Mojawapo kati ya aibu kubwa ya kitabia ambayo hairekebishiki ni mtu kutoona aibu zake. Aghlabu upotofu na ubaya unatokana na ujinga na ujahili.
Mara nyingi sifa na tabia mbaya zinaposhika mzizi katika moyo wa mtu kutokana na ughafilifu wake, husababisha kusimama shina la mashaka na misiba katika maisha yake. Mtu anapokuwa mtumwa wa ujinga wa nafsi yake, roho ya wema hufa moyoni mwake, huwa mtumwa wa matamanio na tamaa mbalimbali, na hukosa furaha na ufanisi wa daima. Katika hali hii, jitahada yoyote au uongozi wowote wa kimaadili hushindwa kutoa natija.
Sharti la kwanza la kurekebisha nafsi ni kuzijua aibu zake mwenyewe, kwa sababu mtu anapozijua aibu na dosari zake huweza kuikata minyororo ya mabaya na machafu yake na akajiokoa kutokana na hatari ya aibu zisizopendeza ambazo humtumbukiza katika taabu na mashaka. Ni muhimu sana mtu azichungue sifa zake za kinafsi ili aweze kuikuza roho yake, kwani hakuna njia nyingine ghairi ya hii ambayo inaweza kumfikisha kwenye ukamilifu wa kiroho na kimaadili. Kujichunguza nafsi humpa mtu uwezo wa kuziona sifa mbaya na pia nzuri za roho yake, na kuwatoa maafriti kutoka katika mashimo ya roho yake. Kwa njia hii, mtu huweza kusafisha kabisa uchafu wa ndani na kukifanya kioo chake cha ndani king'are.
Ikiwa kwa sababu ya upuuzi wetu hatutaweza kuona sura zetu hasa katika kioo cha vitendo vyetu, tutakuwa tumefanya kosa kubwa lisilosameheka. Kabla ya lolote lile, ni wajibu kwetu kwanza kuzichungua hali zetu za kiroho na kuziona waziwazi sura zetu za ndani, ili tuweze kuzitambua aibu zilizoota mizizi na kustawi katika dhamiri zetu bila ya sisi wenyewe kufahamu. Sisi wenyewe tu ndio tunaoweza kuikata mizizi ya sifa mbaya katika nafsi zetu kwa kufanya uchunguzi na jitihada, na tukazizuia (nafsi) zisidhihirishe ubaya wake katika mazingira ya maisha yetu.
Hapana shaka kwamba kuitakasa na kuirekebisha nafsi sijambo rahisi, bali kunahitaji kuvumilia taabu kwa muda mrefu na kusubiri sana. Ili kuikata mizizi ya mazoea yenye hatari na madhara, na badala yake kupandisha sifa njema na mpya, ni lazima tuzitafute aibu zetu wenyewe-jambo ambalo linalazimu mtu kuwa na azma madhubuti katika kumwongoza kutekelezajambo hilo. Kila tutakapoweza kuzidhibiti tabia zetu na kuziwekea utaratibu maalumn ndivyo zitakavyonyooka na kudarijika nguvu zetu za kiakili. Kila hatua itakayochukuliwa katika njia hii itakuwa na athari zenye manufaa na zenye kudumu ambazo zitadhihirika mwisho wa kazi hiyo.
Mwanachuoni mashuhuri aitwaye Profesa Carl, ameandika:
"Ukitaka sera ya maisha iwe na maana, basi njia bora kabisa yenye faida ni kuzipanga kazi zake za kila siku kila asubuhi, na kuzichungua natija ya kazi hizo kila usiku. Kama vile tunavyopanga kazi zetu: tuanze saa ngapi na tumalize saa ngapi, tuonane na nani, tule nini, tunywe nini na mapato yetu yawe kiasi gani, vivyo hivyo, tupange kwamba tutoe misaada gani kwa watu wengine na tuweke wastani wa namna gani katika kazi zetu. Maadili machafu ni machafu kama mwili mchafu. Watu wengi wamezoea kabla ya kulala na baada ya kuamka kufanya mazoezi ya viungo vyao ili vilainike."
Mazoezi ya kifikra hayana umuhimu mdogo kuliko mazoezi ya kimwili, hivyo, ingekuwa bora kama watu hao wangetumia pia dakika chache kila siku kuziimarisha nishati zao za kimaadili, kifikra na kinafsi. Kwa kutafakari kila siku juu ya mwendo wako na kujitahidi kuifuata vyema sera uliyoipanga, unaweza kwa wakati huohuo kuziimarisha akili na azma zako. Kwa njia hiyo, utaivuka mipaka ya ujinga na utapiga mbizi katika kilindi cha akili ambapo kila mtu huweza kuiona sura yake mwenyewe bila ya kificho chochote. Mafanikio yetu katika kutekeleza kanuni za maisha zinategemea sana maisha yetu ya ndani kama vile ambavyo tajiri na mtafiti wanavyopanga kwa uangalifu daftari na nyaraka zao za utafiti. Ni lazima kila mtu, awe maskini au tajiri, mzee au kijana, msomi au mjinga, arekodi kila siku mazuri na mabaya aliyoyafanya. Kwa kutekeleza kwa uvumilivu utaratibu huo ndipo miili na roho zetu zitakapoweza kubadilika kidogokidogo."
Mtu wa maana mwenye mawazo maangavu huzipitisha jitihada na nishati zake katika mikondo inayofaa. Mtu mwenye heshima ya kiasi chochote kile ana haki ya kuheshimiwa na wengine; hivyo, hujiepusha kabisa na mambo yanayowaudhi watu, kwa sababu kitambulisho bora kabisa cha mwungwana ni tabia yake ya kila siku inayoonekana kwa kuingiliana na watu.
Mzee nnoja aliulizwa: "Jambo gani ni gumu kabisa kuliko yote, na jambo gani ni rahisi kabisa kuliko yote?"
Akajibu: "Jambo lililo gumu kabisa ni mtu kujijua mwenyewe, na jambo lililo rahisi kabisa ni kutoa aibu zawengine!"
Kikundi cha Watoao Aibu za wenzao:
Baadhi ya watu wana tabia mbaya ya kupenda kupeleleza udhaifu na aibu za wengine na kuchungua siri za watu. Huwachambua na huwasengenya kwa kejeli na mzaha watu wengine ilhali wao wenyewe wana aibu na udhaifu mwingi ulioshinda mema yao.
Wanazipuuza aibu zao na wanazifumbia macho, na badala ya kuzisafisha nafsi zao wenyewe ndio kwanza wanazitafuta aibu na dosari za wengine.
Kutoa aibu ni katika sifa ambazo huharibu maisha na hushusha hadhi ya kimaadili.
Mambo yanayomshawishi mtu kuwahizi na kuwatolea watu aibu zao yanatokana na aina moja ya hisia ya udhalilifu na uduni ambayo huchochewa na huimarishwa na majivuno na ubinafsi. Uharibifu unaotokea katika maadili na roho za watu kutokana na tabia hiyo huwafanya watoe uamuzi usio sahihi juu ya watu wengine na wao wenyewe kujifikiria kuwa ni watu jasiri na watakatifu wasio na mapungufu.
Wakosoaji wanapoteza bure uwezo wao wa kuyachunga mambo yasiyopendwa na akili, kwa sababu hutumia jitahada zao katika kuwachungua watu na kupeleleza vitendo vyao ili wazipate aibu na dosari zao na waanze kuwachambua na kuwasema. Huendelea kutumia mbinu hiyo ya uharibifu mpaka pale wanapopata fursa ya kuwaumbua na kuwatweza watu. Hapana shaka kwamba kwa kudadisi na kupeleleza kwao mienendo ya wengine, kunawanyima fursa ya kutosha ya kuchunguza tabia na vitendo vyao wenyewe, na kwa sababu hii, hushindwa kufuata mwendo mwema na safi. Kwa kawaida, watu kama hao hukosa unyofu na haya kwa kadiri kwamba wanapojichafua katika mwendo huo huona si lazima kwao kuweka heshima ya mtu yeyote, na hata huwa hayumkiniki kuingiliana kwa moyo safi na marafiki walio karibu nao sana. Mtu anapokwenda kwa rafiki yake hutoa aibu za watu wengine, lakini anapopata uwanja wa kushambulia, haachi kumkosoa, kutoa aibu na kumchambua rafiki yake mbele ya wengine. Kwa hivyo, mtu mwenye tabia ya kutoa aibu za watu hawezi kujipatia marafiki wa kweli ambao watampenda na watamfurahisha moyo wake kwa mapenzi na upole wao.
Mwanadamu mwenyewe ndiye mwenye kujenga heshima na utukufu wake. Mwenye kuvunja heshima ya wengine, hapana shaka atajivunjia heshima yake mwenyewe.
Huenda mtafuta aibu za watu asifahamu matokeo mabaya ya tabia yake, lakini akipenda au asipende hataweza kuepukana na radiamali na bidhaa ya matusi na ufidhuli wake. Tabia hii husababisha nyoyo za watu kuvunjika, huleta chuki na hata uadui, na matokeo yake ni juto la Firauni.
Wahenga wamesema:
"Maneno si kama njiwa ambaye anaporuka hurejea tena tunduni mwake." (Hivyo, maneno yakikudondoka hayarejei tena mdomoni mwako!)
Mtu anayetaka kuishi na kuingiliana vizuri na watu, inampasa azijue nyadhifa zake. Siku zote awe anaangalia mema na mazuri ya watu, na avisifu na kuvithamini vitendo vyema.
Katika maisha ya kijamii, mtu anatakiwa ageuze mwendo na tabia ambazo zinavunja heshima za watu na misingi ya urafiki. Chakubimbi atakayeacha kutoa aibu za marafiki zake, atajenga msingi madhubuti wa mapenzi ya kidhati kati yake na marafiki zake. Usafi wake wa moyo na unyofu wake utaimarika zaidi atakapoiona aibu ya rafiki yake, lakini badala ya kutoa aibu hiyo mbele ya watu wengine, atatafuta fursa nzuri ya kumtanabahisha rafiki yake juu ya aibu hiyo na kumwomba ajirekebishe. Wakati wowote mtu akitaka kumwonesha rafiki yake makosa yake, itambidi atumie maarifa maalumu ili asije kukasirika na kuchukiwa.
Mwalimu mmoja wa maadili amesema:
"Unaweza kumjulisha mwenzako juu ya kosa lake bila ya kutaka kumwambia kwa kumtazama, kubadilisha sauti au kwa ishara ya viungo vyako. Kwa sababu ikiwa utamwambia: 'Umekosea,' hatakubali kwa kuwa utakuwa umetusi kinagaubaga akili yake, uwezo wake wa kufikiri na kutia dosari kujiamini kwake. Kwa kitendo hicho utamfanya akupinge na asibadilishe fikra zake wakati wowote. Huenda ukamtolea hoja za kede kede na zenye mashiko lakini hutaweza kugeuza maoni yake ya ndani kutokana na kitendo chako cha kumwumiza moyo wake.
Unapozungumza usijaribu kabisa kuanza kwa maneno haya: 'Mimi nakuthibitishia.... Mimi nitakupa hoja zangu', n.k. kwa sababu maneno haya yanamaanisha kwamba wewe ni mwerevu zaidi kuliko yeye. Kitendo cha kusahihisha fikra za watu kwa mara nyingi huwa ni kazi ngumu, basi kwa nini ujitie zaidi matatani kwa kutumia mbinu isiyofaa na kujiwekea vizuizi vigumu zaidi? Unapotaka kuthibitisha jambo moja, angalia kwamba wengine wasitambue makusudio yako, na tumia maarifa na uhodari ili wengine wasifahamu unalolikusudia.
Kumbuka msemo wa yule mshairi mashuhuri unaosema:
'Wafunzeni wengine bila ya kuwa wafunzaji."
Ili kuhifadhi umoja wa jamii, binadamu anawajibika kuheshimu misingi ya adabu ya maisha na anakatazwa tabia ya kuumbua na kuambaamba ambayo husababisha utengano na kuvunjika uhusiano wa ki'rafiki. Ni lazima Watu wawekeane heshima zao na wajiepushe kabisa na tabia ya kuhiziana, kudharauliana na kutukanana.
BINADAMU NA UPATIKANAJI WA MVI KATIKA QUR'AN
-
*Msongo wa mawazo katika maisha yetu ya kila siku.*
Sayansi Inathibitisha Kutoka Mvi kwa Haraka kama Ilivyoelezwa Ndani ya
Qur’an
*'MSONGO WA MAWAZO na...
8 years ago
0 comments/Maoni:
Post a Comment