Exhibitionism

maradhi yaitwayo Exhibitionism, ni maradhi ambayo mgonjwa huona raha kuonekana sehemu zake za mwili zisizotakiwa kuonekana. Hawa ndio wale tunaowaita kwa Kiswahili rahisi wendawazimu au wendauchi. Kitaalam mgonjwa huyu anaitwa Exhibitionist.

Maradhi haya yanafanana na yale yanyoitwa Voyeurism yaani mtu kupenda kukodolea macho watu ambao wako faraghani na hawana nguo (makozimeni). Hivyo hawa wagonjwa tunaowachambua leo ukidhi sana haja za ma-Voyeur (Keeping Toms). Kwani wengi wao ndio wale wanaotokea kwenye sinema za X, kwenye kanda za video zinazoonyesha ufuska, pamoja na kwenye magazeti yenye picha za wendawazimu (Ponographic magazines).

Maradhi haya ya wendawazimu yameanza kuingia kwa kasi zaidi katika jamii yetu.

Mara nyingi wendauchi huwa ni wanawake, ingawa na wanaume pia wapo wanaopenda kujiweka wazi waonekane na watu.

Tukianza na wagonjwa mahututi, hawa huona raha tu watu wengine wanapoona "uwazi" wao, na roho zao hufurahi tu sehemu zao "nyeti" zinapoonekana. Kule Ulaya na Marekani, nchi ambazo zimeendelea kwa kila kitu, hadi ufuska, wendauchi wamefikia mpaka kuanzisha jumuiya zao, na wana sehemu zao maalum au kambi ambazo ukifika huko unaacha nguo mlangoni na unabaki wazi kama mnyama. Hawa wanaitwa "Nudists", na Marekani ambako kuna "uhuru" mkubwa wa kufanya mambo, kambi hizi za wenda wazi (nudist camps) zinajulikana na zinapewa baraka zote na serikali, na baadhi ya wananchama ni viongozi wakubwa wa serikali. Kuna hofu kwamba kwa vile nchi za Afrika zimekaa tayari kuiga kila kinachotendeka Ulaya na Marekani, huku kwetu nako kambi hizi karibia zitakuja.

Kwa hiyo kama tulivyo na mbuga za wanyama kama vile Serengeti, Manyara, Mikumi, n.k. hivi karibuni tunaweza tukawa na "mbuga za wendauchi". Nasema hivi kwa sababu madanguro (Casinoes) tayari yamo katika jamii yetu, na yamepewa leseni.

Ugonjwa huu wa wendauchi unaongezeka kwa kasi Afrika. Kwa haraka haraka unaweza kuona hawa wendauchi wamefikia kuwekewa kumbi za kifahari, wakipita uchi mbele za mamia ya Makozimeni na mshindi wa kupewa zawadi ya mamilioni akapatikana. Haya ni mashindano ya urembo, na urembo wa mtu, hasa mwanamke ni mwili wake wote. Hivyo kuonyesha urembo ni kujiweka wazi, ukiwa umevaa vile wenyewe wanavyoviita "vichupi" hushangiliwa na kupewa zawadi, na tiketi ya kwenda Ulaya au Marekani, kuingia katika mashindano ya kimataifa ya wendawazi. Kwa hiyo, jamii yetu imefikia kutoa wendauchi mabingwa katika hadhi ya kimaaifa kwenda kugombea Uendawazi wa dunia.

Dalili nyingine ya kuenea maradhi haya ni wendawazi kuenea kwenye matangazo ya biashara. Kama unataka bidhaa yako inunuliwe sana, basi weka picha ya mwendawazi wa kike, hata kama ni kibiriti mtu atanunua kumi akaviweke tu nyumbani.

Dalili ya wazi nyingine ni ile ya wacheza ngoma wanaotokea kwenye video. Utakuta bendi ya muziki wanaume wote wamejisitiri tena kwa mashati na masuruali mapana kabisa, lakini wanawake wanenguaji wako wazi, na wanaona raha tu kuonekana hivyo.

Mitaani ndio kumejaa hasa ma-Exhibitionist, hasa wa kike, ambao wanavaa visuruali vyembamba kama ngozi (skin tight). Sasa hao ndo wenye nafuu. Kuna wale ambao wanashona visketi vifupi, halafu ufupi wa visketi vyao hauwatoshi, wanaongeza kupasua nyuma. Hawa mimi huwafananisha na mbuzi ambaye kapewa kamkia kafupi, halafu kamkia kenyewe badala ya kulala chini kamhifadhi, kamekaa wima, kwa hiyo kanamuacha mbuzi wazi kabisa bila ya stara kama aliyonayo kondoo.

Wanaume nao wapo wenye maradhi haya. Utamkuta mwanamume kavaa Kibukta , nywele zote za kifuani, tumboni na mapajani ziko nje, wala hashituki eti anapunga upepo. Wengine utawakuta mitaani na hivyo vibukta vyao, wala hawaoni tabu, ili mradi raha yake ni aonekane alivyotunisha misuli ya mapaja yake.

Madhara ya Exhibitionism
Uislamu dini iliyopo kwa maslahi ya wanaadamu unapokataza jambo basi ni lazima lina madhara kwa jamii. Sasa hivi duniani kuna maradhi yameingia, kwani tunaambiwa kuna dawa ya kuongeza nguvu za kiume inaitwa VIAGRA. Watu wanaishangilia bila kujua sababu ya kuja dawa hii. Dawa hii imekuja kwa vile wanaume wabovu wanaongezeka. Ubovu huu wa kupoteza ngvu za kijinsia unasababishwa zaidi na watu kuwa na tabia ya kwenda uchi. Sasa hivi imekuwa ni kawaida kwa mwanamke kupita mapaja wazi na wanaume wengi hawashituki. Yaani kumuona mwanamke yuko wazi ni kama kumuona mbuzi tu. Limekuwa ni suala la kawaida. Ule msisimko wa mtu kumuona mtu wa jinsia nyingine umekwisha.

Nasaha
Kwa kina dada: Kila kitu kina stara yake, hata ndizi. Ndio maana wauza ndizi huwa hawazimenyi kwanza ndio wakaziuza kwa sababu wanajua hakuna atakayezinunua, bali zitang’ong’wa na mainzi. Hivyo hivyo, wale wanawake waliojitoa stara ndio kama ndizi zinazotembezwa zikiwa zimemenywa. Sasa wale wanaowashangilia wakipita uchi si watu bali ni mainzi yanawang’ong’a. Msijidhalilishe kwa kujiweka wazi.

Kwa Waislamu wote: Moja kati ya tofauti ya wanyama nawatu ni kuvaa nguo (kujistiri). Kila unavyozidisha stara, ndivyo unazidisha tofauti yako na mnyama. Na kila unavyopunguza stara ya mwili wako ndio unaukaribia unyama zaidi, yaani unapunguza ule utofauti wako na mnyama. Uislamu ndio unasisitiza stara ili kuwafanya binadamu wawe watu. Ndipo Mwenyezi Mungu akatuambia kwenye Qur’an:

Enyi wanaadamu! Tumekuteremshieni nguo za kuficha tupu zenu, na nguo za pambo. Na nguo za uchamngu ndio bora. Hayo ni katika Ishara za Mwenyezi Mungu mpate kukumbuka.
Qur’an 7:26

0 comments/Maoni: