Aidha, itikadi ya kuadhimisha siku hiyo pia imebeba dhana kwamba Mungu alifanya kazi (ya kuumba) kwa muda wa siku sita na baada ya kuchoka kwa kazi hiyo siku ya saba akapumzika!
Kwa kigezo hicho ndio sasa inaaminiwa na baadhi ya Wakristo kuwa imekuwa ni amri kwa wanadamu wote kwamba kwa muda wa siku sita wafanye kazi na siku ya saba ambayo ndiyo Sabato (Jumamosi) wapumzike na wafanye ibada.
Kwa hali hiyo, kupitia makala hii tutathibitisha kwa maandiko kuwa:
• Nafasi ya kuiadhimisha Sabato kwa wakati tulionao sasa.
• Uhusiano wa Sabato na wasiokuwa Waisraeli.
•Dhana potofu iliyoambatanishwa na Sabato (ya Mungu kuchoka na kumpumzika).
• Siku ambayo wanadamu wanatakiwa wafanye ibada.
Hata hivyo, kabla atujazichambua nukta hizo, ni vyema hapa kwanza tukayarejea maandiko kadhaa yanayoelezea wazi amri ya kuiheshimu na kuishika siku ya Sabato.
Mwenyezi Mungu alisema:
"Ikumbukeni siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibariki siku ya Sabato akaitakasa".
Kutoka 20:8-11
Tunachojifunza kufuatana na maandiko hayo juu ni kwamba, pamoja na kuandikwa maelezo ya "kustarehe kwake" siku ya saba baada ya kuumba kwake vitu vyote, amri ya kuitukuza sabato ilitolewa moja kwa moja na mwenyewe Mungu.
Maelezo mengine ya amri hiyo yamerejewa pia katika rejea (reference) za Kutoka 31:12-17 na Kumbukumbu la Torati 5:12-15.
Hilo halina mjadala. pamoja na hivyo, lakini...
Sabato haikuwahusu watu wengine isipokuwa Waisraeli peke yao.
Pamoja na kukiri amri ya kuishika sabato kwamba ilikuwa ni ya Mungu mwenyewe kama tulivyoona hapo juu, maandiko ya Biblia yanaeleza wazi kuwa amri hiyo haikuwa na uhusiano wowote na watu wa mataifa mengine, yasiyokuwa ya Israeli. Lakini iliwahusu tu Waisraeli na vizazi vyao peke yao. Ukweli huu unadhihirishwa na maandiko yafuatayo:
"BWANA akasema na Musa, na kumwambia, kisha nena wewe na wana wa Israeli, na kuwaambia, Hakika mtazishika sabato zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya mimi na nyinyi katika vizazi vyenu vyote, ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA niwatakasaye ninyi:
"Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika sabato, kuiangalia sana hiyo sabato katika vizazi vyao vyote, ni agano la milele. Ni ishara kati ya mimi na wana wa Israeli milele; kwani kwa siku sita BWANA alikufanya mbingu na nchi, akastarehe kwa siku ya saba na kupumzika".
Kutoka 31:12-13 na 16-17.
Kwa maandiko hayo, kinachodhihirika hapa ni kwamba hakuna watu wa mataifa mengine waliopewa amri ya kuishika sabato isipokuwa wana wa Israeli na vizazi vyao peke yao. Ambapo maandiko yanaeleza vile vile kwamba sababu ya msingi ya wana wa Israeli kupewa amri ya kuishika sabato ilikuwa ni ishara ya kuonyesha uhusiano wao mwema wa utiifu katika kuheshimu na kufuata amri za Mwenyezi Mungu.
Kisha Mungu alitoa tahadhari kwa Muisraeli atakayevunja Sabato
Baada ya Mungu kuwaamuru wana wa Israeli kuishika sabato, ili kutilia mkazo amri hiyo, aliwatahadharisha kwa kutoa adhabu ya kuuawa kwa yeyote miongoni mwao atakayethubutu japo kwa mzaha kuinajisi (kuivunja) au kufanya kazi yoyote siku ya sabato. Mungu aliwaambia wana wa Israeli:"Basi mtaishika hiyo sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia najisi hakika yake atauawa; kwa kuwa kila mtu afanyaye kazi katika siku hiyo, nafsi yake itakataliwa mbali na watu wake. Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni sabato ya kustarehe kabisa, takatifu kwa BWANA; kila mtu atakayefanya kazi yoyote katika siku ya sabato, hakika yake atauawa".
Kutoka 31:14-15
Muisraeli mmoja aliuawa kwa kukusanya kuni tu siku ya Sabato!
Ili kuonyesha ulazima wa kutii amri ya kuiheshimu na kuishika sabato na kutotii tahadhari ya kutofanya kazi yoyote siku hiyo, maandiko ya Biblia hayakuacha kumuelezea Muisreli mmoja aliyehukumiwa adhabu ya kifo kwa kosa la kukusanya tu kuni siku ya sabato.Biblia inasema:
"Kisha wakati huo wana wa Israeli walipokuwa jangwani, wakamwona mtu mmoja akikusanya kuni siku ya sabato. Hao walimwona akikusanya kuni wakamleta kwa Musa na Haruni, na kwa mkutano wote. Nao wakamweka kifungoni, maana, lilikuwa halijasemwa atakalotendwa. BWANA akamwambia Musa, mtu huyo lazima atauawa; mkutano wote wakampiga kwa mawe huko nje ya marago. Basi mkutano wote wakampeleka ya marago, nao wakampiga mawe, akafa; kama BWANA alivyomwagiza Musa".
Hesabu 15:32-36
Kwa ufupi, haya yalikuwa ndio matokeo ya mtu (Muisraeli) anayeivunja sabato. Na ni dhahiri Bwana Yesu alipokuja alilijua hili.
Hata hivyo, uovu ulipokithiri Mungu aliamua kuivunja Sabato
Pamoja na mtu yule kupondwa kwa mawe hadi kufa kwa kosa la kuvunja sabato, hatimaye katika siku za usoni, zama za Nabii Isaya (a.s.), Mungu aliamua mwenyewe kuivunja sabato kutokana na kukithiri kwa maovu, hali iliyopelekea amri za Mungu, ikiwemo ile ya kuheshimu siku ya sabato kuchanganywa na mila na desturi potofu za watu, kiasi kwamba ya Mungu na ya watu hayakutofautishwa.Ndipo Mungu mwenyewe kupitia Nabii Isaya alipoamua kukata shauri kwa kuwaambia:
"Msilete tena matokeo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na sabato, kuita makutano, siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada. Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa; nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua".
Isaya 1:13-14
Kufuatana na maandiko hayo juu, imedhihihirika kwamba kwa kuchukizwa mno na maovu ya watu hao, Mungu alifikia kuishutumu sabato kuwa ni sehemu ya "maovu" kama inavyoonekana katika maandiko hayo hapo juu. Na hili Bwana Yesu alipokuja naye alilijua. Na ndio hakuona ulazima wa kuiheshimu tena sabato, kama tutakavyokuja kuona hapo baadae.
Yesu alidhihirisha kuvunjwa kwa Sabato
Biblia inaonyesha maneno na matendo ya Bwana Yesu yalidhihirisha kwamba amri ya kuiheshimu na kuishika siku ya sabato ilikuwa haina nguvu tena kama ilivyokuwa hapo katika siku za kale. Na huu ni uthibitisho mwingine wa wazi kuwa sabato lkuwa imekwishavunjwa.Maandiko yafuatayo yanayoweka bayana ukweli huu:
"Wakati ule Yesu alipita katika mashamba siku ya sabato; wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kuvunja masuke, wakala. Na Mafarisayo walipoona, walimwambia, tazama! Wanafunzi wako wanafanya neno ambalo si halali kulifanya siku ya sabato. Akawaambia, Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenzake? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkukusoma katika Torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu. Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia. Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato".
Mathayo 12:1-8
Tunachojifunza kutokana na maandiko hayo juu ni kwamba tofauti na mtu yule aliyeuliwa kwa kosa la kukusanya kuni siku ya sabato, Bwana Yesu pamoja na kutowakemea kwa kuvunja kwao masuke siku ya sabato, bado anawatetea wanafunzi wake kwa "kosa" hilo tena kwa kulijengea hoja tofauti. Kubwa zaidi anawadharau wale wote wanaowaona kuwa ni wakosaji wale wanaoivunja sabato, pale alipowaambia:
"... kama mngalijua maana yake maneno haya msingeliwalaumu wasio na hatia (waliovunja masuke siku ya sabato)".
Aidha, kauli ya Yesu hapa kwamba "Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato" haina maana nyingine zaidi ya kuonyesha kwamba yeye (Yesu) ndiye anayehusika zaidi na sabato kwa kuwa kwanza yu Muisraeli (Marko 2:27), pili, ilikuwa kielelezo kwa wanadamu wengine, yeye ndiye anayestahiki zaidi kuwa mtu wa kwanza katika kutii amri za Mungu. Kwa maana hiyo, alijua vyema kwamba wakati ule sabato haikuwepo tena. Ndio maana kama tulivyokwishakuona hakuwachukulia hatua wanafunzi wake hatua inayostahiki walipovunja masuke siku ya sabato, kwa kuwa wakati ule kilikuwa tena si kipindi cha "sadaka" bali cha "rehema", kama mwenyewe (Yesu) alivyosema hapo juu.
Zaidi ya kutowachukulia hatua yoyote wanafunzi wake kama alivyoadhibiwa mtu yule wa kuni, Biblia pia inaonyesha kuwa Bwana Yesu aliruhusu siku ya sabato kufanya kazi, kama zile za kuokoa uhai wa viumbe, kama tunavyosoma maandiko yafuatayo:
"Akaondoka huko, akaingia katika sinagogi lao. Na tazama, yumo mtu mwenye mkono umepooza, wakamwuliza, wakisema, Ni halali kuponya mtu siku ya sabato? Wapate kumshitaki. Akawaambia, Ni mtu yupi miongoni mwenu mwenye kondoo mmoja, na yule kondoo ametumbukia shimoni siku ya sabato, asiyemshika akamwopoa? Je! Mtu ni bora kuliko kondoo mara ngapi? Basi ni halali kutenda wema siku ya sabato.Kisha akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako; akaonyoosha, ukapona, ukawa mzima kama wa pili".
Mathayo 12:9-12
Ukichunguza kwa makini mafundisho haya ya Bwana Yesu utagundua ukweli kwamba sabato ilikwishavunjwa, kwani kama anavyosema (Yesu) kuwa ni halali kutenda wema siku ya sabato, kukusanya kuni pia na katika mambo mema vile vile, lakini kwa vile zama hizo sabato ilikuwa bado haijavunjwa, mhusika aliadhibiwa kwa kuuawa.
La muhimu kuzingatia hapa ni kwamba "ruhusa" hiyo ya Bwana Yesu ya kufanya kazi siku ya sabato ameitoa wakati ambao yapo yale maandiko yanayoitaja wazi marufuku ya kufanya kazi yoyote siku ya sabato, pia yanatahadharisha Muisraeli atakayevunja sabato kwa kufanya kazi yoyote katika siku hiyo, isitoshe, yanamuelezea mtu yule aliyeuawa kwa kosa la kukusanya kuni tu siku ya sabato. Hii inaonyesha dhahiri kuwa alikuwa akionyesha kuwa amri ya kuishika sabato imekwishafutwa. (Isaya 1:13-14)
Kwa hiyo hakuna siku maalum ya ibada
Baada ya kuona Bwana Yesu jinsi alivyoonyesha kutokuwepo tena taadhima ya siku ya sabato, kwa kweli sikukuu hiyo ilibaki kuwa ni historia tu, kama Mungu mwenyewe anavyotukumbusha katika maandiko yafuatayo:"Kisha nikawaambia watoto wao jangwani, msiende katika amri za baba zenu, wala msizishike hukumu zao, wala msijitie unajisi kwa vinyago vyao. Mimi ni BWANA, Mungu wenu; endeni katika amri zangu, mkazishike hukumu zangu, na kuzitenda, zitakaseni sabato zangu, nazo zitakuwa ishara kati ya mimi na nyinyi, mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu".
Ezekieli 20:18-20
Hivi ndivyo sabato ilivyosalia. Na baada ya hapo kwa kweli hakuna siku nyingine yoyote ambayo Mungu aliiteua badala ya sabato kuwa ni siku ya mapumziko na ya ibada. Haipo!
Na kwa kweli mwongozo sahihi na ulio wazi juu ya ibada upo katika Qur’an tukufu peke yake ambamo Mwenyezi Mungu anasema:
"Na umuabudu Mola wako mpaka ikufikie hiyo yakini (nayo ni mauti)".
Qur’an 15:99
Hapa haikuwekwa tena siku maalum ya ibada. Maana yake ni kuwa anatakiwa kila mwanadamu katika kila nukta ya uhai wake ajitahidi kwa kadri ya uwezo wake kuwa katika ibada.
Na labda tatizo la msingi lililopo kwa watu wengi ni la kutokuelewa maana sahihi ya ibada na kwa upana wake. Ambapo kimakosa neno hilo wanalihusisha na kuswali (kusali) peke yake. Yaani kwa wengi inapozungumzwa "ibada" hudhania ni "kuswali" tu! Hapana!
Labda jambo ambalo ingepasa watu hawa waelimishwe ni kwamba neno "ibada" siyo neno la Kiswahili. Lakini ni neno la Kiarabu lenye maana kwa Kiswahili ya "kutumika". Na kwa upana wake ni kumtumikia Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu kwa kufuata maamrisho yake na kuacha makatazo yake yote. Na kwa hiyo, kuswali ni sehemu ya ibada na siyo ndio ibada yenyewe kamili.
Kwa mantiki hiyo, mtu huhesabika kuwa anaabudu (anafanya ibada) iwapo tu atatenda yale aliyoamrisha Mwenyezi Mungu na kuacha yote aliyoyakataza. Na jambo hilo (la ibada) ni lazima kwa muumini wa kweli alifanye kila siku na siyo kwa siku maalum.
Mungu wa kweli kamwe hana sifa ya kuchoka
Kwa bahati mbaya tumeona katika Biblia kuna mgongano mkubwa na wa kimsingi wa maandiko yake mengi. Miongoni mwa hayo ni kuhusiana na dhana ya Mungu kufanya kazi akachoka akahitaji kupumzika siku ya sabato, kama tulivyoona katika utangulizi wa makala hii.Hata hivyo, kwa upande mwingine zipo shuhuda nyingine nyingi katika Biblia zinazoonyesha kuwa Mungu kamwe hana sifa kama hiyo (ya kuchoka na kupumzika). Shuhuda mojawapo ni kama ile iliyothibitishwa na Nabii Isaya (a.s.) kwamba:
"Je! Wewe hukujua, hukusikia? Yeye Mungu wa milele, BWANA Muumba miisho ya dunia, hazimii, HACHOKI, akili zake hazichunguziki. Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo".
Isaya 40:28-29
Kwa shuhuda hizi, Nabii Isaya (a.s.) anakanusha kata kata Mungu kuwa na sifa yoyote ya kuchoka hata kupumzika (astarehe). Lakini yeye ndiye huwapa nguvu wale wasiokuwa na uwezo wa kukabiliana au kuhimili msukosuko wowote.
Na ndio maana katika Qur’an tukufu mwenyewe Mwenyezi Mungu akatilia mkazo kwamba:
"Na tumeziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yao katika nyakati sita, wala hayakutugusa machovu".
Qur’an 50:38
Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu mwenyewe katika Qur’an tukufu anakanusha vikali dhana ya kwamba alipumzika siku ya saba baada ya kuumba kwake vitu vyote. Aidha, hiyo pia Mwenyezi Mungu anaipinga kwa hoja zake zifuatazo:
"Mtanifananisha na nani, na kunisawazisha naye, na kunilinganisha naye, ili tuwe sawa sawa?"
Isaya 46:5
"Wala hana anayefanana naye hata mmoja".
Qur’an 112:4
"BWANA akamwambia Musa, Ondoka asubuhi na mapema, ukasimame mbele ya Farao, umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, asema, Wape watu wangu ruhusa waende wakanitumikie kwani wakati huu nitaleta mapigo yangu yote juu ya moyo wako, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako, ili upate kujua ya kuwa hapana mmoja mfano wa mimi ulimwenguni mwote".
Kutoka 9:13-14
Kinachodhihirisha katika aya hizi chache ni kuwa Mungu wa kweli kamwe hawezi kufanana kwa namna yoyote na viumbe wake. Na ni dhahiri kuwa sifa za kuchoka na kupumzika ni za viumbe ambazo ni udhaifu na upungufu mtupu asiokuwa nao daima Mwenyezi Mungu. Ushahidi mmojawapo ni ule wa Bwana Yesu ambaye baada ya kukiri kuwa yeye ni mwana wa Adamu zaidi ya mara 82 katika Biblia, ameripotiwa kuwa aliwahi kuchoka. (Rejea Yohana 4:6)
Kwa hiyo, Yesu naye kama binadamu, alikuwa na udhaifu kama huo na hivyo hawezi kuwa Mungu. (Isaya 40:28-29). Mwenyezi Mungu daima hachoki na milele hapumziki, kama Yesu mwenyewe anavyothibitisha.
"Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi".
Yohana 5:16-17
0 comments/Maoni:
Post a Comment