Je Yesu Alibatizwa?

 Misalaba, Vinanda na Magitaa Kanisani Ni ruksa?

Lengo la makala hii si kuwavuta Wakristo katika Uislamu, bali kuelezea Waislam kile ambacho kipo kwenye Biblia na Ukristo kwa ujumla. Wakristo wengi utawasikia wakielezea ubatizo na kuhunasibisha na uwokovu. Jambo ili lina utata sana kwenye Biblia kwa sababu Biblia yenyewe si kitabu ambacho kimeandikwa na Mitume ya Mwenyezi Mungu, bali ni mkusanyiko tu wa maneno ambayo watu waliyasikia miaka mingi sana baada ya mitume kuondoka. Na hii inatoa nafasi kubwa sana kuingia kwa maneno ambayo si ya Mwenyezi Mungu bali ni maneno ya watu wenye kutaka mambo yao ndio yafuatwe. Vilevile kila kukicha kunatengenezwa nakala (Version) mpya mpya zenye tafasiri zinazokinzana baina ya toleo na toleo, kiasi cha kuacha maswali mengi hewani.
Mambo mengi yana utata katika Biblia hivyo kuwachanganya hata wenye kuufuata ukristo. Katika swala hili la Ubatizo, tunaweza kuanza kwa kusema kwamba ubatizo wa Yesu kwenye Biblia pia kuna utata, tuanze na mistari ifuatayo inavyosema:

" Naye Yesu alipokwisha kubatizwa..." (Mathayo 3: 16). Aliyembatiza ni Yohane kama ilivyo katika msitari wa 15 katika kitabu hicho cha Mathayo.

"Yohana alitokea, akibatiza nyikani…Na Yohana alikuwa amevaa singa za ngamia na mshipi wa ngozi kiunoni mwake... Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani" (Marko 1: 4-9).

"Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa," (Luka 3: 21).
Kitabu cha Yohane kinatueleza kuwa Yohane alikuwa anabatiza lakini hakumbatiza Yesu, kwani alishuhudia tu kuwa Yesu ni mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu (Yohane 1: 24-29).
Ama kuhusu vinanda na magitaa (ala za muziki) ipo mistari yanayoruhusu na mengine kukataza. Hilo linafanya wasomaji wa Biblia kuwekwa kwenye hali ya utata kuwa ni lipi lililo sawa.
Hebu tutazame baadhi ya maandiko:

Mwenyezi Mungu asema hivi:
"Mimi nazichukia sikukuu zenu, nazidharau, nami sitapendezwa na makutano yenu ya dini. Naam, ijapokuwa mnanitolea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za unga, sitazikubali; wala sitaziangalia sadaka zenu za amani, na za wanyama walionona. Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa maana sitaki kuzisikia sauti za vinanda vyenu." (Amosi 5: 21-23)
Tunaelezwa katika kitabu hicho hicho tena:

"ninyi mnaoimba nyimbo za upuzi pamoja na sauti ya vinanda, na kujifanyizia vinanda vya namna nyingi, kama vile Daudi;"
(Amosi 6: 5)

Hii mistari inatuelezea nini sisi?
Mstari wa awali unakataza muziki na wa pili unatuelezea kuwa kulikuwa kukibuniwa ala mpya za muziki kwa kumwiga mfalme Daudi. Je, mstari wa pili unaunga mkono muziki au unakataza?
Kipengele kimoja kinakataza lakini cha pili kinaunga, lakini kwa utata. Hii inapelekea swala ili kuwa na utata.
Tukiangalia tena tunakutana na mistari inayoruhusu suala hilo kwa uwazi kabisa. Hebu tutazame haya:
"Mwimbieni Mungu, nguvu zetu, nyimbo za furaha, Mshangilieni Mungu wa Yakobo. Pazeni zaburi, pigeni matari, Kinubi chenye sauti nzuri, na kinanda. Pigeni panda mwandamo wa mwezi, Wakati wa mbalamwezi, sikukuu yetu." (Zaburi 81: 1-3).
Hata hivyo, suala linakuja ni nani aliyeruhusu jambo hilo ikiwa Zaburi 72: 20 inasema:

"Maombi ya Daudi mwana wa Yese yamekwisha."

Biblia nyingine imeandikwa hivi:
"Mwisho wa sala za Daudi, mwana wa Yese"
Ikiwa ibara hii ndio mwisho wa Zaburi ya Daudi, sasa hii sura ya 81 inayoruhusu nyimbo na ala za muziki imeruhusiwa na nani? Bila shaka, itakuwa imeruhusiwa na mwingine na wala sio Daudi.


Katika Agano la Kale tunaelezwa:
"Kwa nini ulitoroka kisiri, ukanihadaa wala hukuniarifu ili nipate kukuaga kwa shangwe, nyimbo, matari na vinubi" (Mwanzo 31: 27).

Ibara hii haiwezi kuchukuliwa kama ni ruhusa kwani aliyesema ni mshirikina ambaye katika msitari wa 32 amesema:
"Lakini kwa nini uliiba vinyago vya miungu yangu?"

Ruhusa nyingine inapatikana katika Kutoka 15: 20:
"Basi nabii Miriamu, dada yake Aroni, akachukua kigoma mkononi, na wanawake wengine wote wakamfuata wakiwa na vigoma vyao wakicheza"

Hii ni taarifa ya furaha iliyopatikana kwa upande wa wanawake pale Firauni alipoangamizwa na Mwenyezi Mungu wakiwa wanawake wapo peke yao.
Suala hili mbali na kuwa na utata dalili ya mistari yenye nguvu ni ile inazokataza matumizi ya ala za muziki.
Ama utumiaji wa msalaba katika kuvaa umezagaa kabisa kwa Wakristo wa zamani na wa sasa. Kufanya hivyo kwao ni kukumbuka kule kusulubiwa kwa Yesu kwa ajili ya dhambi za wanadamu nao waingie katika kusamehewa dhambi zao hapa duniani na kurithi uzima wa milele Siku ya Qiyaama.
Hata hivyo, tukisoma katika Biblia tunapata kuwa Yesu hakusulubiwa kwani aliyesulubiwa atakuwa amelaaniwa.
Hebu tutazame mistari ifuatayo:
Akiwa mtu ametenda dhambi ipasayo kufa, akauawa, nawe ukamtundika juu ya mti; mzoga wake usikae usiku kucha juu ya mti; lazima utamzika siku iyo hiyo; kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu; usije ukatia unajisi katika nchi yako akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi wako. (Kumbukumbu la Torati 21: 22-23)
"Kristo alitukomboa kutoka katika laana ya sheria kwa kujitwalia laana hiyo kwa ajili yetu; maana Maandiko yanasema: 'Yeyote aliyetundikwa msalabani amelaaniwa" (Wagalatia 3:13).

Hakika ni kuwa wenye kuamini kuwa Yesu kasulubiwa na misalaba kwa ajili ya kusamehewa dhambi wanapingana na Biblia. Hebu tusome mistari ifuatayo:
"Maana ninachotaka kwenu ni upendo na si dhabihu, kumjua Mungu na si kutoa sadaka za kuteketezwa" (Hosea 6: 6)

Toleo lingine limeandika hivi:
"Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa." (Hosea 6: 6)
"Basi, kajifunzeni maana ya maneno haya: 'Nataka huruma, wala si dhabihu'. Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi" (Mathayo 9: 13)

Biblia nyingine imeandikwa hivi:
 "Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi." (Mathayo 9: 13)

"Kama tu mngejua maana ya maneno haya: 'Nataka huruma wala si dhabihu', hamngewahukumu watu wasio na hatia" (Mathayo 12: 7)
"Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia." (Mathayo 12: 7).

Kwa hivyo Yesu hakuja kuwa dhabihu, yaani kuuliwa msalabani bali amekuja kuwaokoa wenye hatia waingie katika mafundisho ya haki na hivyo kupata msamaha wa Mwenyezi Mungu.

1 comments/Maoni:

Unknown said...

Jazakumullahu kheir ndugu zangu kwa jitihada ya Kuelimisha Ummah.

Allah akulipeni malipo yasio na idadi. Bi idhnillah.

Amiin