Nakala iliyopita tuliangalia maradhi yaitwayo Sexual sadism yaani mtu wa jinsia moja anapoona raha kuona mtu wa jinsia nyingine akidhalilika au kudhalilishwa kijinsia.
Leo tuangalie maradhi mengine, ambayo pia huathiri maeneo ambayo zinaa imeachwa huru kwa watu. Maradhi haya ni Frotteurism, yaani maradhi ya mtu kupenda kugusa, kushika au kujiminya (kujigandamiza) kwa mtu au watu wa jinsia tofauti na yeye. Wenye maradhi haya hupendelea michanganyiko ya kiholela ya wanaume na wanawake, na hawa hupenda sana miminyano ya kwenye mabasi, kwenye lifti za kupandia magorofani au sehemu zenye mikutano ya watu wengi, au hata kwenye foleni za huduma.
Katika jamii yetu, maradhi haya yameanza kuingia kwa kasi kama ilivyokuwa kule Ulaya na Marekani. Wale wenye tabia ya kusoma magazeti wanakumbuka miaka michache iliyopita watu kadhaa walifikishwa mahakamani baada ya kukamatwa na kosa la kujiminya kwa wanawake hadi kufikia hatima ya kukidhi haja zao za kimaumbile. Maradhi haya huwatokea wanaume na wanawake kadhalika.
Wanaume wenye maradhi haya katika nyoyo zao wana tabia kwanza kabisa ya kuangalia wanawake wapitao na kuanza kuchunguza ramani za maumbo yao. Kwa vile haya ni maradhi ya kisaikolojia, wanaume hawa hujaribu kuvuta picha ya kuwa na mwanamke amuonaye, na picha hii humpa liwazo la kiakili kama tayari anaye, ingawaje liwazo lile halifikii ukomo au kilele chake.
Mgonjwa huyu huweza hata kufunga safari, akiacha shughuli zake, kumfuatilia mwanamke mwenye umbo lililompendezea hadi mwanamke huyo atakapofika kwenye nyumba na kuingia, ndipo bwana yule hurudi alikotoka, na akiona mwingine mwenye umbo lililomvutia huanza safari. Wanaume hawa ili kuficha maradhi yao, ukiwauliza wanaenda wapi, kwa vile wanajua hawana wanapokwenda zaidi ya kuvutwa na uhayawani wao, huwa na lugha ya "kunyoosha miguu".
Tabia hii ndiyo huwafikisha watu kwenye Frotteurism na kuanza tabia ya kuwashika watoto wa kike na wake za watu. Kesi nyingi za mahakamani sasa hivi ni za wanaume kuwatomasa wanawake bila ya ridhaa yao. Hawa ni wale wanaume ambao hawana nia ya kuwadhalilisha wanawake, bali roho zao hufurahi tu sehemu ya miili yao inapogusana na mwanamke. Wagonjwa hawa ni hatari kwa sababu saa nyingine maradhi yao huyapeleka hata kwa watoto wadogo wa kike, wakijifanya kucheza nao, hata kuwabeba na kuwabusu, kumbe hukidhi haja zao. Tahadhari sana na mtu mzima mwenye tabia ya kuwaita mabinti "mchumba", wengine ni wagonjwa hawa.
Wagonjwa mahututi ni wale sasa wenye kupenda kuminyana kwa mfano siku hizi kwenye madaladala wake kwa waume hukubali tu makondakta wanapowaambia wabanane. Utamkuta mtu mwingine ni mnene, na anapoambiwa akae anaona hapamtoshi, pakiwa na madume wenzake, atagoma kukaa, lakini kama ni wanawake atakwenda aminyane nao. Atajitia kulaani, lakini ndani ya moyo wake anaona raha. Vile vile wanaume wanaweza kuwa wamekaa kwenye siti, nafasi imebaki ndogo. Akija mwanaume mwenzao, wanakuwa wakali kusogea, lakini akija mwanamke wanakuwa wepesi kuminyana ili nafasi kwake ipatikane. Na ukizingatia mambo ya wanawake sehemu za makalio huwa kubwa kuliko wanaume, basi wagonjwa hawa hufurahi zaidi mminyano unapozidi.
Kama basi limejaa na watu wamesimama, hapo ndio utaona fedheha. Watu wameminyana, wake kwa waume, lakini kwa wenye maradhi ndio huona raha na ndio maana wengine yamewatokea kama ya wale waliopelekwa mahakamani. Wale walioshikwa ni wachache tu, wengi huteremka mabasi bila ya kujulikana hali zao.
Kawaida ya utamaduni wa kikafiri (kufru culture) ni kutumia maradhi ya watu katika kupata faida. Ndio maana wenye kuchezesha madisko hutangaza "wanawake kuingia bure" kwenye madisko kule ndio wenye maradhi haya wako wengi, maana huko hukosi wa kuminyana naye, hata kama humjui atokako. Kwa hiyo waminyanaji wengi utawakuta kwenye majumba yanayoitwa ya starehe. Kuongezeka kwa madanguro haya na makasino kwenye jamii yetu ni dalili ya wazi kwamba waminyanaji (frotteurs) wameongezeka mno.
Wanawake pia huugua maradhi haya ya uminyanaji kupenda tu kuminya minya kwa wanaume. Dalili ya mwanamke mminyaji ni kuwa na macho juu, na haoni haya kujichomeka au kupita na kupigana vikumbo vikumbo na wanaume. Halafu huona tabu kukaa kwenye vikao ambavyo wanaume na wanawake wametenganishwa.
Cha kusikitisha zaidi ni kwamba mzazi anaweza akawa na imani na shule ambayo kampeleka mtoto wake, kuwa ni shule ya wasichana watupu, au wavulana watupu, akadhani kuwa mtoto wake yuko salama, lakini shule hizi za watoto wa jinsi moja zina siku zao maalumu, wasichana wanapelekewa wavulana wa shule nyingine, au wavulana wanapelekewa wasichana, halafu wanacheza disko tena usiku. Siku hiyo ya disko ulinzi unakuwapo mkali ili wavulana na wasichana hao "wasitende dhambi", wacheze tu, kwa hiyo usiku kucha wavulana na wavulana watakumbatiana, kuminyana na kutomasana. Haya ndiyo wanayofundishwa watoto. Utakuta mwalimu wa mambo ya starehe amekaa na wasichana wanajadili eti wasichana wanataka waletewe wavulana wa shule gani. Je, hapa hatutengenezi jamii ya waminyanaji?
Rafiki yangu mmoja, Mkristo safi, alinishutumu kwa kusema dini yetu, Uislamu ina ubaguzi, eti hata kwenye ibada tunawatenga wanawake, wao hukaanao bega kwa bega Kanisani kwa jina la Bwana. Alitaka nimpe sababu za sisi kuwaficha wanawake nyuma ya pazia hata kwenye ibada.
Nilimueleza kuwa katika dini zote, Uislamu ndio unaofuata amri za Mungu kimatendo. Kwa mfano, amri ya kuiepuka zinaa ilikuja kwa manabii wote. Tukianza kwa Musa, katika amri kumi imo ile inayosema "usizini". Yesu alipokuja akasisitiza kuwa, imeandiwa usizini, lakini si hivyo tu, bali hata kuangalia kwa jicho la matamanio nako pia ni kuzini. Muhammad (s.a.w.) akaja na "Laa Taqrabuz-Zinaa" yaani usiikurubie zinaa.
Nikamuuliza swali yule rafiki yangu. Kama kuangalia kwa tamaa pia ni kuzini, basi watu wanazini sana, barabarani, sokoni n.k. Je? Tuzini hadi kwenye nyumba za Ibada? Ndipo wanaume na wanawake wanapotengana angalau kwa wasali kwa unyenyekevu.
Hivyo, kuhamasisha wake kwa waume wasio ndugu kukaa mbalimbali kutapunguza wimbi la maradhi ya kupenda kuminyana minyana yaani Frotteurism.
BINADAMU NA UPATIKANAJI WA MVI KATIKA QUR'AN
-
*Msongo wa mawazo katika maisha yetu ya kila siku.*
Sayansi Inathibitisha Kutoka Mvi kwa Haraka kama Ilivyoelezwa Ndani ya
Qur’an
*'MSONGO WA MAWAZO na...
8 years ago
0 comments/Maoni:
Post a Comment