Revised Standard Version – RSV

Katika dibaji ya tafsiri ya Biblia inayotumiwa sana. Revised Standard Version – RSV - (Tafsiri ya Nakala ya Biblia Sanifu Iliyo Sahihishwa), waandishi waliandika yafuatayo:

“Biblia ya RSV ni masahihisho yaliyoruhusiwa kufanywa kwa nakala ya American Standard Version – ASV – (Nakala Sanifu ya Marekani) iliyochapishwa mwaka 1901, ambayo nayo ilikuwa ni masahihisho ya King James Version – KJV – (Nakala ya Mfalme James), iliyochapishwa 1611….


KJV ilikuwa ni lazima ishindane na Geneva Bible (Biblia ya Geneva – 1560) kwa umaarufu wake; lakini mwishowe ikashinda, na kwa zaidi ya karne mbili na nusu (zaidi ya miaka 250) hakuna tafsiri nyengine yoyote iliyoidhinishwa ya Biblia kwa Kiingereza ilifanywa. KJV ndiyo iliyokuwa “Nakala Iliyo Ruhusiwa” kwa watu wanaozungumza Kiingereza… Japokuwa KJV ina dosari na upungufu mkubwa sana. Katikati ya karne ya 19, ukuuzi wa somo la Biblia na kupatikana kwa miswada mingi ya kale zaidi kuliko yale yaliyotegemewa na KJV, ilidhihirika kuwa dosari hizi ni nyingi, nzito na kubwa, hivyo kuitisha masahihisho ya tafsiri ya Kiingereza. Kazi hiyo ilifanywa, na wenye mamlaka wa Kanisa la Uingereza, katika mwaka wa 1870. English Revised Version (Nakala ya Kiingereza Iliyosahihishwa) ya Biblia ilichapishwa katika kipindi 1881 – 1885; na ASV, kibadala chake kilichounganisha uteule na upendeleo wa wanazuoni wa Marekani walioshirikishwa katika shughuli hiyo, ilichapishwa mwaka wa 1901”[1].

“KJV ya Agano Jipya ilitegemea matini ya Kiyunani iliyoumbuwa na kuharibiwa na makosa, ikiwa na makosa yaliyokusanyika kwa karne kumi na nne (14) ya kunakili miswada. Kimsingi hii ilikuwa ni matini ya Kiyunani ya Agano Jipya kama ilivyohaririwa na Beza, 1589, ambaye alifuata kwa karibu ile iliyochapishwa na Erasmus, 1516 – 1535, ambayo ilitegemea miswada michache ya kale. Ya kale na miswada mizuri zaidi ambayo Erasmus aliitumia ni yale ya karne ya kumi, naye aliyatumia kwa uchache sana kwa sababu yalitofautiana sana na maandiko yaliyopokewa; Beza alifanikiwa kupata miswada miwili yenye thamani kubwa, yaliyoandikwa baina ya karne ya tano na sita, lakini aliyatumia kwa uchache sana kwa sababu yalitofautiana na andiko lililochapishwa na Erasmus”[2].

“ASV iliwekewa haki ya kunakili, kuilinda matini yake kutokana na mabadiliko yasiyoidhinishwa. Katika mwaka wa 1928, haki hii ya kunakili ilipatiwa International Council of Religious Education (Baraza la Kilimwengu la Elimu ya Kidini), hivyo kuingia katika umiliki wa Makanisa ya Marekani na Canada, ambayo yalishirikishwa katika Baraza hiyo kupitia kwa kamati na halmashauri za elimu na uchapishaji. Baraza ilichagua kamati ya wanazuoni ili wamiliki matini na andiko la ASV na kufanya uchunguzi kama nakala hiyo itahitaji masahihisho ya ziada… [Baada ya miaka miwili] uamuzi ulifikiwa kuwa ipo haja ya kufanya masahihisho kamili kwa nakala ya 1901, ambayo itabaki kuwa karibu iwezekanavyo na ada ile ya Tyndale-King James… Katika mwaka wa 1937 masahihisho yaliruhusiwa kura ya Baraza”[3].

“Wanazuoni thelathini na mbili (32) walishiriki kama memba wa Kamati iliyopatiwa jukumu la kusahihisha na walikuwa tayari wamepewa ruhusa ya kuchambua, kuhakiki na ushauri wa Kamati ya Ushauri ya wakilishi hamsini (50) kutoka katika madhehebu yanayoshirikiana… RSV ya Agano Jipya ilichapishwa 1946”[4].
“RSV ya Biblia, iliyokuwa na Agano la Kale na Jipya, ilichapoishwa Septemba 30, 1952, ambayo imekubaliwa sana”[5].


Katika Biblia ya RSV, idadi kubwa ya vifungu muhimu kutoka kwa Agano la Kale na Jipya ya KJV, ambazo wanazuoni wa Biblia walihitimisha kuwa ziliongezwa katika karne za baadaye, ziliondolewa kutoka kwa matini na kuwekwa kuwa tanbihi chini ya kurasa. Kwa mfano, kifungu maarufu katika Injili ya Yohana 8: 7 kuhusu mzinzi mwanamke ambaye alikaribiwa kuuawa kwa kupigwa mawe. Ilisemekana kuwa Yesu alisema: “Mtu asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe”. Tanbihi za chini ya kurasa katika RSV ya Biblia (ya 1952) inasema: “Hati kongwe za kale hazina sehemu hii 7: 53 hadi 8: 11”[6]. Kuanzia kwa mswada wa Vatican nambari 1209 na mswada wa kodeksi ya Sinai kuanzia karne ya nne hazina kifungu hiki cha aya kumi na mbili (12), wanazuoni wa Biblia wameamua kuwa maneno haya hayawezi kunasibishwa kwa Yesu. Mfano mwengine ni kifungu kinacho nasibishwa na Yesu na kutumiwa kama dalili ya Utatu katika Maandiko Matakatifu. Katika 1 Yohana 5: 7, Yesu alinukuliwa kuwa amesema: “Basi wapo mashahidi watatu wanaoshuhudia mbinguni, Baba, Neno na Roho Mtkatifu: na hivi vitatu ni mmoja [7].

Mwanachuoni maarufu wa Biblia, Benjamin Wilson, anaandika kuwa kifungu kinachohusu “mashahidi wa mbinguni” haipo kabisa katika mswada wowote wa Kiyunani ulioandikwa kabla ya karne ya 15! Kwa hiyo, katika RSV, aya hii iliondolewa katika matini bila ya kuekewa tanbihi yoyote. Hata hivyo, ili kubakisha jumla idadi ya aya katika RSV sawa kama zile za KJV, wasahihishaji waliigawa aya ya 6 kuwa ni aya mbili.


Toleo la Pili kwa tafsir ya Agano Jipya (1971) ilifaidika kutokana na masomo ya kimatini na ya isimu iliyochapishwa kuanzia Agano Jipya la RSV ilipotolewa 1946[8]. Baadaye, baadhi ya vifungu vilivyofutwa vilirudishwa, na baadhi ya vifungu vyengine vilivyokubaliwa vilifutwa. “Vifungu viwili, mwisho mrefu wa Marko (16: 9 – 20) na kadhiya ya mwanamke aliyeshikwa katika uzinzi (7: 53 – 8: 11), zilirudishwa katika matini, ikiwa zimetengwa na nafasi tupu isyoandikwa kitu na kufuatiliwa na maneno yenye kujuvya… Kwa kusaidiwa na mswada mpya, vifungu viwili, Luka 22: 19b – 20 na 24: 51b, zilirudishwa katika matini, na kifungu kimoja, Luka 22: 43 – 44, kiliwekwa katika tanbihi ya chini ya kurasa, kama vile ibara ya Luka 12: 39”[9].
______________________________________
[1] The Holy Bible: Revised Standard Version, uk. iii.
[2] The Holy Bible: Revised Standard Version, uk. v.
[3] The Holy Bible: Revised Standard Version, uk. iii - iv.
[4] The Holy Bible: Revised Standard Version, uk. iv.
[5]The Holy Bible: Revised Standard Version, uk. vi.
[6] The Holy Bible: Revised Standard Version, uk. 96.
[7] The Holy Bible: King James Version.
[8]The Holy Bible: Revised Standard Version, uk. vi.
[9]The Holy Bible: Revised Standard Version, uk. vii.

0 comments/Maoni: