Alfa na Omega (Kuwepo kwa Yesu Kabla)

Katika Kitabu cha Ufunuo 1, ayah ya 8, inaonyeshwa kuwa Yesu alisema yafuatayo kuhusu yeye mwenyewe: “Mimi ni Alfa na Omega”, asema Bwana, aliyeko, aliyekuwako na anayekuja, Mwenye Nguvu”. Hizi ni sifa za Mwenyezi Mungu. Hivyo, Yesu, kulinagana na Wakristo wa mwanzo, hapa anadai uungu. Hata hivyo, maneno yaliyotajwa hapo juu, ni kulingana KJV. Katika RSV, wanazuoni wa Biblia walisahihisha tafsiri na kuandika: “Mimi ni Alfa na Omega”, asema Bwana Mungu, aliyeko, aliyekuwako na anayekuja, Mwenye Nguvu”. Masahihisho pia yalifanywa kwa New American Bible (Biblia Mpya ya Marekani) iliyochapishwa na Katoliki. Tafsiri ya Ayah hiyo imerekebishwa ili kuiweka katika muktadha wa sawa kaa ifuatavyo: “Bwana Mungu anasema: ‘Mimi ni Alfa na Omega, yule aliyeko na aliyekuwako na anayekuja, Mwenye Nguvu’”.
Kwa masahihisho haya, ni dhahiri kuwa hii ni kauli ya Mwenyezi Mungu wala sio kauli ya Nabii ‘Iisa (‘Alayhis Salaam).

Kuwepo kwa Yesu Kabla
Ayah nyengine inayotumiwa sana kuunga mkono uungu wa Yesu ni Yohana 8: 58:

Yesu akawaambia, ‘Kweli nawaambieni, kabla Abrahamu hajazaliwa mimi niko’”.

Ayah hii inachukuliwa kudokeza kuwa Yesu alikuwepo kabla ya kuumbwa kwa ardhi. Hitimisho lililotolewa kutoka kwayo ni kuwa Yesu ni lazima awe mungu, kwa kuwa alikuwepo hata kabla ya kuzaliwa kwake duniani. Hata hivyo, fikra ya kuwepo kwa Manabii hapo mbeleni, na mwanaadamu kiujumla, inapatikana katika Agano la Kale na pia katika Qur’ani.

Yeremia anajieleza mwenyewe katika Kitabu cha Yeremia 1: 4 – 5 kama ifuatavyo:

Mwenyezi Mungu aliniambia neno lake: ‘Kabla hujachukuliwa mimba, mimi nilikujua, kabla hujazaliwa, mimi nilikuweka wakfu; nilikuteua uwe nabii kwa mataifa”.

Nabii Solomoni amenukuliwa katika Methali 8: 23 – 27, kuwa alisema:

Nilifanywa mwanzoni mwa nyakati, nilikuwako kabla ya dunia kuanza. Nilizaliwa kabla ya vilindi vya bahari, kabla ya chemchemi zibubujikazo maji. Kabla ya milima haijaumbwa, na vilima kusimamishwa mahali pake, mimi nilikuwako tayari. Kabla Mungu hajaumba dunia na mashamba yake, wala chembe za kwanza za mavumbi ya dunia. Nilikuwako wakati alipoziweka mbingu, wakati alipopiga duara juu ya bahari”.


Kulingana na Yobu 38: 4 na 21, Mwenyezi Mungu anamuhotubia Nabii Yobu kama ifuatavyo:

Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya dunia? Niambie, kama una maarifa. … Wewe unapaswa kujua, wewe ambaye umekwisha ishi miaka mingi”.

Katika Qur’an, Suratul A‘raaf (7): 172, Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatueleza kuwa mwanaadamu alikuwepo katika hali ya kiroho kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu.

Na kumbuka Mola wako Mlezi Alipowaleta katika wanaadamu kutoka migongoni mwao kizazi chao, na Akawashuhudisha juu ya nafsi zao: ‘Je, mimi siye Mola wenu?’ Wakasema: ‘Ndiye; tunashuhudia kuwa Wewe ndiye Mola wetu’. Akasema Allah: ‘Msije mkasema siku ya Kiyama kuwa sisi tumekuwa tumeghafilika na hayo’”.

Hivyo, kauli ya Nabii ‘Iisa (‘Alayhis Salaam): “Kabla Abrahamu hajazaliwa mimi niko”, haiwezi kutumika kama dalili ya uungu wake. Katika muktadha wa Yohana 8: 54 – 58, Yesu anadaiwa kuwa alisema kuhusu elimu ya Mwenyezi Mungu kuhusu Manabii wake, ambayo ipo kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu huu.

0 comments/Maoni: