Fetishism

Ni maradhi anayokuwa nayo mtu aliyeelemewa na mawazo ya ngono hadi kuwa na tabia ya kupenda vitu ambavyo anavihusisha na mtu wa jinsia tofauti na yake. Kwa tafsiri finyu, mtu mwenye maradhi haya hususan mwanaume huwa na mapenzi na vitu vinavyohusiana na mtu mwingine, hususan mwanamke, kama vile nguo za ndani au hata viatu. Mtu huyu akiviona vitu hivi anaweza kuvifuga nyumbani kama ambavyo watu hufuga ndege.

Kama ni nguo ya ndani, labda iliyosahauliwa bafuni au iliyoanikwa, au hata iliyochorwa tu kwenye picha, au iliyotundikwa dukani ikiuzwa, basi humsisimua na kumfanya katika mawazo yake kuona zaidi ya kile anachokiona wakati huo.

Mgonjwa wa maradhi haya anaitwa Fetishist, na vile vitu vinavyomvutia vinaitwa Fetish. Kwa tafsiri pana, Fetishism ni maradhi ya kujawa na wazo la zinaa kwa kupitia kitu (Fetish) fulani.

Ukiacha tafsiri za kwenye vitabu, ambazo zinachukulia Fetish kuwa ni nguo za ndani tu au vitu, kwa upana wake, Fetish ziko nyingi mno. Tukitoa Fetish hizi, nguo za ndani na viatu, nitaziorodhesha Fetish nyingine ambazo huwaathiri wagonjwa hawa.

Umbile la mwili la aina fulani pia linaweza kuwa ni kivutio (Fetish) kwa Fetishist. Umbile hili ni la mwili, kwa mfano wanawake wenye maumbo makubwa hasa sehemu za makalio huwa ni Fetish nzuri sana kwa wagonjwa hawa, na ndio maana magazeti ya habari za kipuuzi na ngono ambayo sasa hivi yamejaa katika jamii yetu na yanapendwa mno na wenye maradhi haya, huwa na picha za kuchora zenye wanawake wenye makalio makubwa kupita kiasi ili picha iwe na mvuto fulani.

Stara ya Hijab humsaidia mwanamke asiwe ni Fetish kwa wenye maradhi haya.

Harufu: Pia inaweza ikawa ni Fetish , hususan manukato. Mara nyingi wenye maradhi haya wanaposikia harufu ya manukato inawapa hisia ya "mwanamke mzuri kama jini". Mara nyingi manukato hutumiwa na wanawake wanaopenda kujipamba wakitoka nje ili watu wawasifie au wawapende. Wanawake hawa huvaa nguo za fahari na nyingine fupi (hasa za wendawazi) na hujipaka manukato.

Hivyo mtu anaposikia harufu ya manukato, hata kama haoni mtu, harufu hiyo humpa hisia ya wanawake walio katika hali fulani ya mvuto wa zinaa. Ndio maana wanawake wa Kiislamu huambiwa wapake kila aina ya manukato kwa ajili ya waume zao ndani, lakini wakitoka nje wanaambiwa wasijitie manukato makali, ili wasije wakawafanya watu wachemkwe kwa kupata harufu watakayoihusisha na mwanamke, hasa wale wenye maradhi katika nyoyo zao.

Kwa wanaume wenye maradhi haya, sauti ya mwanamke pia huwa ni Fetish. Kwa kawaida sauti ya mwanamke huwa ni tofauti na ya mwanaume, kwani ya mwanamke ni nyororo. Hivyo utofauti huu humfanya Fetishist kushtuka asikiapo sauti ya mtu mke, au huburudika tu kusikia mwanamke akiongea, kulia au kuimba. Kwa tahadhari ya kuwahemsha watu wenye maradhi haya, wanawake wanaaswa kurembesha sauti zao kwa waume zao tu, na wanapoongea nje, wazikaze sauti zao,
kama walivyoambiwa wake za Mtume (s.a.w.) katika Qur’an:
"...basi msilegeze sauti, asije akatamani mtu mwenye maradhi katika moyo wake, na semeni maneno mazuri".
Q33:32

Kwa wagonjwa wengine, hata mwandiko huwa ni Fetish. Kwa kawaida, miandiko ya wanaume na wanawake huwa inatofautiana. Katika jamii yetu tumezoea kwamba mwandiko wa herufi zinazolalia kushoto ni wa kike, basi Fetishist akiwa mwanafunzi atakwambia daftari likiandikwa na mwanamke linasomeka na kueleweka vizuri zaidi. Vile vile, hawa wagonjwa hupenda marafiki wa kalamu, na wanaweka masharti kwamba rafiki huyo ni lazima awe mwanamke wa umri fulani, basi miandiko ile humridhisha, akawa hana kazi ya kufanya zaidi ya kusoma na kurudia kusoma barua za wanawake asiowajua.

Fetish nyingine huwa ni picha, hasa za wendauchi. Wenye maradhi haya ukiingia vyumbani mwao utakuta wamebandika picha za watu waliovaa vichupi na sidiria tu. Hayo ndio mapambo waliyonayo. Pia wenye maradhi haya hupendelea magazeti ya picha za ngono (ponography), au magazeti ya upuuzi yenye manyang’unyang’u na mafindo findo na zile wanazoziita "chachandu" ili mradi maradhi haya ni kichaa cha aina fulani kilichowakumba watu wengi, wengi wao wakiwa ni wenzetu.

Nyimbo za aina fulani pia huwa Fetish . Mara nyingi Fetishist hupenda kusikiliza na kuimba nyimbo zinazoamsha hisia za ngono. Hapa na wanawake pia wanakuwa Mafetishist . Katika jamii yetu, taarabu kwa mfano zilikuwa na nyimbo zenye mashairi mazuri yenye nasaha na maliwazo mbalimbali mazuri, lakini sasa hivi taarab imevamiwa na watu "wa kuja" ambao hawana asili na taarab, basi wamechafua taarab kwa kuingiza nyimbo za kifuska, na kwa bahati mbaya nyimbo hizo, hata redioni hazipigwi kwa ubaya wake, lakini utazikuta zinapigwa majumbani.

Utamkuta mwenye maradhi kakaa anasilikiza, tena wengine na vibalaghashia vyao, anatingisha kichwa kwa raha ya wimbo wa matusi, na wanawake walio karibu, hadi mabinti wadogo nao wanaisaidia redio kaseti katika kumliwaza au kumhemsha mgonjwa.

Sehemu ya mwili, hasa wa mwanamke, pia inaweza kuwa ni Fetish kwa wenye maradhi haya, hasa
sehemu za mapaja na kifua. Hapa wenye maradhi haya hufaidi sana wanapoishi kwenye jamii yenye wendauchi.

Nywele pia huwa ni Fetish ya ajabu. Utakuta wanaume wengi wa Kiafrika hupendelea nywele za Kizungu. Kasumba iliyojengeka miongoni mwa Waafrika malimbukeni ni kwamba kila kitu cha Kizungu ni kizuri, basi hata nywele. Kwa kujua hili, kwamba wanaume wa Kiafrika huvutiwa sana na nywele za Kizungu, ndipo wanawake wengi mno huzibadilisha nywele zao (kwa vile hufurahia kuwa Fetish Object), wakaweka dawa za ajabu ambazo nyingine huwafanya wanuke vibaya, nyingine huwanyonyoa nywele, na nywele zinaponyonyoka ndipo wanapoamua kuunganisha nywele za brashi au kuvaa manywele ya bandia (wigs).

Ukimkuta mwanamke kavaa chupi ya mtoto ya mkojo kichwani ujue anaogopa nywele zake zikingiia maji zitaharibika na zikiharibika hawezi kuwa mteja wa Mafetishist. Mwanamke wa Kiislamu hawezi kufanywa chanzo cha starehe ya wanaume wenye maradhi ya Fetishism.

Kwani Mwanamke wa Kiislam anapaswa kijistiri kwa kuvaa hijab, inayomstiri mwili mzima, haonekani mapaja, kifua wala nywele zake. Ni Uislamu tu ndio unaoweza kuleta ponyo ya maradhi haya na mengineyo...

0 comments/Maoni: