No Valentine (Ni Haram)



Katika nchi nyingi hususan za Ki-magharibi, msemo wa “acha msimu wa mapenzi uanze”unaanza kusikika tena. Ni wakati kama huu wa Februari 14 ndani ya kila mwaka ambapo maua, stika, kadi za mapenzi, kukiri makosa ya kimapenzi na miadi yakimapenzi hutolewa baina ya wapendanao.

Februari 14 inajulikana kama siku ya St. Valentine. Huu ni wakati ambao kwa karne kadhaa umewekwa maalum wa kuwatukuza wapendanao. Katika siku hii watu hutuma ujumbe wa“penzi la kweli (true-love)” kwa wanaowapenda. Watoto nao pia huwa wanatengeneza kadi za Valentine na wanapokuwa katika viwanja vya michezo na huhimizwa na kuhamasishwa kuwapatia kadi hizo wanaowapenda.

Je kuna madhara gani katika hayo? Mtu anaweza kusema, mwisho wa yote, hii ni siku ya kuwaonyesha watu jinsi unavyowapenda na kuwajali, na kwa watoto huwa ni kama kujifurahisha tu. Lakini Je umeshawahi kujiuliza St. Valentine alikuwa ni nani hasa, na wapi utamaduni huu wa St. Valentine umetoka?

Mnamo karne ya tano Kanisa katoliki lilitaka kumaliza ukuaji wa mila za kipagani zilizokuwa zikifanywa naWaroma kila mwaka tokea karne ya 4 BC. Walikuwa kila mwezi wa Februari wa kila mwaka wakichezesha kamari maalum kwa kuwashirikisha vijana wao wa kiume kwa mila zao za kidini kwa ajili ya kupeleka zawadi kwa “mungu” Lupericus. Vijana wa kike walishiriki katika kamari hiyo kwa kuweka majina yao kwenye kisanduku maalum na kisha vijana wa kiume huchagua majina hayo. Kupitia kamari hiyo msichana aliyebahatika kuchaguliwa na mvulana huwa na mvulana huyo kwa mahusiano ya kimapenzi kwa kipindi cha mwaka mzima hadi kamari ya mwakani.

Kanisa halikufurahishwa na hali hiyo na mpango huo wa kiibada za kipagani na hali ya kufanya mapenzi kiholela kupitia kamari, na likaamua kutokomeza mila hiyo kwa kuchagua “mpenzi mtakatifu”, ambaye hutunukiwa badala ya mila za kamari za “mungu” Lupericus. Wakamchagua askofu kwa jina la Valentine, mtu ambaye alihukumiwa kuuwawa katika karne ya 3 AD kutokana na kukaidi amri ya mtawala (Emperor Claudius) aliyepigta marufuku kuoa wakati wa utawala wake kwa madai ya kuwa wanaume waliooa wanafanya vibaya vitani na wakati mwengine huwa hawataki kuziwacha familia zao na kwenda vitani. Valentine alikuwa anawaalika watu wanaotaka kuoana na kuwaozesha kwa njia ya siri. Kwa sababu hiyo aliuliwa. Kabla ya kuuliwa alikuwa akituma ujumbe wa kimapenzi kwa binti wa mlinzi wa jela aliyewahi kuwa na mahusiano naye kimapenzi wakati alipokuwa gerezani kabla ya kuuliwa. Ujumbe ulikuwa ukisomeka “kutoka kwa wako Valentine (from your Valentine)”.

Kwa hivyo, kanisa katoliki likamchagua askofu huyu kwa jina la Valentine ili awe mfano wa kuigwa kwa wapendanao na kutokemeza ibada za kipagani za kufanya mapenzi kiholela kwa kuchagua mwanamke kwa njia ya kamari.

Mengi yanaweza kusemwa kutokana na utamaduni huo, lakini kuna fikra moja msingi ambayo Waislamu wanapaswa kuwa nayo. Uislamu ni mfumo kamili wa maisha uliokamilika ambapo kwamba chimbuko lake ni Hukmu za Ki-Sheria. Hukmu hizo za kisheria ndio chanzo cha mila, desturi, na vitendo ambavyo Muislamu huruhusiwa kuvifanya. Kutokana na chanzo hicho (i.e Hukmu za Ki-sheria), Uislamu waziwazi umeharamisha kushiriki katika Sikukuu za kikafiri, kama vile kusherehekea sikukuu ya Valentine ambayo mwanzoni ilikuwa ya kipagani na kisha ikaboreshwa tena katika sura tofauti kidogo.

Uislamu kupitia Hukmu za Kisheria umeeleza kwa uwazi ni zipi sikukuu za Kiislamu na jinsi gani sikukuu za kikafiri ziangaliwe.
Imeelezwa kwamba, Anas bin Malik (ra) amesema:“Wakati Mtume (saaw) alipokuja Madina, watu walikuwa wana sikukuu mbili kutoka katika masiku ya ujinga”. Yeye Mtume (saw) akasema: “Wakati nilipokuja kwenu, mlikuwa na sikukuu mbili mlizokuwa mkisherehekea katika kipindi cha ujinga. Allah (swt) ameziondoa na kuwapatia badala yake, Sikukuu ya kuchinja (Eid-l-adha) na Eid-el-Fitr”. (Imam Ahmad). Kwa hivyo, japokuwa kuna sikukuu nyingi katika ulimwengu lakini hizo ndio sikukuu zetu kama Waislamu ambazo Allah (swt) ametuchagulia.

Kwa kweli, kuigiza mila na vitendo vya kimagharibi ni mbinu ambazo makafiri hutumia kuwatumbukiza Waislamu katika mwenendo usiokuwa wa kiislamu. Kila mara makafiri wanafikiria jinsi gani wataweza kuwamaliza kabisa Waislamu, na kujaribu kupanga mbinu mbali mbali ili kuweza kutimiza azma yao ya kuutokomeza kabisa Uislamu.

Katika jamii leo, dhana ya mchanganyiko usiokuwa na mipaka baina ya wanawake na wanaume ni jambo linalopigiwa debe na makafiri na kupandikizwa katika mabongo ya Waislamu ili lionekane kuwa ni jambo la kawaida, na kututaka tuzikubali fikra zao hizo ati kwa kuelezwa kwamba sisi ni sehemu katika jamii yenye mchanganyiko wa mila (multicultural society). Umma wa Kiislamu unatakiwa uwe makini na kutambua mbinu ambazo makafiri hutumia, ili tuweze kuhuisha uelewa wetu juu ya miondoko yetu ya kimaisha kama ilivyopokelewa kutoka katika Qur-an na hadithi za Mtume (saw) jinsi gani Waislamu wanatakiwa waishi baina ya wanawake na wanaume, mahrim na wasiokuwa mahrim, katika maisha ya ndani (Private life) na maisha ya nje (Public life), tutakuta kuwa Uislamu haukuacha kitu juu ya hayo.

Sikukuu ya Valentine ni moja ya mifano, ambapo mahusiano nje ya taasisi ya ndoa si tu huruhusiwa bali pia huhamasishwa. Vyombo vya habari pamoja na matangazo mbali mbali hupigia debe mahusiano hayo hasa katika sikukuu hiyo. Ni ukiukaji wa Sheri’a ulioje, ambapo mila za kimagharibi zinazotokamana na fikra zao za uhuru huhamasishwa na kuwafanya vijana kuchanganyikiwa na kukimbilia mahusiano haramu ya kimapenzi kwa kutafuta mtu wa kuwa na mahusiano naye hususan katika sikukuu hii.

Takriban nchi nzima, mashule, vyuo, vilabu vya starehe zimo katika maandalizi ya sherehe hizo za sikukuu ya wapendanao. Pia kuwajumuisha Waislamu waliochanganyikiwa. Hii inaonyesha ni jinsi gani umma wa kiislamu ulivyokuwa mbali na fikra yake safi ya kiislamu na hatimaye kukumbatia fikra na mila za kikafiri.

Ni vigumu kufikiria kile ambacho kanisa katoliki kilitaraji kukifikia kwa kutaka kuhifadhi taasisi ya ndoa kwa kuzipinga mila za kipagani na kuanzisha siku ya mtakatifu Valentine! Leo tunaona mahusiano ya kiholela ya kimapenzi yamerudi tena na yamezidi katika jamii na hasa sikukuu hii ya Valentine imekuwa ndio kichocheo kikubwa ambayo matokeo yake ni uzinifu, mimba zisizohitajika, utoaji wa mimba na yote yanayopelekea kuporomoka kwa maadili na kupoteza utukufu/ heshma ya jamii. Je huo ndio ujumbe tunaotarajia kuwafikishia watoto wetu?

Katika Uislamu mahusiano ya kimapenzi baina ya mwanamke na mwanamume yameelezwa wazi na Sheria kupitia utaratibu maalumu ambao ni ndoa pekee. Ibn Masoud amesema kuwa. Mtume (saw) amesema:

“Enyi makundi ya vijana, yeyote mwenye uwezo wa kuoa na aoe, kwani jambo hilo litamsaidia kuinamisha macho yake, na itamuhifadhia sehemu zake za siri kutokana na uchafu wa zinaa.Na asiyeweza kuoa basi na afunge kwani hiyo itakuwa ngao kwake”.

Hukmu za kisheria zinahakikisha kuwa jamii iliyosimama juu ya misingi hiyo itakuwa mbali na uzinifu wa kiholela na itakuwa na mwamko wa kimaadili. Mambo haya yamekosekana katika jamii za kimagharibi na kwa bahati mbaya tunayaona yanafikishwa katika ardhi za Kiislamu pia. Sheri’a inatambua mahitaji na ghariza (hisia za kimaumbile) za wote wanawake na wanaume na ndio maana ikaweka utaratibu maalum katika kuzishibisha ghariza hizo na mahitaji hayo katika utaratibu ambao mwanadamu atapata utulivu wa nafsi yake.

Waislamu tunapaswa kufahamu malengo yetu katika maisha. Kwa kuwa kila kitendo chetu ni lazma kifuatane na Hukmu za Kisheria, kwa kuwa ndio chanzo kitukufu cha mwongozo wetu. Matendo yetu hayo yakiwa ni kwa vitu vidogo vidogo au kwa maamuzi makubwa, katika maisha ya ndani (private) au jamii kiujumla (public). Tunalazimika kutenda kitendo baada ya kufahamu hukmu aliyoiteremsha Allah (swt). Vyenginevyo tutaingia katika makucha ya upotofu, kama vile uhuru, demokrasia, michanganyiko ya jisia tofauti pamoja na maslahi binafsi. Vile vile ikiwa tutachukua taratibu zisizokuwa za kiislamu katika maisha yetu, kwa ajili ya kuwaridhisha wale waliotuzunguuka, lazima tufahamu kuwa kufanya hivyo kutatufanya tuwe madhalili, na starehe zao zitakuwa pigo kwa dini yetu. Allah (swt) anasema:


وَلَنْ تَرْضَى عَنْكَ الْيَهُودُ وَلاَ النَّصَارَى حَتَّى تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ

“Hawataridhia juu yako Mayahudi wala Manaswara mpaka ufuate mila zao…”
Q 2:120).

Ni lazima tuwe macho Waislamu kwani kila wanachokifanya makafiri, iwe katika michezo yao ya sinema (movies) au vitabu vyao vya hadithi na vyenginevyo, wana malengo makubwa dhidi yetu waliyoyaficha katika vifua vyao, ambayo yana athari mbaya kwa ummah wa kiislamu. Ni wakati wa kuamka na kutafuta mamlaka yetu ya dola ya Khilafah katika ulimwengu ili tuonje ladha ya Uislamu kivitendo na kukomesha mila na sherehe potofu za kikafiri.

0 comments/Maoni: