Biblia Inasema Yesu Kaja Kwa Waisrail Tu

Wakristo wote wanaamini kuwa Nabii Issa a.k.a Yesu kaja kwa watu wote, Je ni kweli Bwana Yesu ametumwa kwa watu wote au na kama si kweli Biblia inasema nini kuhusiana na jambo hili...? Na ametumwa awendee nani? Hebu tuiache Biblia itueleze:

Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo. Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu. Akajibu, akisema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Naye akaja akamsujudia, akisema, Bwana, unisaidie. akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani za bwana zao. Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile.
Mathayo 15.21-28
Kwa maneno yasiotatanisha Yesu Kristo anasema kuwa yeye hakutumwa ila kwa "kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli." Hakuwajia Waarabu, wala Wazungu, wala Wahindi, wala Waafrika, wala Machina. Kama hayo hayakutosha kuonyesha kuwa yeye hakuwajia wasio Mayahudi anazidi kufahamisha kwa mfano wa kumkata mtu kiu: Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa." Ikiwa ipo shaka yo yote katika akili ya mtu kuwa maana ya maneno hayo ni kuwa Yesu anasema kuwa hakutumwa kwa kabila nyengine zo zote ila Waisiraili tu na atazame mwenye shaka tafsiri kubwa kabisa ya Wakristo inayoeleza maana wazi maneno ya Biblia, The Interpreter's Bible, sahifa 441 jalada VII ambamo imeandikwa hivi: "Yaonekana wazi kuwa Yesu hakika aliamini kuwa ujumbe wake kwanza na khasa ni kwa watu wake mwenyewe." Ndio maana alisema:
Msiwape mbwa kilicho kitakatifu, wala msitupe lulu zenu mbele ya nguruwe, wasije wakazikanyaga chini ya miguu yao, wakageuka na kuwararua.
Mathayo 7.6
Mbwa na nguruwe ni watu wa mataifa yasiyokuwa wana wa Israili. Ukristo haufai kufundishwa watu wo wote isipokuwa Mayahudi. Hayo ndiyo mawazo ya Yesu, au ya hao walioandika Injili na wakatia maneno hayo kinywani mwa Yesu. Kama asemavyo Isaac Asimov katika kitabu chake Guide to the Bible (Uwongozi kwa Biblia):
"Suala liliopo ni nani hao mbwa na nguruwe wnaokusudiwa katika mstari huu? Yaweza kuwa maana ya mstari huu ni kuwa haifai kufunza ukweli wa dini kwa wale wasiotubu katika kejeli zao, au wale waliozama katika madhambi, lakini hayo hayaelekei kabisa. Basi mtu amfundishe nani? Wale waliokwisha amini? Yesu mwenyewe anakanya hayo, kwani aliposhutumiwa kuwa anachanganyika na wenye dhambi ananukuliwa kusema:
Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi.
Mathayo 9.12
"Upande mwengine, huku kutaja mbwa na nguruwe huweza kuwa ni maneno aliyoyachagua Mathayo kulipa nguvu wazo lake kuwa isifanywe juhudi kubwa kueneza mafunzo ya Yesu miongoni mwa Mataifa mengine. Labda ni nadhari ya Mathayo kuwa ipo khatari kubwa ya hayo Mataifa kuudhika na juhudi za kutaka kuwatanasarisha na kwa hivyo wakawatesa Wakristo; itakuwa ndio 'watageuka na kuwararua'.Na hayo kwa hakika waliwahi kuyafanya. Yaweza kuwa aliona kuwa yale Mataifa yaliyoukubali Ukristo bila ya kuijua Sharia ya Musa yangeweza kuyavuruga mafunzo ya Yesu: 'na kuyakanyaga chini ya miguu yao.'"

Na juu ya kauli ya Yesu : "Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa," Asimov anasema:
"Hapa Mathayo kwa uwazi anatuletea Yesu ambaye kazi yake ni ndani ya mipaka ya uwananchi wa Kiyahudi tu."

Tukiendelea na isemavyo Biblia juu ya ujumbe wa Yesu tunapata ushahidi zaidi kutokana na Injili ya Mathayo:
Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.
Mathayo 10.5-6
Hao Thenashara ni wanafunzi wake kumi na mbili aliowateua mwenyewe Yesu kutangaza mafunzo yake. Hapo anawapa amri zilizo wazi kuwa wasiwaendee watu wa Mataifa, yaani wasiokuwa Waisraili. Hao wanafunzi kumi na mbili ndio wanaoitwa katika Biblia "mitume" kwa kuwa walitumwa na Yesu. Na wao kama yeye mwenyewe hawakutumwa ila kwa "kondoo waliopotea wa Israel" kwani "si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa." Na wanawakirisha kabila 12 za israil.

Aliwasisitiza: "Lakini watakapowafukuza katika mji huu kimbilieni mwingine, kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli hata ajapo Mwana wa Adamu
Mathayo 10:23

Kwa nini Yesu alisema maneno kama haya ya kukataa na kukataza kuwafunza dini ila Waisraili tu? Kwa nini alitumia mifano mibaya kama hivyo "mbwa" na "nguruwe" kwa kuwakusudia hao watu wengine wasio Mayahudi, yaani ndio mimi na wewe mwenzangu? Wataalamu wa Kikristo na wasio Wakristo wamestaajabishwa na maneno hayo. Ni maneno machache katika aliyoyasema Yesu ambayo yamewatatiza wasomaji Wakristo kuliko maneno haya. Wapo wanaoona kuwa Yesu alitumia matusi yale kuwaita wote wasio Mayahudi kufuata mwenendo wa Kiyahudi, yaani ndio hivyo Mayahudi wawaonavyo binaadamu wote wasio kuwa wao. Na wapo wasemao kuwa Yesu akipenda kufunza kwa mifano, na hivyo anafananisha kama kwamba yeye anaamini hiyo imani mbovu ya Kiyahudi ya kudharau watu wasiokuwa kabila yao. Na wapo wengine kama Asimov ambao wanaona maneno yale ni ya Mathayo, na yeye Mathayo (au ye yote yule aliyeandika Injili hiyo) kamuambatisha nayo Yesu maneno hayo, kwa kuwa yeye mwandishi alikuwa Mkristo wa kabila la Kiyahudi na anacho kiburi cha Kiyahudi.

Ama kusema kuwa hakutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa Israeli inaonekana kama kilivyosema kitabu cha The Interpreter's Bible kuwa Yesu hakika kwanza aliamini kuwa alitumwa kwa Waisraili tu. Ni jambo la kustaajabisha kuwa Mungu au Mwana wa Mungu aje duniani atumwe na kwanza asiujue utumwa wake ila aamini tu kuwa katumwa kwa watu wake wa Kiyahudi basi. Na kama yeye ni Mungu au Mwana wa Mungu, katumwa na nani? Kama katumwa na Mungu, basi yeye si Mungu. Si hilo tu, bali hata akiwa ni Nabii na Mtume wa Mungu tunamtaraji aujue tangu mwanzo huo ujumbe wake aliokuja nao, asiwe kutapatapa, kupapasa, na kuhangaika katika jambo la msingi.
Hapana haja ya kuyatafutia tafsiri hii na maana hii, hayo maneno yaliyo wazi ya Yesu Kristo. Yesu hakika hakutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Yesu hakika kawakataza "mitume" wake wasende kuwahubiria mataifa mengine. Yesu ni kweli kaonya kuwa kuwafundisha mafunzo yake hayo mataifa mengine ni sawa sawa na kuwapa mbwa kilicho kitakatifu, na kuwatupia lulu nguruwe. Kwa nini ikawa hivi? Ikiwa Yesu kweli katumwa na Mungu, kwa nini ujumbe wake uwekewe mipaka kwa jamaa zake tu wa Kiisraili, na yeye asikiuke mipaka ile? Naam, zipo sababu zenye nguvu kwa hayo.
Kwa hakika hayo hayakuwa mageni, wala Yesu hakuwa Mtume wa mwanzo kutumwa hivyo na Mwenyezi Mungu. Mitume wote waliokwisha kuja kabla yake walikuwa ni Mitume wa vikundi vyao tu, na zama zao tu, na walikuja na mafunzo yao maalumu machache. Musa alikuwa hivyo, na Yesu hali kadhaalika. Hali yake hali ya wenziwe, ila yeye alikuwa ndiye Mtume wa mwisho katika Mitume waliotumwa kwa kabila maalumu. Kwa nini Mwenyezi Mungu akafanya hivyo?
Kwa nini Yesu alikatazwa, mathalan, asiwahubirie yeye wala wafwasi wake, Waafrika, au Wazungu, au Wahindi, au Machina, au Waarabu? Amekatazwa kwa sababu kabila zote hizo zilikuwa hata hazijachukua khatua ya mwanzo ya kuamini Mungu Mmoja. Kabila hizo na mataifa hayo yalikuwa makafiri ama wa kuabudu masanamu, au kuabudu mapango au miti au viumbe vyengine au kuabudu wanaadamu wenzao. Na ujumbe wake Yesu ni kutengeneza mwenendo, tabia ya watu ambao tangu hapo wanayo imani ya Mungu mmoja. Yeye hakuwa na uwezo wala muda wa kujenga tangu chini. Yeye kazaliwa katika umma wenye kuamini Mungu Mmoja, umma wenye sharia ya Mwenyezi Mungu. Kazi yake kwa muda mchache alioishi na kuhubiri ni kiasi ya kuwapiga msasa tu Mayahudi ambao walikwisha tahiriwa, wanajua cha halali na haramu, na muhimu kabisa wanamjua Mwenyezi Mungu Mmoja, asiyezaa wala kuzaliwa. Ila yao Mayahudi ni kutokuwa na huruma, na kuifanya dini sharia tu isiyo na roho na imani. Mayahudi waliishika sharia ya Musa kwa dhaahiri yake, lakini waliutupilia mbali uchamngu wa Ibrahimu, wakashika ya kuonekana na watu, na wakatupa ya ndani anayoyaona Mwenyezi Mungu na dhamiri zao. Walipoacha "mitume" wa Yesu amri hiyo ya Mungu ya kutowendea makafiri wasiomjua Mungu wala msingi wa sharia, ndipo mafunzo ya Yesu yalipochafuka. Kwani hao makafiri walipoingia katika Ukristo walijigeuza jina tu, lakini waliingiza karibu yao yote ya kikafiri katika dini ya Yesu, ikaitwa Ukristo, na hali sio Ukristo kabisa aliyoufundisha Yesu. Mahekalu yao ya kipagani yakageuzwa makanisa, na mizimu na mapango yao yakawa ndio monastari za Kikristo. Lau kuwa Wana wa Israili wangeli mwitikia Yesu, basi Ukristo usingelichafuka kama ulivyo chafuka.
Upton Sinclair akiandika juu ya wakati ilipoingia Dola ya Kirumi katika Ukristo na ikaufanya ndio dini rasmi ya taifa, amesema kwa masikitiko: "Ulikuwa ni ushindi kwa Kanisa, na kwa mwenyewe mwenye kuanzisha (yaani Yesu) ni kushindwa kwa muda. Maana yake ni kuwa maadui zake wamelichukua jina lake, mafunzo yake, na nguvu zake."
Yesu alionya, lakini Paulo hakusikia:
"Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Msiwape mbwa kilicho kitakatifu, wala msitupe lulu zenu mbele ya nguruwe, wasije wakazikanyaga chini ya miguu yao, wakageuka na wakawararua."

Akazidi kuwaasa: "Mwanafunzi hampiti mwalimu wake bali yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake"
Mathayo 10:24
lakini tunaona paulo amempita hata mwalimu wa walimu, na hii inathihirisha kuwa Paulo hakuwa mwanafunzi wa Yesu.

Yesu anasema; Jitieni nira yangu mjifunze kwangu" (Mat 11:29-30) Sasa ndugu yangu wewe unajifunza kwa nani mpaka useme Yesu ni Mwokozi wa Ulimwengu?

Yaliyosemwa yamekuwa. Kwa kitendo cha Paulo kuwaingiza mapagani wa Kizungu katika dini ya Yesu sharia ya Mwenyezi Mungu ikaambiwa ni laana, ikatolewa ruhusa kula nyamafu, nguruwe na damu, na kila kiuzwacho sokoni bila ya kutia wasiwasi wo wote katika dhamiri. Tohara aliyoamrishwa Ibrahimu na Mwenyezi Mungu na Manabii wote wakaifuata mpaka mwenyewe Yesu na wanafunzi wake, Paulo aliipuuza kuwaridhi makafiri. Imani za kipagani za mungu mwana na utatu zilizoenea katika mila za Mithra, Osiris, Attis n.k. zikaingizwa katika dini ya Kikristo.
Katika ufalme wa mbinguni Yesu ana yakini kuwa hatokuwa nao ila wana wa Israili tu. Injili ya Mathayo inasema:
Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli. Na kila aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada au baba, au mama, au mke*, au watoto, au mashamba kwa ajili yangu basi atapokea mara mia na kurithi ufalme wa mbinguni.
Mathayo 19.28-29
NB:*kwenye matoleo mengine ya biblia neno mke limeondolewa

Hata katika maombi yake inaonyesha kuwa Yesu alikuwa anajua mipaka yake na uwezo wake. Madai ya kuwa yeye ni mwombezi, mbali kuwa ni mwokozi, wa ulimwengu mzima ni kumsingizia jambo ambalo mwenyewe hakulidhania. Kumpa mtu cheo asichokuwa nacho ni kumtukana, ni kumvika kilemba cha ukoka, kama Mayahudi walivyotaka kumkejeli kwa kumvika taji la miba. Cheo alicho nacho kwa hakika si kidogo. Kuwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa Mitume na Manabii watukufu ni jambo kuu kweli kweli. Kuwa mtumishi wa Mwenyezi Mungu mwenye kupendeza si utukufu mdogo. Na Yesu alitafakhari nao, na alitafakhari kuwa yeye hakutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa Ki-Israili. Na hayo si kwa upungufu wo wote kwa upande wake, ila ni kuutumikia ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa kuulinda usiharibiwe na washirikina mpaka ufike wakati wa kuja huyo atayekuwa kazi yake ni kuitangazia risala ya Mungu kwa ulimwengu mzima.
Katika Injili ya Yohana ananukuliwa Yesu kusema:
Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa.
Yohana 17.9
Tukiyachungua vilivyo maneno ya Yesu kama yalivyosimuliwa na Mathayo na Marko ya kuwa yeye alitumwa kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israili, na maamrisho yake yalio wazi kuwapa "mitume" wake wasende kwenye mataifa mengine isipokuwa Mayahudi tu, na kuwa yeye na wanafunzi wake kumi na mbili watakaa katika viti vyao vya utukufu wakizihukumu kabila kumi na mbili za Israili katika ulimwengu mpya wa mbinguni, hatuwezi ila kuhukumu kuwa hao watu anaowaombea Yesu ni hao hao waliokwisha tajwa kabla, yaani wana wa Israili, sio ulimwengu, sio mimi na wewe. Mimi na wewe si Wana wa Israili. Mimi na wewe ni mataifa mengine. Mimi na wewe na ulimwengu, usiokuwa wa Kiyahudi, Yesu kesha sema hatuombei, ikiwa tutakubali maneno yaliyoandikwa katika Injili zote.
Ni jambo linalojuulikana katika historia - na hata ukisoma katika Biblia kitabu cha Matendo ya Mitume utaona - ya kuwa Ukristo kwanza haukuhubiriwa kwa mataifa mengine mpaka alipoingia Paulo. Na yeye alipingwa vikali sana kwa kutoa shauri hiyo na wanafunzi wake Yesu waliomwona na wakawa naye siku zote na wakajifunza vilivyo mafunzo yake na makatazo yake ya kwenda kuwahubiria watu ambao bado ni makafiri. Dr. Marcello Craveri anaandika katika kitabu chake The Life of Jesus:
"Na hapo Paulo akaingia uwanjani. Kwa heba yake ya kitisho na tamaa yake, hakupoteza wakati ila alijifanya kuwa ni mmoja miongoni mwa 'nguzo' za kikundi kile, kama mwenyewe alivyokuwa kwa kejeli akiwaita Yakobo na Petro. Ukazuka ugomvi na ushindani baina yao na Paulo, na khasa katika shauri ovu la huyu Mkristo mpya kutaka kuivusha dini mipaka ya Uyahudi."

Mtaalamu wa Biblia, Dr. Hugh Schonfield, katika kitabu chake, Those Incredible Christians, (Wale Wakristo wa Ajabu) ameandika juu ya Paulo na ugomvi wake na wafuasi wa kweli wa asli wa Yesu hivi:
"Saulo wa leo, aliyetumia jina la Kirumi la Paulo, alionekana kama ni adui aliyepandwa na shetani wa Daudi mpya. Hatimaye alipokuwa mfungwa wa Warumi, hapana Mkristo aliyenyanyua hata udole kumsaidia, la Wakristo wa Yerusalemu wala wa Roma. Juhudi zake Paulo zote, hata kule kukusanya michango kuwasaidia watakatifu masikini wa Yuda, hazikupunguza upinzani dhidi yake. Wale walioshika kani miongoni mwa wana-kanisa la halali walimwona Paulo kuwa ni mtu wa khatari na mharibifu aliyeazimia kupata wafuasi wengi katika Mataifa yasiyokuwa Mayahudi ili apate ushindi wa idadi kuweza kuwapinga Wazee walioko Yerusalemu. Paulo alikuwa ni adui tangu mwanzo, na kwa sababu alishindwa katika ule uadui wake wa wazi, alijipenyeza kwa hila katika kikundi ili aweze kukibomoa kwa ndani. Hili aliweza kulifanya kwa kuitenga Torati takatifu na kumuingiza katika dini ye yote anayetaka kumfuata kwa kutamka tu imani. Ingelifaa asingekubaliwa kabisa mtu huyu; lakini walikuwapo watu ambao hawakujua wala hawakuwa na shaka naye kwa hivyo hawakutambua nini khasa makusudio yake. Na tazama basi ile imani yao imefikisha wapi hali ya mambo! Unasara wote, juhudi ya Masihi mwenyewe ikaingia katika khatari ya kudharauliwa kabisa katika Israili. Kwa sababu Paulu ni mmoja katika wasemaji wao wakubwa, na yeye alikuwa akitangaza kuwa Torati ni baatili, haifai tena kwa uwokofu, ikawa inaaminiwa na Mayahudi wachamngu kuwa wafuasi wa Yesu ni makafiri wa mwisho."

Busara ya Mwenyezi Mungu kukataza mafunzo ya Yesu yasikiuke mipaka ya Israili ni kuwa isije dini ya haki ikaharibiwa na ushirikina wa makafiri ulioenea pande zote katika zama zile. Ulimwengu ulikuwa bado haujawa tayari kupokea ujumbe wa ulimwengu mzima, na huyo mwenye kuweza kubeba ujumbe ule hajazaliwa, na umma wa kutimiza jambo hilo na kulieneza bado haujapikika ukawa tayari. Yaliyotokea tumeyaona. Ukristo tuuonao na ulioenea ulimwenguni sio Ukristo aliofundisha Yesu. Wa Yesu ulitoweka na mwenyewe na wafuasi wake wa mwanzo wa kabila la Kiyahudi. Paulo kaufuja Ukristo.
Kauli zinazonukuliwa kwa kudai kuwa ni ushahidi kuwa Yesu mwenyewe alitaka mafunzo yake yakafundishwe kwa ulimwengu wote yamo katika Injili ya Mathayo 28.19-20, Injili ya Luka 24.46-49 na Marko 16.15. Mathayo inasema:
Basi, enendeni, mkwafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.
Mathayo 28.19-20
Luka anatwambia:
(Yesu) akwaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya. Na tazama, naweletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kueni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.
Luka 24.46-49
Na Injili ya Marko inasema:
(Yesu) akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
Marko 16.15
Je, imekuwaje? Yesu ni kigeugeu? Mbona huku anawakataza wanafunzi wake wasende kuwahubiria ila kabila kumi na mbili za Israili, na huku anawaambia nendeni kuwahubiria Injili ulimwengu mzima. La, Yesu si mbabaishi, wala si kigeugeu. Hebu natuziangalie vilivyo hizo amri mbili, moja ya kuwa mafunzo yake wasifunzwe ila wana wa Israili tu, na ya pili ni hii ya kuwa watu wote wafunzwe dini.
Vipande vyote vitatu tulivyonukulu mwishoni havitaji mambo ya Yesu alipokuwa na maisha yake ya uhai wa kidunia, lakini vyaeleza mambo yaliyotukia baada ya "kufufuka kutoka wafu" kama inavyosimuliwa na Injili zote tatu. Yajuulikana kuwa Injili ya mwanzo kuandikwa ni Injili ya Marko. Hizo nyingine ziliandikwa baadae, na labda ujuzi wao ulitegemea hiyo hiyo Injili ya Marko. Yajuulikana vile vile kuwa maneno yote yaliyohusu kufufuka Yesu kutokana na wafu, pamoja na hayo maamrisho ya kwenda kuihubiri Injili "kwa kila kiumbe", kinyume na maamrisho yake yote ya kuwa asihubiriwe ila Muisraeli tu - maneno hayo yote hayakuwamo katik Marko ya asli, bali yaliongezwa baadae.
Encyclopaedia Brittanica, nakla ya 11, jalada 17, sahifa 730, yasema ya kuwa kipande chote hicho kiliongezwa baadae, yamkini mwanzo mwanzo wa karne ya pili, kuchukua maneno yaliyopotea, au yaliyoonekana kuwa ni mapungufu.
William Neil akiandika katika tafsiri ya Biblia iitwayo Harper's Bible Commentary anasema:
"Kama lipo jambo lolote katika uchunguzi wa Injili ambalo juu yake wataalamu wamekubaliana, ni kuwa kufika hapa (yaani Marko 16.8) Injili ya Marko inakoma. Sehemu iliyobaki ya sura (yaani 16.9-20) ndio hiyo iitwayo "Kimalizio kirefu" cha Injili. Kimalizio hicho hakionekani katika nakla za miswada ya zamani, na ambacho ni nyongeza iliyopachikwa katika karne ya pili kutokana na maongezo ya Mathayo, Luka na Matendo...ushahidi wa kale kabisa ulioandikwa juu ya Kufufuka (Yesu) haumo katika Injili bali katika barua ya kwanza ya Paulo kuwapelekea Wakorintho 15.3-8."

Maneno hayo ya Paulo aliyowaandikia Wakorintho na ndio mara ya kwanza kutajwa kufufuka kwa Yesu ni haya:
Kwa maana niliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maaandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; badaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake.
1 Wakorintho 15.3-8
Ikiwa kipande chote tangu mstari 9 mpaka mstari 20 katika sura 16 ya Injili ya Marko, kimepachikwa, basi kisa chote cha kufufuka Yesu kimebuniwa. Mwenye kubuni kisa hichi ni Mtakatifu Paulo. Hivyo ndivyo tunavyoweza kuagua kutokana na kuisoma Biblia, kwani maandishi ya kwanza hayamo katika Injili bali yamo katika barua ya Paulo kwa Wakorintho.
Amesema Craveri katika Maisha ya Yesu:
"Paulo alijihakikishia mwenyewe kuwa ijapokuwa Yesu ni kweli alikufa, lazima awe amefufuka, akiuwacha mwili wake wa kidunia nyuma ili avae mwili wa 'kiroho'...Paulo alichanganya mawazo yake mwenyewe ya kikafiri kafiri ya Yesu kuwa na maisha mapya kwamba ni malipo yake kwa mema yake, pamoja na imani ya Kiyahudi ya kuwajibika mapatano na Yehova (Mungu) na agano la pili. Kwa hivyo Paulo akafunza kuwa ndiyo haya khasa yaliyokuwa ni kazi ya Yesu, na hicho ndicho cheo chake machoni mwa Mungu: kafara ya nafsi yake kwa utakatifu wake na kutokuwa na dhambi kwake ili afutie kwa pamoja makosa ya wote."

Ikiwa basi msingi wa hadithi nzima ya kufufuka Yesu hadi ya ubora wake ni kuwa ni ya shaka shaka - licha ya kuwa ni wazi kuwa ni ya uwongo - hapana njia ya kuamini ya Kuwa Yesu wakati wo wote katika historia aliwahi kuamrisha watu "Enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu," kwa sababu haya hakuyasema ila baada ya huko kunakoambiwa ni kufufuka.
Katika Biblia ya Kiswahili iliyo mbele yangu iliyotangazwa na The British and Foreign Bible Society 1950 kifungu cha Marko 16 tangu mstari wa 9 mpaka mwisho yaani mstari wa 20 kimetiwa katika mipinde miwili hivi ( ) kuonyesha kuwa maneno hayo hayakuwamo katika maandiko ya asli. Ilivyokuwa imethibitika kuwa hayo ya Marko si madhubuti, basi yaliyonukuliwa na Mathayo na Luka juu ya mambo hayo ya kufufuka, na kuamrisha kwenda kuhubiria watu wa ulimwengu, na kuutaja Utatu, yote hayo ni baatili.
Kwa mukhtasari tunaona kuwa Biblia inashuhudia kuwa Yesu alikuwa ni Nabii aliyetumwa na Mwenyezi Mungu kwa Waisraili waliopotea njia. Hadithi ya kuwa aliamrisha mafunzo yake yakatangazwe kwa watu wote "kwa jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu" imebuniwa na kuongezwa mwishoni mwa Injili tatu za Mathayo, Marko na Luka. Kadhaalika kuwa Yesu alifufuka kutoka wafu kwa njia ya kimiujiza imeongezwa, na kauli ya Utatu basi ya kuwa mafunzo yakatangazwe "kwa jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu" pia nayo imebuniwa na wala haina asli yo yote ya kweli.

Ndugu yangu Injili ya Paulo, Imani itendayo kazi bila matendo 2 Tim 2:8 kwa kumfata Paulo soma (Gal 2:16).

Lakini Je! Paulo anaongozwa na nani?
Soma 1 The 2:17-18 "Lakini sisi ndugu, tukiwa tumefarakana nanyi kwa kitambo, kwa uso si kwa moyo, tulizidi kutamani kwa shauku nyingi kuwaona nyuso zenu, kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam mimi Paulo mara ya kwanza, na mara ya pili na "Shetani" katuzuia. Paulo hana Roho Mt (Gal 3:15). Alikupata kwa hila 2 Wak 12:16.

Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.
Mathayo 7:21-23

0 comments/Maoni: