Utambuzi wa mu’min kuwa yumo kwenye mtihani humuongoza azingatie mambo yake kwa sura ya kuyaangalia mbeleni. Lakini “kuyaangalia mambo mbeleni” kunamaanisha nini hasa?
Ijapo taabu na shida humkumba binadamu, hali hio hakika si ya kudumu milele bali ni ya muda wa kupita tu. Mtu, kwa mfano, anaweza kutuhumiwa kiuwongo kuwa amefanya hatia fulani na kudhulumiwa. Bila shaka utakuja wakati ukweli wa mambo utadhihirika. Hata kama taabu inayompata mtu huyo haitakwisha hapa duniani, kwa ajili ya dhuluma hiyo, wale waliosababisha hiyo dhuluma watapata jazaa yao kamili siku ya Kiyama. Na vilevile, yule aliyedhulumiwa anatarajia kupokea zawadi nzuri sana kwa subira yake katika siku hiyo. Wakati unakwenda haraka sana, na kama mambo mengine yale, hali hii itawadia mwishowe kama vile kasi ya mwendo wa kufumba na kufumbua jicho. Pia Qur’ani inadhihirisha kuwa dhiki hufuatiwa na faraja kwa Mwislamu:
Basi kwa hakika baada ya dhiki faraja. Hakika baada ya dhiki faraja.
(Surat Al-Inshirah, 5-6)
Mu’min anaamini kwa uadilifu kamili na kwa haki iliyo ya daima ya Mola wetu, anategemea faraja baada ya dhiki, na hakati tamaa kwa hali yoyote ile. Anakumbuka vyema kuwa taabu anayoipitia itabadilika mbeleni kwa kuja kuwa furaha kubwa kwake hapa duniani na Akhera.
Mwislamu anajua kuwa anaitizama qadari. Lengo moja zuri sana katika siri hii ni kuangalia kila kitu kile kwa nia ya kumuamini Allah kabisa, kwa radhi ilio timamu na utiifu kamili.
Tusisahau kuwa msimamo wa hali hii ni pekee tu kwa wale waumini wa kweli wa Mwenyezi Mungu, kwa wale ambao wameridhia kabisa hali ya qadari ndio wanaoweza kuutambua kikamilifu. Watu wasiokuwa na dini, kwa upande mwengine, wanaangukia chambo cha kufa moyo na kukata tamaa, huwa na wasiwasi na kuonekana kubanwa na shida nyingi sana kwa sababu ya kukosa kuwa radhi na mambo ya qadari, wanadhania kuwa hakuna njia ingine yoyote ile mbele yao. Kwa vile hawana matumaini wala mategemeo ya Akhera, daima huwa ni watu wenye kuhangaika kwa wasiwasi na taabu nyingi. Hali ya watu kama hao inaelezwa hivi katika aya ingine:
Basi Yule ambaye Allah anataka kumwongoza, hufungulia kifua chake Uislamu. Na Yule ambaye Allah anataka kumhukumu kupotea, hufanya kifua chake kuwa na dhiki na taabu kama anaepanda angani. Namna hii Allah anajaalia uchafu juu ya wale wasioamini.
(Surat al-An'am, 125)
Hali hii ya taabu ilioelezewa kwenye aya ni kidonda cha kujitonyesha, hali ambayo inachimbukia kwenye shina la ukosefu wa watu kuiamini qadari ilioumbwa na Mwenyezi Mungu. Uhakika wa kuwa Mwenyezi Mungu, Mfalme, Mwenye uhai wa maisha na milele, anayeendesha qadari ya mtu, ni baraka kubwa sana kwa yule mtu aliyeamini. Lakini kwa wale wenye imani dhaifu na wale wasioamini basi hawana uwezo wa kutambua thamani ya baraka hiyo. Hawawezi kuwa radhi na qadari, kwa hiyo wanataabika katika kila wakati wa maisha yao. Hali hii hasa ni natija ya athari ya ukosefu wao wa kumuamini Allah vilivyo ndio maana inakuja kuwakumba maishani mwao hapa duniani. Watu hao wanajidhulumu nafsi zao wenyewe.
Hakika Allah hawadhulumu watu chochote; lakini watu wanajidhulumu wenyewe nafsi zao.
(Surat Yunus, 44)
0 comments/Maoni:
Post a Comment