Uwaminifu Na Utii

Qur’an inatupa maelezo ya kina ya asili ya mwanadamu. Ufisadi wote na sifa mbaya za makafiri zinatajwa na sifa nzuri za waumini piya zinatajwa. Sifa za waumini watiifu wanaojitupa kwa Allah na ambao nyoyoni mwao Allah amewapulizia roho itokanayo naye ndizo zinazojenga muruwa bora wa maadili.

Kwa hakika, kiwango hicho cha juu cha maadili ya waumini kinatofautiana kabisa na kile cha makafiri. Ikhlasi na uwadilifu ni mambo yanayotofautiana na silika ya utovu wa ikhilasi na unafiki ya wasioamini.

Halikadhalika, tabiya ya ukarimu, ujasiri na heshima ya waumini ni tofauti kabisa na tabia ya kiburi, ukatili na ubinafsi ya wasioamini. Kipengele kimoja kinachotofautisha makundi haya mawili- yaani kati ya waumini na makafiri ni tabiya ya uwaminifu au ukosefu wa uwaminifu

Kwa maana sahihi ya uwaminifu, makafiri hawawezi kamwe kudumu katika kweli, hii hasa ni kutokana na ukweli kuwa wanasukumwa na matamanio ya nafsi zao: Ni wepesi kukata tamaa katika kupigania kile ambacho wao wanadhani ni sahihi kwa mtazamo wao.

Lakini waumini wana mwenendo tofauti kabisa. Mwenendo wanaoufuwata wao unajieleza katika aya hii; Sema:
“Hakika Sala yangu, na ibada zangu na uzima wangu, na kufa kwangu; ni kwa MwenyeziMungu si kwa kutaka viumbe. Na yote ninayoyafanya nayafanya kwa ajili yake).”
Q 6:162.

Kwa hali hiyo wale wenye imani huwa makini na tabiya zao wakijitupa kumtumikia Allah na hubakiya na msimamo katika lengo hilo kwa gharama yoyote ile. Kamwe hawaachi njiya ya ucha Mungu kwa sababu ya maslahi machache ya duniya.

Na huonesha utiifu usioyumba wala kutikisika kwa waumini na hasa kwa Kiongozi wa Waumini. Allah anaelezea ukweli wa wa waumini katika Qur’an kama ifuwatavyo:

Wapo watu miyongoni mwa walioamini waliotimiza ahadi waliyoahidiana na Mwenyezi Mungu: Baadhi yao wamekwishamaliza umri (wamekufa), Na baadhi yao wanangoja (siku yao kufika) wala hawakubadilisha (ahadi yao) hata kidogo.
Q 33:23)

Imani huwathubutisha Waumini wanaopigania itikadi yao katika kulielekea lengo. Sifa hii ni sifa ya msingi katika dhamira na ni sifa muhimu kwa jamii yoyote ya Waumini.

Muumini atakuwa ameshindwa kuchunga heshima yake kama atathubutu japo mara moja kuonesha kupuuzia uwaminifu. Pale mtu anapopoteza uwaminifu kabisa, basi kidogo kidogo mtu huyo hufikia mahala pa kupoteza imani.

Baada ya hapo mambo humuharibikiya kwa kasi na matokeo yake huwanza kuwa na ule ule mwenendo alionao mnafiki. Hii ni kwa sababu ile hali ya kukosa imani humsukuma kufanya aina nyingine ya udanganyifu.

Kwanza kabisa, huwanza kukengeuka kwa kujaribu kuficha ule utovu wake wa imani usionekane kwa Waumini wengine. Hapo sasa huanza kusema uongo, na kujitahidi kuwahadaa wengine. Baada ya muda fulani uhodari wake wa kuongopa humfanya ajione kuwa anaweza kuwazuga kikwelikweli waumini na huanza kuishi maisha ya ujanja ujanja.

Mtu huyu mdanganyifu huanza kupoteza mapenzi kwa waumini. Kwa mwenendo huu huanza kutafuta kufurahisha watu badala ya kutafuta radhi za Allah. Ndio maana huanza kutafuta umashuhuri. Huliona kila jambo linalomvurugia umaarufu huu kuwa ni hatari kwa sifa yake na hivyo hujitahidi kujikinga kwa kuongopa zaidi.

Wakati huo huo waumini wanapoanza kung’amuwa uwongo wake, hudhihirisha sifa zaidi za mtu mnafiki. Huthubutu kujihami. Lakini jitihada hii humgeuza hata kuwa mtu ambaye hasiti kuungana na na makafiri na wanafiki.

Mlolongo wa matukio yaliyotajwa hapo juu hufichuwa mambo fulani yanayorandana na tabia ya kinafiki ya mtu huyo ambayo huonekana madogo na yasiyo na uzito. Haya ndiyo sasa humpelekea mtu kuwa kafiri.

Lakini waumini, kwa upande mwingine, kwa imani yao thabiti, hudumu katika uchaMungu hadi siku ya kufa kwao, kwani wao hawaelekezi utii wao kwa mwingine yeyote isipokuwa Allah. Jambo hili linaelezwa katika aya ifuwatayo:

Mwenye kumtii Mtume wa MwenyeziMungu amemtii MwenyeziMungu, (kwani anayoyaamrisha Mtume yametoka kwa MwenyeziMungu). Na anayekengeuka (anajidhuru mwenyewe). Hatukukupeleka wewe kuwa mlinzi juu yao;(wakipotea ulaumiwe wewe. La. Hatukukufanya hivyo).

Kuwa mkweli ni moja ya mambo muhimu ambayo muumini ayazingatie. Huku akitufahamisha wanafiki ambao huwa tayari kuyakwepa majukumu yao, Allah anatutaka kutilia maanani ahadi walizochukuwa katika Qur’an kwamba wasigeuze migongo yao na kwamba watu hao wanabeba dhima kubwa:

Na kwa yakini walikwishafanya ahadi na MwenyeziMungu zamani ya kwamba hawatageuza migongo (wakija makafiri kushambuliya); na ahadi ya MwenyeziMungu ni yenye kuulizwa. (Basi wataulizwa kwa nini wakatengua ahadi).
Q 33:15

Ahadi iliyotolewa kwa Allah ni dhima kubwa, ndiyo sababu Allah anawaamrisha hivi waumini:

Wala msiuze ahadi ya MwenyeziMungu kwa thamani chache (mnayopata hapa ulimwenguni). Kilicho kwa MwenyeziMungu ndicho bora kwenu, ikiwa mnajuwa.
Q 16:95

Bila shaka ishara muhimu ya uwaminifu ni utii. Utii ni sifa muhimu ya waumini, kama ilivyoelezwa katika Qur’an. Kwa kweli ni nyenzo muhimu ya kupatia Rehema za Allah, kupatia pepo na kupatia ushindi dhidi ya makafiri.

Na mtiini MwenyeziMungu na Mtume ili mpate kurehemewa.
3:132

Hiyo ni mipaka ya MwenyeziMungu. Na anayemtii MwenyeziMungu na Mtume wake, (MwenyeziMungu) atamwingiza katika Bustani zipitazo mito mbele yake; wakae humo milele. Na huko ndiko kufaulu kukubwa.
Q 4:13

Enyi mlioamini! Mtiini MwenyeziMungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka juu yenu,walio katika nyie (waislamu wenzenu). Na kama mkikhitilafiana juu ya jambo lolote basi lirudisheni kwa MwenyeziMungu na Mtume, ikiwa mnamwamini MwenyeziMungu na siku ya mwisho. Hiyo ndiyo kheri, nayo ina matokeo bora kabisa.
Q 4:59

Na hatukumleta Mtume yeyote ila atiiwe kwa amri ya MwenyeziMungu. Na wangalikuja walipojidhulumu nafsi zao wakaomba msamaha kwa MwenyeziMungu, na Mtume pia akawaombea msamaha, bila shaka wangemkuta MwenyeziMungu ni Mwenye kupokea toba na (Mwenye) kurehemu. Naapa kwa haki ya Mola wako wao hawawi wenye kuamini (kweli kweli) mpaka wakufanye wewe hakimu katika yale wanayokhitilafiana, kisha wasione uzito nyoyoni mwao juu ya hukumu uliyotowa, na wawe wanyenyekevu kabisa.
Q 4:65

Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume, basi hao watakuwa pamoja na wale aliowaneemesha Mwenyezi Mungu, Manabii na Masadiki na Mashahidi na Masalih. Na uzuri ulioje(kwa mtu) watu hao kuwa rafiki (zake)
Q 4:69

0 comments/Maoni: