TRANSSEXUALISM

Leo tuangalie maradhi mengine yaitwayo Transsexualism. Mwenye maradhi haya anaitwa Transsexual (inasomwa Trans - sekshual). Mgonjwa huyu huwa na tamaa ya kuwa na jinsia tofauti na ile aliyonayo, kwa mfano, mwanaume anatamani kuwa mwanamke, na mwanamke anatamani kuwa mwanaume.

Wagonjwa wa Transsexual hufikia kiwango cha kutaka kubadilishwa maumbo yao, hata kwa njia ya operesheni au kwa kutumia madawa yanayoweza kubadilisha hali zao za asili.

Kule Ulaya na Marekani, na sehemu nyingine zinazofuata nyayo za "maendeleo", ambako watu wamekubuhu katika fani ya ufuska, baadhi ya watu wamediriki kwenda hospitali na kufanyiwa operesheni kuondolewa sehemu zao za viungo zinazowanasibisha na jinsi yao asilia.

Katika jamii yetu, japo hakuna hospitali za kubadilisha jinsi za watu, wapo wanaume wanaoonyesha silka za kike katika maisha yao. Mfano hai ni pale tunapowaona watu waliopewa majina ya "anti" fulani, au wale wanaoshiriki katika ngoma za "kibao kata". Hawa ni wagonjwa mahututi.

Maradhi haya hupenyeza vile vile hadi kuingilia majukumu ya kijinsia. Kwa mfano, katika jamii yoyote ya watu waungwana, mahusiano ya ndoa huwa baina ya watu wenye jinsia tofauti, lakini tunasikia na kusoma kwenye vyombo vya habari kwamba kule Ulaya, kwenye maendeleo wanaume kwa wanaume wanafunga ndoa, tena Kanisani; na vile vile mahusiano ya wanawake kwa wanawake (Lesbianism) ni jambo la kawaida lililopewa kibali na mamlaka ya nchi.

Katika hali ya kimaumbile, viumbe hutofautiana kijinsia katika hali tatu tofauti, ambazo kitaalamu zinaitwa gender. Kuna viumbe vyenye hali ya kiume (Masculine gender), vyenye hali za kike (feminine gender) na vyenye hali haidi, yaani isiyo ya kike wala ya kiume (neutral gender). Transsexualism ni hali ya mtu kujibadilisha (kifikra au kifizikia) kutoka katika hali yake ya kijinsia ya asilia, na kujifanya kuwa na hali nyingine. Hivyo, hata kujitoa katika hali ya kike au ya kiume na kujiweka katika hali haidi (isiyo ya kike wala kiume) pia ni Transsexualism.

Wapo wanawake, kwa mfano, waliotoka katika hali yao ya kike (feminine gender) na kuwa haidi (neutral). Hawa wamefikia hali hii baada ya kuielewa vibaya dhana ya "ukombozi wa mwanamke".

Dhana hii ya "ukombozi wa mwanamke" ni dhana nzuri, kwani ni kweli wapo wanawake wengi wanonyanyaswa, kuonewa na kudhulumiwa kutokana na mila na mienendo ya jamii zao, lakini dhana ya "usawa" imewafanya wanawake wengi kutaka kuwa "sawa" na wanaume hata kimaumbile.

Jamii za kinyonyaji zimechukua fursa (advantage) ya propaganda ya "usawa" wa wanawake na wanaume kwa kumtaka mwanamke amenyeke katika kazi sawa na wanaume bila ya kujali maumbile yake. Sasa hivi katika jamii yetu kumeletwa miradi mbalimbali, eti ya kuwakomboa wanawake, na kumeenezwa vitengo vinavyoshughulikia "mitandao" ya kijinsia, lakini ukweli wa mambo ni kwamba nchi hizo hizo zinazotaka kuleta ukombozi ndizo hizo zilizoleta ukoloni na zinatuletea ukoloni mamboleo, na ndizo hizo hizo zinatuletea dhana ya "ukombozi". Mimi sioni ukombozi unaofanyika zaidi ya kuwatia wanawake maradhi, hasa haya ya kisaikolojia kama vile Exhibitionism (wendawazi), Lesbianism (usagaji) na haya maradhi ya wanawake kutaka kuwa sawa na wanaume ambayo tunayaita kichaa cha kijinsia. Maradhi yanayosumbua nchi zao, na kuziparaganyisha familia zao wanaya leta huku kwetu.

Sehemu nyingi za kikazi zilizokuwa mahsusi kwa wanaume sasa hivi zimeshikwa na wanawake, na jamii hizi zianzowafanyisha kazi wanawake sambamba na wanaume, chini ya nembo ya "usawa", hujisifia kuwa na idadi kubwa ya wanawake maofisini na viwandani, lakini watu, hata wanawake wenyewe, wamesahau kuwa mwanamke ana kazi kubwa ambayo katika Uislamu huhesabika kama Jihaad.

Dunia leo ina mamilioni na mamilioni ya watu. Kila mwanaadamu unayemuona anatembea katika mgongo wa ardhi ni lazima alimtesa mwanamke. Mwanamke alimbeba binaadamu huyu tumboni mwake, kwa tabu na mashaka makubwa, kwa muda wa miezi tisa, na siku ya kujifungua, mwanamke alipata uchungu mkubwa unaosemekana kuwa unakaribia uchungu wa kutoka roho (na wanawake wengine hufa kwa uchungu huu).

Baada ya hapo, mtoto anakuwa akitegemea kumnyonya mama yake kwa zaidi ya mwaka mmoja. Huyu mwanamke pia anakuwa mwalimu wa kwanza wa binaadamu. Ukifikiria yote haya ndipo inakuwepo hoja kuwa, mwanaume, ambaye hapati tabu katika mahusiano yake na mwanamke, zaidi ya raha za kimapenzi, inabidi yeye ndiye ahenyeke kwa uchungu na ugumu wa kazi za uzalishaji mali katika jamii, lakini mtu anang’ang’ania wanawake wawe sawa na wanaume katika uzalishaji mali, wakati yeye mwanaume hawezi kuwa sawa na wanawake katika uzalishaji watu.

Kwa vile wanawake wamevamia uwanja wa uzalishaji mali sawa na wanaume, basi wengi wao wanaona iko haja ya kuepuka jukumu lao la kuzaa watoto, ili waweze kufanya kazi kwa nafasi, sawa na wanaume. Basi wanawake hawa hukwepa uzazi (asili yao) kwa kuzuia mimba, kunyofoa mimba au kuua watoto, maana wasiposhika mimba kama wanaume wasivyoshika mimba ndio watakuwa wachapakazi wazuri. Matokeo yake, wanawake wanatoka kwenye uanauke na kuwa hawawezi kuwa wanaume, wanabakia kuwa haidi (neutral).

Kwa vile wanaume nao eti wanachangia sana katika "kuharibu" ufanisi wa wanawake, nao wanapigwa propaganda hadi wanakubali kufungwa kizazi. Utakuta mwanaume anafunga kizazi, eti kwa kuogopa "kumuathiri" mke wake. Basi mwanaume huyu naye huenda hospitali, akaonyoosha miguu, na wanaume wenzake wakamuondoa uwezo wake wa kuzaa. Anakubali kuwa haidi. Mwanaume anayejitoa uanaume kwa kuogopa kumzalisha mwanamke, ni wa ajabu sana. Kwa vile anajibadilisha kuwa haidi, basi na yeye anakuwa ni Transsexual, kwa vile kajitoa silka ya uume (masculinity) akajitia au akatiwa uhaidi (neutrality).

Kuna suala la kuwa na mke zaidi ya mmoja, ambalo pia hupigiwa kelele. Eti watu hung’ang’ania usawa, mume mmoja kwa mke mmoja (one-to-one-function). Suala la kuzingatia hapa ni kwamba, kuhusu uzazi, mwanamke ana uwezo wa kushika mimba ya mwanaume mmoja tu kwa mwaka mzima (miezi tisa ya kubeba mimba na angalau miezi mitatu ya kunyonyesha kabla ya hali ya kubeba mimba nyingine haijawa tayari). Lakini mwanaume, katika mwaka huo mmoja ana uwezo wa kuwapa mimba wanawake wengi mno. Mwanaume mwenye nguvu anaweza kuwapa mimba hata wanawake watatu kwa siku moja.

Lakini tumchukue mwanaume dhaifu, ambaye anaweza kumpa mimba mwanamke mmoja kila siku, ambaye yuko katika hali ya kuweza kushika mimba. Kwa hiyo, kwa wiki anaweza kuwapa mimba wanawake saba. Kwa mwezi wanawake 28. Kwa hiyo kwa mwaka, kama kila mwanamke atakayekutana naye atakuwa katika siku muafaka, ataweza kuwapa mimba wanawake 330 (28 mara miezi 12).

Hivyo kinadharia, kama kungekuwa na kazi maalum ya kuzaa ili kuijaza watu jamii fulani yenye hatari ya kutoweka, basi mwanaume mmoja anahitaji wanawake 330 kwa mwaka, wakati mwanamke mmoja anahitaji mwanaume mmoja tu kwa mwaka. Sasa kutaka mwanaume awe na mke mmoja tu, hata kama kuna sababu ya kuongeza mwingine, angalau mmoja ni kubadilisha jinsi ya mwanaume . Na hii ni kumgeuza Transsexual. Kimaumbile, mwanaume anahitaji zaidi ya mke mmoja, ibaki matashi yake tu na sababu nyingine za kiuwezo.

"Usawa" na uwepo, lakini tusibadili asili ya maumbile ya mtu. Shetani hupenda kuwashawishi watu wabadilike kinyume na Mwenyezi Mungu anavyowataka wawe, ndio maana akasema:

"Na nitawapoteza na nitawatumainisha na nitawaamrisha (ninavyotaka mimi) ... na nitawaamuru, nao watabadili umbile la Mwenyezi Mungu (alilowapa)..."
Qur’an 4:119

Waislamu tunatakiwa tuwe na msimamo wa Nabii Mussa, alipomjibu Firauni, kwa kumwambia:

"Mola wetu ni yule aliyekipa kila kitu umbo lake kisha akakiongoza (kufuata kinachoafiki umbo lake hilo)".
Qur’an 20:50

0 comments/Maoni: