla ya kubadilika kuwa binadamu huyu wa sasa. Na kutokana na mazingira aliyopitia yaani kwa kiingereza ni kutokana na Natural Selection kwa kiswaili ni uwezo wa wanyama kuishi ama kutoweka kwa mujibu wa uwezo wao wa kubadilika kufuatana au kulandana na mazingira Na hayo yote yametokea kwa bahati nasibu tu. Kwa maana hiyo basi binadamu huyu hawajibiki kwa yeyote yule isipokuwa kwake mwenyewe mtu binafsi. Na hapa ndipo wazimu mwingine mkubwa wa kutomjua Mwenyezi Mungu unapoanza. Kwani binadamu huyu kwa kukosa wa kumuogopa na kukosa mwongozo sahihi, ndio amejikuta akiingia katika matatizo mengi ya kijamii na kiutawala na ubinafsi wa hali ya juu sana. Kwani kila binadamu inabidi ajijali yeye binafsi na kufanya vile atakavyo.*(Wataalamu wa kipindi hiki tulicho nacho, wamegundua kuwa Australopithecus au south Afriacan Ape, Homohabilis na Homoerectus ni viumbe ambavyo viliishi duniani kwa wakati mmoja lakini katika mazingira na maeneo tofauti hapa dunian). Na isitoshe masalia ya Australopithecus au south Afriacan Ape yanaonyesha kuwa ni sokwe wa kawaida tu, na si vinginevyo. Utafiti huu ulisimamiwa na Lord Solly Zuckerman toka England na Prof. Charles Oxnard wa USA).

ZAMA ZA MAWE
Tuangalie basi kipindi hicho walichokiita zama za mawe yaani Stone Age. Kwa hakika kabisa ukiangalia tafiti za wakati huu utagunduwa kuwa duniani hakujawahi kutokea zama walizo ziita zama za mawe, kwa sababu kila magunduzi mapya yanayofanyika tunaona kuwa watu hawa walioitwa wa zama za mawe walikuwa wakiishi maisha yaliyo kamili kabisa bila ya wai wasi wowote ule mfano walikuwa wakiishi kifamilia kama ivi leo tunavyoishi na pia walikuwa wakipika vyakula vyao kwa kutumia majiko ya moto, wakitembelea majirani zao, wakitibiwa na madaktari wao, wakiimba na kucheza muziki, wakishona nguo, kujishughulisha na kazi za sanaa mbali mbali kama kufinyanga, kuchonga, na ufuaji wa vyuma.

Ebu angalia vyungu, vikombe na kijiko na meza picha vilivyo kwenye vitabu vya Historia, utakuata vifaa vingi vina zaidi ya miaka 7-11,000 BC, lakini ukichunguza kwa makini utagunduwa kuwa binadamu hawa walikuwa na ujuzi na utaalamu wa hali ya juu sana. Je haitoshi tu kuamini kuwa binadamu hawa walikuwa kama sisi tu na hakuna tofauti yoyote ya msingi? Lakini kulingana na wana evolusheni kipindi hiki bina damu halikuwa bado hana uwezo wa kutengeneza zana kama hizi. Lakini kila kukicha wataalamu wa (archaeology) akiolojia yaani elimu ya mambo ya kale wanagunduwa mambo mapya kuhusu binadamu hao tunawaita wa kale. Na kutuonyesha kuwa binadamu hao walikuwa wameendelea katika nyanja mbali mbali kwani inaonyesha kuwa walikuwa wakitumia meza, vijiko uma, vikombe, sahani na mabakuli kama tunavyo tumia ivi leo. Wataalamu wa akiolojia wamegunduwa mawe hayo ambayo yalikuwa yakitumika kama shanga ambayo yana miaka 12,000 BC ebu tizama vizuri matundu ya shanga na vifungo yalivyotobolewa kiustadi, je uwezi kujiuliza waliwezaje kutoboa tundu za shanga hizi kama watu hawa walikuwa hawana tekinolojia yoyote ile zaidi ya kutumia mawe kugonga gonga tu? Kwa hakika watu hawa walikuwa na zana madhubuti za chuma zilizo wawezesha kutoboa matundu kama haya.

Watu hawa walikuwa wanauwezo wa kushona nguo zao na kuweka vifungo kama tufanyavyo leo. Picha za mbali mbali zipatazo umri wa miaka zaidi ya 95,000 na hii inatujulisha kuwa watu hawa walikuwa wanatumia ala za muziki kama firimbi na kadhalika.
Walikuwa wanuwezo wa kutengeneza sharasi au kigingi (Awl) kilicho tengenezwa kwa shaba halisi watu hawa walikuwa na utaalamu wa kutosha kujuwa kuwa shaba haipati kutu ndo mana wakatumia kama sindano za kushonea na hii pia inatujulisha watu hawa walikuwa na uwezo wa kuchimba madini mbali mbali kwa matumizi yao ya kila siku.


Miaka zaidi ya laki moja na zaidi binadamu alikuwa akiishi ndani ya majumba wakijishughulisha na kilimo wakibadilishana bidhaa mbali mbali kama vile nguo bidhaa za mashambani na kadha wa kadha. Inaonyesha kuwa baadhi yao walikuwa wanaafanya ibada kama ivi leo na wengine walikuwa si watu wa ibada. Na hii inaonyesha hata ivi leo kuna walio endelea kisayansi na wapo wanaoishi nyuma na maendeleo na hii ipo tangia dunia ilipoumbwa na kuwepo binadamu. Na ebu tizama ulimwengu huu wa leo tunao huita wa sayansi na tekinolojia, kuna baadhi ya nchi zinarusha vyombo angani kwenda kwenye sayari na kuna nchi hata umeme mashaka kwao, nah ii haina maana kuwa watu waliokuwa katika nchi zisizo endelea au zinazoendelea kuwa akili zao ni duni na wale walio katika nchi zilizo endelea akili zao ni nzuri sana la hasha haya yote ni mopango yake M'Mungu ili binadamu tupate kutegemeana na tuweze kumtambua muumba wetu tu basi.

Binadamu hawa walikuwa na uwezo wa kutengeneza vifaa vilivyo tengenezwa kwa madini ya kioo ambavyo vina leo hii vina umri wa miaka 10,000BC. Je ni rahisi kweli watu hawa tunao waitwa wa zana za mawe waliweza kutengeneza kifaa kama hivi kwa kuponda ponda tu bila ya kuwa na dhana nzuri kwa kazi hii?

Kuna vitu vilivyotengenezwa kwa maru maru na barsalt na bangiri ambazo zinakisiwa kuwa na umri wa miaka 8500-9000bc. Na kwa mujibu wa wana evolusheni kipindi hiki binadamu alikuwa hana uwezo wa kutengeneza zana kama izi, kwa kuzingatia kuwa barsalt ni madini ngumu sana kutengenezea umbo lolote kwa kutumia mawe tu. Bado watu hawa wameweza kutengeneza mikufu, bangiri na vifaa vingine ambavyo vinaitaji vifaa vilivyo vigumu na utaalamu kuvitengeneza.

Vifaa vya Kale:
(1) Mawe ya nakshi (Stone mosaic fragments) yanakisiwa kuwa na umri wa miaka 10,000 BC(2) Kinu na mchi wenye umri wa miaka 11,000 BC(3) kifaa kilicho tengenezwa kwa madini ya kioo (An obsidian tool) 10,000 BC

(4) Vifaa vilivyhotengenezwa kwa miamba 11,000 BC
(5) Simbi lilotobolewa lilokana na malakati 9-10,000 BC
(6) Sifongo yenye umbo kama msumali ilotengezwa kutokana na jiwe 10,000 BC

(7) Kichwa cha nyundo umri 10,000 BC.

Tafakari kwa makini je dhana kama hizi zinaweza kuwa zimetengenezwa na watu waliokuwa wakitumia mawe tu katika utaalamu wa kuchonga?

Natural Selection & MutationKwa Mujibu Wa U-Darwin (Darwinism).

Natural Selection: Kwa mujibu wa nadharia ya Darwin haya ni mabadiliko yanayotokana uwezo wa wanyama kuishi ama kutoweka kwa mujibu wa uwezo wao wa kubadilika kufuatana au kulandana na mazingira ya asili. Hali inavyokuwa ni kwamba linapotokea janga la kiasili kama vile ukame au mafuriko, kuna viumbe watakaohimili misukosuko hiyo, na wapo watakaoshindwa kuimili misukosuko hiyo. Sasa wale watakaohimili misukosuko hiyo ndio hao watakaokuwa wamechaguliwa kuishi kwa mujibu wa Natural Selection.Lakini hapa bado nadharia hii haielezei ni vipi Natural Selection inaweza kutoa viumbe vipya, kwani ikitokea kuwa kwa kiumbe mmoja kati ya wale waliofanikiwa kuishi katika misukosuko hiyo akakatika kidole au mguu bado kizazi chake kitakuwa ni kizazi kilicho kamilika viungo vyote vilivyo kamili, na wala haitatokea kuwa ni wenye kuzaliwa wakiwa na viungo visivyo timia. Yaani wawe ni wenye vidole pungufu au wawe ni wenye mguu mmoja mmoja, kama alivyo mzazi wao aliye tangulia. Au mfano rahisi ni vipi mafuriko na matetemeko ya ardhi yanaweza kujenga miji? Hii kwa kweli haikubaliki hata kidogo kwani siku zote majanga ya kiasili huleta uharibifu na si kutengeneza. Mutation: Haya ni mawazo yaliyokuja baadae sana, ni pale watetezi wa nadharia hii ya Darwinism walipoona kuwa hawana hoja zenye nguvu na ushawishi wa kina kuhusiana na dhana nzima ya kile wanachokiamini kuwa hakina mashiko au ushahidi yakinifu (concrete evidence). Ndipo walipokutana kuangalia upya dhana hii, na Mjerumani mmoja mwana paleontoolojia aitwae Otto Schindewolf katika miaka ya 1930 (German paleontologist in the 1930s). Alipokuja na dhana hii ya Mutation. Yeye anaamini kuwa mabadiliko ya gene ndio yanayoweza kuleta viumbe wapya. Na hapa ndipo yalipoletwa na kupigiwa mifano mingi tu na kuithibitisha mifano iliyotangulia. Mfano wao wanasema kuwa maisha yanatokana na vitu visivyo na uhai kama vile wadudu wanatokana na mabaki ya vyakula yalioachwa muda mrefu majalalani, na pia minyoo (Worms) wanatokana na nyama zilizo oza au panya wao asili yake ni masuke ya ngano. Mambo haya baadae katika majaribio yalio fanyika kwenye maabara ikagundulika kuwa dhana hizo zote si za kweli, kwani minyoo inatokana na nzi wanaokuja kula zile nyama huwa wanabeba lavae ambazo baada ya kurutubishwa ndipo wanapozaliwa minyoo. Vile vile mabadiliko haya wanayoyaita Mutation katika mwili wa kiumbe yeyote yule yanapotokea, siku zote huleta uharibifu katika Gene za kiumbe yeyote yule. Na hii ni kutokana na muundo wa DNA ulivyo kuwa mgumu kueleweka na kuelezeka kirahisi. Kwani inapotokea uharibifu wa aina yoyote ule katika Gene basi kitakacho patikana hapo ni kiumbe kisicho na uhai au maumbile yasio kamilika. Mfano waathirika wa bomu la atomic kule Nagasaki na Hiroshima Japan. Au walio na maradhi ya pepo punda, Saratani (Cancer) au wale wenye mtindio wa ubongo. Kutokana na Nadharia hii kutokidhi haja ya wasomi, kwa kushindwa kwake kuelezea viumbe wengine wametokana na nini na kwa sababu gani. Ndio maana wasomi wa karne zetu hizi wameweza kugundua, vitu vingi ambavyo vinapingana na nadharia hii potofu. Na hii ni kutokana na Darwin mwenyewe kushindwa kuthibitisha nadharia yake mwenyewe. Pale aliposema, na nukuu. “…But I believe in Natural selection, not because I can prove in any single case, that it has changed one spicies into another, but because it groups and explains well (as it seems to me) the host of facts in classification, embryology, morphology, rudimentary organs geological succession and distribution...” Mwisho wa kunukuu. (kwa tafsiri hisiyo rasmi ana maana ya …“Lakini nina amini uteuzi wa kiasili (“natural selection”) sio kwamba naweza kuthibitisha japo jamii moja kwamba imebadilika kutoka hali moja hadi nyingine ila kwa sababu inagawanya na kueleza vizuri (kwa nionavyo mimi) ukweli wa mambo juu ya uainishaji, taaluma ya ukuaji wa mtoto tumboni, ufanyikaji na mgawanyiko wa miti na wanyama, viungo masalia na mabadiliko ya udongo na mawe na mchanganyiko wake…”).

Qur’an 56:57-59
Sisi tumekuumbeni; basi hamsadiki? Je! Mnaiona mbegu ya uzazi mnayo idondokeza? Je! Ni nyinyi mnayo yateremsha kutoka mawinguni au ni sisi ndiyo wenye kuyateremsha?

Hali hii inaonesha kuwa hata Darwin mwenyewe alikuwa na wasiwasi na hakuwa hakika na nadharia yake hiyo ya Evolution. Lakina alikuwa na matumaini kuwa ipo siku tatizo ili la kinadharia litakuja kugunduliwa, hapo sayansi itakapo pata wavumbuzi wapya. Tukichunguza kwa makini tutakuta kuwa wakati wao hawa kina Lamarck na Darwin sayansi ilikuwa bado ipo katika hali ya ujima (hali duni sana). Kwani hata vifaa walivyo tumia wakati wao vilikuwa duni sana, na elimu nyingi zilikuwa hazijagunduliwa bado. Mfano elimu ya Biochemistry ni elimu ambayo inahusisha mambo ya kemia na maisha ya viumbe hai na Microbiology ni elimu inayo husu mambo ya viumbe hai vidogo vidogo. Na ndio maana ikawa rahisi kwao kudhani kuwa binadamu alitokea kwa bahati nasibu tu, na tena bila ya sababu yoyote ile. Kwani kwa wakati wao elimu inyouhusiana na mambo ya Genetic haikuwepo bado. Na hii ni kutokana na zana duni walizokuwa nazo wakati huo. Mwenyezi Mungu anasema nini kuhusu jambo ili.
Qur’an 31: 6-7
Na miongoni mwa watu wapo wanao nunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipo kujua, na wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha. Na (mtu kama huyo) anapo somewa Aya zetu huzipa mgongo kwa kujivuna, kama kwamba hakuzisikia, kama kwamba masikioni mwake mna uziwi. Basi mbashirie kuwa atapata adhabu chungu.

Wanasayansi wa wakati wetu huu, baada ya uchunguzi wa kina na huku wakisaidiwa na vifaa vilivyo bora kabisa, wameweza kuichunguza seli ya mwanadamu na za viumbe mbalimbali vilivyoko duniani, na kugundua mfumo wa ajabu kabisa katika maumbile ya seli hizo. Na ndani ya seli hizo wamegundua kuwa seli imegawanyika sehemu mbalimbali, na sehemu moja muhimu inaitwa Cell Nucleus yani kiini cha seli. Katika kiini hicho kuna vitu viitwavyo Chromosome. Humo ndimo kunapatikana Gene. Chromosome hizo zina umbile la Nyuzi nyuzi zenye sehemu mbili, ambazo ni DNA (Debonucleic Acid) na Histamine. Protini zilizoko mwilini mwa wanyama ufanyika kutokana na kitu kinachoitwa Amino Acid. Na unapoitaja DNA hii ni kama benki inayohifadhi taarifa zote za kiumbe, kuanzia tabia mpaka ukuaji wa kiumbe huyo. Utakapotaka kuelezea DNA kwa ufupi basi humo ndimo zapatikana sifa zote za kiumbe hai. Katika DNA kuna vitu vingi sana kiasi unaweza kujaza kurasa million za vitabu na usimalize sifa zake. Hayo ni mavumbuzi ambayo wakati wa kina Darwin hayakuwepo na wala hawakuota kuyavumbua. Wataalamu wa sasa wanasema kuwa kutokea kwa kinasaba kimoja kwa bahati nasibu ni sawa na kuandika namba ya kimahesabu kwa namna hii 1/10 x 950. Namba hii ina maana kuwa 1 gawa kwa 1 yenye sifuri 950 mbele. Ambayo ni muhali kutokea kwa bahati nasibu, yaani kwa ufupi ni kitu kisicho wezekana. Kwa binadamu wa kawada tu nakadiriwa kuwa na seli zipatazo, trilioni mia moja. Na kwa maajabu ya udogo nusu kipenyo (Radius) cha Nucleus ni cm10*-12 (0.000000000001) cm. Na radius ya atom ni 10*-8 (0.00000001) yaani seli ni ndogo kuliko kichembe kimoja cha vumbi, yaani smaller than tiny dust. Hapa sasa hebu na tuangalie kiungo kimojawapo cha mwanadamu, na maumbile yake na jinsi gani kilivyoumbwa kwa mpangilio wake wa ajabu. Kiungo hicho si kingine bali ni Jicho la mwanadamu.

JICHO:
Jicho ni kiungo cha kuonea katika mwili wa mwanadamu. Jicho la mwanadamu huanza kuchukua umbo lake katika wiki ya sita, tangia mimba kutungwa, katika mji wa mimba, katika mpangilio wa ajabu kabisa, sehemu mbalimbali za seli huanza kugawanyika na kujitenga kwa maana ya kila eneo la jicho huanza kuchukua nafasi yake. Mfano baadhi ya seli hujiunda na kuwa konea, ambayo ni sehemu ya mbele ya jicho iliyo ngumu, na yenye kupitisha mwanga. Na nyingine huwa Pupil yaani mboni, na nyingine kuwa lensi ya jicho na nyingine hujitengeneza kuwa ute wa jicho na kadhalika. Jicho la mwanadamu lina sehemu zaidi ya arobaini na kila sehemu ina kazi yake maalum. Jicho ili ambalo imekamilika lina tabia ya kupitisha mwanga, na tena kwa kiwango maalumu, mwanga upitishwa mpaka kwenye retina ambayo ina sehemu zipatazo 11, sehemu iliyo maalum kwa kupokea mwanga, na kusafirishwa kiumeme kupitia katika seli mpaka sehemu ya nyuma ya ubongo inayoitwa tiny spot au centre of vision. Na huko utambuliwa kama picha. Lakini ni kitu cha ajabu sana hufanyika kwani hiyo sehemu inayoitwa tiny spot kuna kiza sana na mwanga hauruhusiwi kufika hapo, bali mwanga ukishabadilishwa kuwa katika hali ya kiumeme (electrical signal), ndipo huruhusiwa kufika huko. Kujitengeneza huku si kwa bahati nasibu bali ni kwa mpangilio ambao kama hauku kamilika basi jicho hilo litakuwa na hitilafu kubwa sana na usumbufu kwa mtu mwenye jicho hilo.

Vilevile tukiangalia macho ya wadudu mfano kereng’ende (Dragonfly) ni mdudu mwenye macho zaidi ya elfu na kila jicho lina lensi zipatazo elfu thelathini (30,000). Mdudu huyu wa ajabu mweye uwezo wa kuona takriban pande zote za Nyuzi 360, mabaki yake (fosil) yaligundulika hivi karibuni, baada ya kuchunguzwa yalionekana kuwa yana umri wa miaka 50 milioni. Mdudu huyo hakuonyesha tofauti yoyote na Kereng’ende wa wakati huu tulionao. Kwa hali hiyo basi tunaweza kuona ni jinsi gani ni vigumu viumbe vyote hapa dunian vilivyo hai na visivyo hai kuwa haviwezi vikatokea tu kwa bahati nasibu. Yaani bila ya aliye vitengeneza. Wakati huo huo tunaamini kwa asilimia zaidi ya mia moja kuwa tunapo ona gari ikitembea barabarani au eroplane ikiruka angani basi kuna alie itengeneza na kuiwezesha kuruka.Je vipi kiumbe hai hususani mwanadamu ambaye anajitambua? Akika elimu hii ya Nadharia ya evolusheni itabakia katika mawazo ya wendawazimu wachache na kwenye vitabu vyao hao wasiomini kuwepo kwa Muumba na si kwa binadamu mwenye akili timamu.


Qur’an 59:24
Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Muumbaji, Mtenenezaji, Mtia sura, Mwenye majina mazuri kabisa. Kila kilioko katika mbingu Na ardhi kinamtakasa, naye Ni Mwenye kushinda, Mwenye hekima.

Qur’an 32:6-9
Huyu ndiye Mwenye kuyajua yasiyo onekana na yanayo onekana. Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. Ambaye ametengeneza vizuri umbo la kila kitu; na akaanzisha kumuumba mtu kwa udongo. Na kisha akajaalia uzao wake utokane na kizazi cha maji madhaifu. Kisha akamtengeneza, na akampulizia roho yake, na akakujaalieni kusikia na kuona, na nyoyo za kufahamu. Ni uchache mnavyo shukuru.

0 comments/Maoni: