Uislamu ni nini?

Uislamu ni ile imani kuwa muumba ni mmoja tu kwa dhati na sifa zake. Nguzo nyingine za imani zinajengwa juu ya imani ya Mungu mmoja wa kweli. Imani juu ya maisha baada ya kifo, imani juu ya Malaika wa Mungu, vitabu vyake na kudra na tafsiri ya vitendo ya imani hii ni Swalah, Zakaah, Funga na Hija.

Muhammad (saw) alitumwa kuwaita watu kwa Mwenyezi Mungu na kuwafundisha namna ya kutimiza jukumu waliloumbwa kwalo.
Nalo ni kumuabudu Allah. Wengi miongoni mwa watu aliowalingalinia walikuwa na dhana hafifu juu ya Mungu. Walimwamini Mungu lakini walimshirikisha na vijiungu vidogovidogo, wengine walikuwa Makafiri kabisa au wamuumini wa maumbile.

Uislamu ndio dini ya maumbile bila ya mashindano.
Yaani Uislamu ndio mfumo wa maisha unaokwenda sambamba na maumbile ya mwanadamu na ulimwengu wake. Kwa mantiki hii tunaweza kusema kwa kinywa kipana kabisa kwamba Uislamu ndio dini ya jamii ya wanadamu.

Uislamu haukuitwa dini ya jamii ya wanadamu kwa kuropoka tu au kwa hamasa na jazba. Imeitwa hivyo kwa sababu zifuatazo:-
  • Imesheheni desturi zinazokubaliana na akili.
  • Ina uongofu unaouangazia na kuupa nuru moyo.
  • Inabeba maendeleo yanayofaa kwa hali, mahala na zama zote.
  • Ina sheria inayokidhi hali na mahitaji yote ya jamii katika nyanja zote za maisha.
  • Ina dhana ya usawa unaowaunganisha pamoja watu wote bila ya kujali lugha, rangi au hali zao za kimaisha.
Sheria yake ina dhima ya kumpa mwanadamu maisha ya amani, utulivu, raha, furaha na heshima katika nafsi, mwili, akili na mali.

Haya na mengineyo ndiyo yanayoufanya Uislamu uwe ni dini inayokubaliwa na kuridhiwa na mwanadamu kwa kuwa inayogusa moja kwa moja maumbile yake.

UISLAMU NI NINI?
Uislamu ni mfumo kamili na sahihi wa maisha unaozienea nyanja zote za maisha ya mwanadamu katika hali, mahala na zama zote.

Mfumo uliofumwa na Allah Mola Muumba ulimwengu na walimwengu kwa ajili ya waja wake na akawaleta kupitia mitume wake. Tangu Nabii Adamu mwanadamu wa kwanza mpaka Nabii Muhamad Mtume wa mwisho. Ili uwe ni muongozo na katiba ya kukiendesha kila kipengele cha maisha yao katika maisha haya ya mpito ya ulimwengu huu yenye dhima ya kuwaandaa na maisha ya milele ya Akhera.

Ufuatao ni mukhtasai wa baadhi ya vipengele vya Uislamu ambavyo, mara nyingi huwavutia wasio Waislamu;

1. Uislamu unakubaliana na akili. Mafundisho yake hayapingani na mantiki na hoja.

2. Uislamu haupendelei imani ya kibubusa bali unapenda imani ya kuhoji misingi ya imani

3. Uislamu unapendelea njia ya kati na kati yenye tahafifu na upole.

4. Unaweka Urari kati ya Duniya na Akhera.

5. Uislamu sio dini mpya, bali ni dini ya Manabii wote wa Mungu hivyo Uislamu unawapa heshima manabii wote na ujumbe wao.

6. Uislamu unaitazama duniya kuwa ni njema na maisha kama neema na fursa muhimu ya kupatia mema ya akhera.

7. Usahihi na hifadhi ya matini ya asili ya Qur'an ni jambo linalokubaliwa na wanahistoria- Waislamu na wasio Waislamu.

8. Mvuto, upokezi na ukamilifu wa Qur'an ni miongoni mwa mambo yanayovutia. Ni kitabu chenye maudhui mazito kiasi kwamba watu wanahoji kama kweli binadamu angeliweza kukiandika.

9. Qur'an inataja hakika kadha wa kadha za kisayansi nyingi kati ya hizo hazikuwa zikifahamika na hazikujulikana hadi nyakati za karibuni tu hapa.

10. Uislamu unafundisha itikadi ya utakaso ya kumpwekesha Mungu na ibada ielekezwe moja kwa moja kwake yeye pekee bila kupitia njia nyingine- binadamu au nguvu za kimaumbile.

11. Hakuna ukasisi katika Uislamu. Kila mmoja anahusiana na Mungu sawa na mwingine na anawajibika kwa maisha anayoishi.

12. Hakuna urithi wa dhambi au wema kila mmoja anazaliwa na rekodi yake safi. Matendo yanahukumiwa kwa nia.

13. Uwokovu haupatikani kwa imani na amali njema pekee imani na amali ni muhimu lakini kikubwa zaidi ni rehema na msamaha wa moja kwa moja wa Allaah.

14. Mafundisho ya Uislamu yanawiana na silka njema ya binadamu.

15. Uislamu unatia nguvu udugu wa wanadamu wote [kama watoto wa Adam] na udugu wa imani [kama Waislamu] vyote kati yao vinafuta rangi, taifa, kabila, koo, jinsia na tabaka

16. Ubora wa mtu [mwanaume au mwanamke] unategemea UchaMungu ambao Mungu ndiye ajuae vizuri zaidi.

17. Uislamu una uwezo mkubwa usio kifani wa kutatua matatizoya kibinafsi na kijamii kuliko dini nyingine.

18. Katika Uislamu, Manabii ni vigezo vya maadili mema, lakini ni wanadamu kamili, si Mungu na wanawajibika kwa imani na matendo yao kama wengine.

19. Katika Uislamu. Uwokovu hauishii kwa wafuasi wa Mtume Muhammad [Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam] bali uko wazi kwa wote wanaoutafuta kwa dhati ukweli ambao waweza kuwa hawana hatia kwa kutoijua Qur'an au ukweli wa maudhui yake. Anaowakataa Allaah ni wale wanajua ukweli lakini hawataki kuukubali.

20. Maisha ya Mtume Muhammad yamehifadhiwa vema katika vitabu na yeye ndiye anayefaa kuwa kigezo kwa mambo mengi, kijana, mfugaji, baba, mtu aliyedhulumiwa, kiongozo aliyelazimika kuhama nchi yake, Nabii, kiongozi wa nchi aliyefanikiwa, kiongozi wa kijeshi, hakimu, mtengenezaji wa amani na kadhalika. Hakuna maisha ya Nabii mwingine yaliyoandikwa kwa ukamilifu na kuhifadhiwa namna hiyo, yanayoweza kuwa kigezo cha mwenendo wa maisha katika mambo na mazingira mbalimbali.

21. Uislamu unatoa muundo wa utaratibu mzima wa maisha-kijamii, kiuchumi, kisiasa, kisheria, kifalsafa na kisayansi, ukioanisha miongozo yake ya kiroho, kimaadili na vipengele vyote hivi vya maisha yetu, Uislamu hauruhusu mgawanyo wa mambo ya kiroho na ya kisekula.

22. Swalah tano njia nyepesi, ya mara kwa mara na ya utulivu ya kudumisha mawasiliano na muumba wetu. kwa vile “duniya mzima ni msikiti” zinaweza kusaliwa mahali popote pasafi kwa mtu mmoja moja na kwa jamaa. Zikisaliwa kwa ikhlasi na kwa lengo, zinasaidia kuondosha dhana ya kuabudia duniya, kuondosha maovu na mapungufu.

23. Adhana za vipindi vitano vya Swalah kila siku, huwa kama ukumbusho wa mara kwa mara wa kumuelekea Allaah kwa shukurani na toba, kuomba muongozo wake na neema zake.

24. Swalah za jamaa ambazo ndizo zinazohimizwa zaidi kuliko Swalah za mtu mmoja mmoja kuimarisha mshikamano wa jamii na udugu

25. Uislamu hauhitaji mabadiliko ya jumla ya utamaduni-bali kufanya tu mambo fulani na kuyaepuka mengine, yote kati yao yakichangia katika mfumo wa maisha wa kufaa na kunufaisha, wenye misingi ya haki, wema, heshima, uungwana, ukweli na huruma kwa wasiojiweza.

26. Uislamu unawataka watu wawe wema na wafanye hisani sio tu kwa malipo binafsi bali hata bila malipo kwa ajili ya kutafuta radhi za Allah.

0 comments/Maoni: