Tetemeko La Ardhi “Haiti” Na Mafunzo Tunayopata

Maisha ya dunia sio chochote mbele ya Muumba na yaweza kukatika ghafla bila ya kuletewa taarifa. Tuna amka tukilala tukiwa ni wenye kusindikiza vijana kwa wazee kwenye malazi ya milele ndani ya Barzakh.

Zipo njia nyingi za kukatika maisha haya kama vile ajali, maradhi na mauaji. Hata hivyo, kuna aina nyingine ambayo kwa karne mbili hizi zilizopita, imepamba moto. Ni hii ardhi yetu tunayoringa nayo kushindwa kabisa kuhimili madhambi yetu yaliyopindukia mipaka. Hapo tunaona kimbunga, mitetemeko, kiwango cha juu cha joto au baridi kali na kadhalika.

Ardhi ya Haiti ni mfano mzuri wa kuwazindua ndugu zetu wa Kiislam. Hakika kuna mengi ya kujifunza kwa Waislam kutokana na tetemeko lililotokea tarehe Tarehe 12 Januari 2010, saa 21:53 UTC, (saa 10:53 jioni kwa saa za Afrika Mashariki) tetemeko lenye ukubwa wa magnitude 7,0 huko Haiti. Maisha ya maelfu yalipotea ghafla bila ya matarajio. Maelfu walipoteza viungo ambavyo kina dada wakivipigia mnada bure kabisa. Maelfu ya matajiri waliokuwa wakitakabbar kwa utajiri, siha na neema aliyowapa Allah waliondoka kwa wepesi kabisa. Mamilioni ya maisha ya watu yalibadilika ghafla ndani ya kipindi kisichozidi nusu saa... ALLAAHU AKBAR! Yapo wapi macho ya Waislam kutanabahi kiumbe hichi kinachoitwa ardhi kushindwa kuhimili madhambi ya wanaadamu?!

Majanga haya hayajaacha kuganduka kwa Haiti ingawa ina idadi kubwa ya wananchi wake kuwa sio Waislam. Juu ya kwamba wamekuwa na ubinaadamu na moyo wa kusaidia haraka, hata kwa wale waliokuwa hawana uwezo, nao wamejitolea kusaidia. Sisi Waislam leo uwezo tunao, badala ya kusaidiana tunaleta jeuri ya neema tuliopewa.

Ni funzo kwa Waislam kuwa Maneno ya Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) hayaanguki abadan, kuwa siku za mwisho kutakuwa na majanga mengi, vifo vitatokea vingi kwa pamoja na mengineyo:

Uharibifu umedhihiri barani na baharini kwa sababu ya yale iliyofanya mikono ya watu, ili Awaonjeshe (adhabu ya) baadhi ya mambo waliyoyafanya, huenda wakarudi (wakatubia kwa Mwenye Enzi Mungu).
Ar-Ruum 30: 41

Naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekwisha bainisha kuwa maafa yatakuwa ni mengi karibu na Qiyaamah:

“Saa (Qiyaamah) haitosimama hadi elimu ifutwe, wakati kukimbia kwa kasi, mitetemeko kuzidi kwa sana, fitna kutokea na al-Harj kuengezeka.” Akaulizwa, “Ewe Mjumbe wa Allaah, nini hiyo al-Harj?” Akasema, “Al-Qatl, al-Qatl (Mauaji, Mauwaji)”.
Imepokewa na Imaam Ahmad

Na kwa vile maneno ya Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) pamoja na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni mazima; tujue kuwa mitihani hii ipo, na bila ya shaka kila tuliloahidiwa litatokea, ikiwemo Qiyaamah chenyewe. Kwa mantiki hiyo; tunatakiwa tustaghfiru na tujiweke tayari na kifo wakati wowote.

Hakuna mwenye mihadi (appointment) na Malakul-Mawt. Anakuja ule wakati anaopangiwa na Mola wake aje kuzichukua roho zetu. Wahaiti wale waliokufa kwa mpigo hakuna hata mmoja aliyejuwa kama siku ile angekufa, ya kwamba angekwenda nchi jirani kwa kukimbia mauti. Laiti ghayb ingejulikana na viumbe, Serikali ya Haiti ingekuwa na uwezo wa kuwahamisha watu wake kutoka kwenye eneo la epicenter kabla maharibiko hayajatokea.

Hili jambo liwaguse wanaosema: "acha ni-enjoy, mie kijana, bado damu inachemka kotekote". Waliokufa katika maafa walikuwemo vijana waliochemkwa na damu mpaka zikatokota kwa afya njema na uzuri. Na wale walionekana na maumbo madogo, hawakuwa ni mbilikimo (watu wafupi), bali ni watoto wadogo kuonesha kwamba kifo au maafa hayachagui umri.

Hili jambo pia liwaguse wenye uwezo wanaogoma kuhiji, wakisema kuwa watakwenda baadae. Nadhani, pengine katika mamilioni ya watu wale kuna ambao walikuwa na mawazo kama hayo japo mmoja na hakufanikisha malengo. Na hiyo ni khiyana kwa Allah mtakatifu tunamfanyia, kuwa Katupa uwezo na tunautumia kinyume na malengo ya Dini. Liwaguse hili jambo, wale wanaosema watajistiri... tusubiri... tusubiri kwanza...

Ni vyema nikakomaa hapa, kwani ni mengi tunayojifunza kutokana na mitetemeko hii ya ardhi. Mimi moyo wangu umeingiwa na khofu kubwa juu ya mauti na amali zetu, nimeingiwa na imani na watu waliopoteza viungo ambavo sisi tunavyo na badala ya kumshukuru Mola Mlezi wetu, hatuinami (hatusali) mpaka tuanguke (tufariki).

Nimeingiwa na imani kuona vitoto vichanga vinakosa wazee. Nimesikitika kwa kila hali na nikalia ndani ya moyo wangu.

Wa billahit Tawfiyq.

0 comments/Maoni: